Kikosi cha Azam FC 2012/2013 |
BILIONEA Mrusi, Roman Abramovich aliinunua klabu ya
Chelsea Juni mwaka 2003, kwa dau la pauni Milioni 140 na mara moja akatumia
zaidi ya pauni Milioni 100 kununua wachezaji wapya, wakati huo kocha akiwa
Claudio Ranieri ambaye pamoja na uwekezaji huo mkubwa alishindwa kutwaa taji
lolote na akafukuzwa, nafasi yake akapewa Jose Mourinho.
Na Mahmoud Zubeiry |
Chini ya Mourinho, Chelsea ikawa klabu ya tano England
kushinda mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu, tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia (msimu
wa 2004/2005 na 2005/2006) pamoja na kutwaa ubingwa wa Kombe la FA Cup (2007) na
Makombe mawili ya Ligi (mwaka 2005 na 2007).
Pamoja na hayo, Septemba mwaka 2007, Mourinho aliondolewa
na nafasi yake akapewa Avram Grant, ambaye aliifikisha timu fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza, ambayo walifungwa kwa mikwaju ya penalti na
Manchester United. Naye akafukuzwa.
Mwaka 2009, Kocha wa Muda, Guus Hiddink aliiongoza
timu kutwaa taji lingine la FA na msimu wa 2009/2010, mbadala wake, Carlo
Ancelotti aliiongoza timu kutwaa mataji ya Ligi Kuu na Kombe la FA, na kuweka
rekodi ya kuwa klabu ya kwanza England kufunga mabao 100 katika ligi hiyo tangu
msimu wa 1963.
Lakini Juni mwaka 2011, Ancelotti alifukuzwa na
nafasi yake akapewa Andre Villas-Boas, ambaye naye akafukuzwa Machi mwaka huu.
Wakati wote huo, Abramovich alikuwa anatafuta taji
moja tu, Ligi ya Mabingwa ya Ulaya na alijitahidi kuajiri kila kocha ambaye
aliitwa bora duniani ili kulisaka taji hilo.
Lakini hata AVB, mapema tu hakuonyesha dalili za
kufanya kile kitu ambacho Abramovch alikuwa anataka, naye akafukuzwa na nafasi
yake, akapewa aliyekuwa Msaidizi wake, Roberto Di Matteo, huku Chelsea ikisaka
kocha mwingine wa kudumu.
Lakini kocha ambaye hakupewa nafasi ya kufanya jambo
la maana Chelsea, ndiye ambaye alifanya kile ambacho kilimfanya Abramovich
atumie fedha nyingi kusaka kocha wa kumpa Ligi ya Mabingwa.
Di Matteo aliiwezesha Chelsea kutwaa taji la saba la
FA na ubingwa wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa, akiiwezesha timu kuifunga Bayern
Munich kwa penalti 4–3, The Blues wakiweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya London
kutwaa taji hilo.
Roman aliinunua Chelsea mwaka 2003, ambayo ilianzishwa
1905 na alilazimika kusubiri hadi Mei mwaka huu kushinda taji la Ligi ya
Mabingwa, tena chini ya kocha ambaye alipewa timu amalizie tu msimu wakati
akitafutwa kocha mbadala wa kuiongoza timu.
Kichwa kilimuuma Roman baada ya Chelsea chini ya
mchezaji wake wa zamani, Di Matteo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa akipita
katika reli ngumu, iliyokuwa na vigogo wakiwemo mabingwa watetezi, Barcelona FC
kabla ya kukutana na Bayern katika fainali- na hatimaye akasitisha mpango wa
kuendelea kusaka kocha mpya.
Di Matteo amepewa mikoba kamili ya ukocha Chelsea
hivi sasa na anaendelea na zoezi la usajili katika hatua za mwishoni, akiwa na
jukumu la kuthibitisha msimu ujao kwamba yeye si kocha wa kubahatisha.
Azam FC ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa
kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu
yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam, lengo la wafanyakazi hao wa kampuni
inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya
kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16,
mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne,
wakitumia jina la Mzizima FC na baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa,
Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni
zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd,
Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni
hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye
Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne
na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King,
aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa
zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na
Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin
kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo
katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo
kutoka nje ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache
walioipandisha timu hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’.
Baadaye Itamar alipewa Ukocha Mkuu, baada ya Santos
kutupiwa virago, lakini Itamar naye aliondolewa mwaka jana na nafasi yake akapewa
Muingereza Stewart Hall, ambaye amefanikiwa kuipa taji la kwanza Azam, Kombe la
Mapinduzi Januari mwaka huu na Aprili akaiwezesha kushika nafasi ya pili katika
Ligi Kuu, ikiwapiku vigogo, Yanga.
