Amir Maftah, miongozi mwa wachezaji walioibiliwa kwenye michuano ya Rollingston |
Na Prince Akbar
TIMU 10 za vijana Tanzania Bara zikiwemo Azam FC, Simba na
Yanga, zitashiriki kwenye michuano ya Rollingstone kwa vijana wenye umri chini
ya miaka 20 ambayo mwaka huu itafanyika Makamba nchini Burundi kuanzia Julai 7
mwaka huu.
Jumla ya timu 24 zinashiriki mashindano hayo na zimepangwa
katika makundi sita tofauti. Timu nyingine zinatoka Burundi, Kenya, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Uganda na Zanzibar.
Timu za Tanzania zilizoingia katika mashindano hayo ni Azam,
Bishop High School, Chakyi Academy, Coastal Union, Rollingstone, Ruvu Shooting,
Simba, TAYFA Academy, Yanga na Young Life.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Rollingstone, Issa Karata timu
zote zinatakiwa kwenda vyeti vya kuzaliwa vya wachezaji wake ili kuthibitisha
umri wao. Kamati ya Mashindano itakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu umri wa
mchezaji yeyote.
Kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji 20 na viongozi watano
ambao watagharamiwa na waandaaji kwa huduma za malazi na chakula kwa muda wote
wa mashindano hayo yaliyoanzishwa miaka 13 iliyopita.
Wakati huo huo: Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) imeridhia ombi la Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) kuanza
mchakato wa uchaguzi wake Julai 15 mwaka huu.
DRFA iliwasilisha ombi TFF ili kusogeza mbele kuanza kwa
mchakato huo kwa vile Katiba yao ambayo waliagizwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF
kuifanyia marekebisho kabla ya kuingia kwenye uchaguzi huo bado iko kwa
Msajili.
Awali DRFA ilikuwa ianze mchakato wa uchaguzi Julai Mosi
mwaka huu. Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, mchakato wa
uchaguzi unatakiwa kuchukua siku 40 tangu kuanza kutolewa fomu kwa wagombea
hadi siku yenyewe ya uchaguzi.
Pia Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) kuanza mapema mchakato wa uchaguzi wake.
Sasa mchakato wa uchaguzi wa chama hicho utaanza Septemba Mosi mwaka huu badala
ya Septemba 15 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.
0 comments:
Post a Comment