Azam ambayo kwa kuwa washindi wa pili wa Ligi Kuu
watacheza Kombe la Shirikisho mwakani, mwezi uliopita walicheza fainali za
michuano miwili, na yote wakafungwa na kuambulia nafasi ya pili, nyuma ya
vigogo wa soka Tanzania, Simba na Yanga.
Kwanza ilikuwa fainali ya Kombe la Urafiki
walipofungwa na Simba kwa penalti baada ya sare ya 2-2 na wiki tatu baadaye
wakacheza fainali ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, ambako
walifungwa na Yanga 2-0.
Kufungwa kwenye fainali ya Kombe la Urafiki,
hakukuwaumiza sana Simba SC, lakini kipigo cha Jumamosi kinaonekana kuvuruga
amani kidogo katika klabu hiyo. Kuna tuhuma za hujuma, kwamba wapo baadhi ya
wachezaji walicheza chini ya kiwango kuihujumu timu na hata ukiwasikiliza
baadhi ya viongozi wa timu hiyo, unaweza kuamini moja kwa moja kuna hali hiyo
ndani ya Azam.
Lakini kitu ambacho kinajitokeza kwa haraka ni jinsi
ambavyo Azam imewekeza katika timu yake, kuliko timu nyingine yoyote Tanzania,
lakini bado inashindwa kuongoza katika soka ya nchi hii na ndiyo maana hawataki
kuamini kama wanazidiwa kwa halali na Simba na Yanga.
Lakini wakati mwingine, Azam wanapaswa kuwa makini
sana na watu ambao wamewazunguka, kwa sababu wakati mwingine wanaweza kutumia
mianya kama hii ya timu kupoteza mechi, kupandikiza sumu ndani ya timu, ambayo
mwisho wa siku itawasaidia wao kutimiza malengo yao.
Azam ni timu nzuri na imesajili vizuri mno na
unaweza kuona kwenye Kombe la Kagame, bado kuna wachezaji wazuri wapya kama
George Odhiambo ‘Blackberry’ hawajatumika vizuri. Nataka tu kuwaambia Azam,
mafanikio ambayo wamepata ndani ya miaka minne ya kucheza Ligi Kuu ni makubwa.
Ni kweli Tukuyu Stars walipanda Ligi kuu mwaka 1986
na moja kwa moja kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu, lakini soka ya wakati huo siyo
soka leo- utandawazi umebadilisha mambo mengi sana na unapoambiwa soka
inahitaji mbinu na mipango ili kupata matokeo mazuri, ni zaidi ya masuala ya
kiufundi.
Haya ni mambo ambayo taratibu Azam wanakwenda
wanajifunza, wanazidi kukusanya uzoefu na itafika wakati nao watakuwa magwiji
wa hizo mbinu na mipango, ambayo niseme wazi mimi siiafiki kabisa, kwa sababu
mimi ni muumini wa soka inayozalisha matoeo halisi uwanjani.
Ila kwa kuwa wakubwa wameshindwa kupambana na huo
mchezo mchafu na ili hata timu nyingine zigombee ubingwa, ziweze kupambana na
magwiji nazo lazima ziige. Ukweli ni kwamba soka yetu inachafuka, lakini kama
ndio staili ambayo wakubwa wameiafiki, tutafanya nini?
Namalizia kwa kuwaambia Azam, wasiruhusu wajanja
wakawavuruga, wamefanikiwa kuwa na timu nzuri iliyokaa pamoja muda mrefu.
Wamefanikiwa kuwa na wachezaji wazuri sambamba na makocha pia.
Kama wanahisi kambi yao iliingiliwa, wakubali
matokeo na wajipange wasithubutu kurudia makosa. Simba na Yanga wana kinga zao
za kupambana na hujuma, kuwapa ahadi ya fedha wachezaji wake wakishinda mechi,
naamini Azam wanazidi kujifunza juu ya namna ya kuicheza soka ya Tanzania.
Mrisho Ngassa inawezekana kweli kwa mapenzi yake
aliyoyadhihirisha kwa Yanga akawa hana madhara kwenye mechi dhidi ya timu hiyo,
lakini vipi mechi dhidi ya Simba, au mechi nyingine zote ambazo Azam itacheza
msimu mzima? Ngassa atakuwa hana manufaa?
Azam wanapaswa kutulia kabla ya kufikia maamuzi
mazito, tena ndani ya muda mfupi. Kwa sasa nawaambia, wao ni bora na wakati
utafika watabeba mataji makubwa.
Kocha wa Azam, Stewart Hall kushoto akijadiliana na wachezaji wake wakati wa mapumziko katika moja ya mechi za Kagame |
0 comments:
Post a Comment