Wachezaji wa Azam |
Na Prince Akbar
HATIMA ya Azam FC kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Urafiki,
inatarajiwa kujulikana leo, wakati itakaposhuka dimbani kumenyana na Mafunzo
katika mchezo wa mwisho wa kundi A, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Azam ina pointi mbili tu, baada ya kucheza mechi mbili na
kutoa sare zote dhidi ya U23 ya Zanzibar, maarufu kama Karume Boys na Simba SC,
wakati Mafunzo haina hata pointi moja.
Simba inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake nne na leo
itakuwa inamaliza na Karume Boys yenye pointi nne pia.
Azam inatakiwa lazima ishinde na wakati huo huo ikiombea
duwa mbaya Karume Boys ifungwe na Simba, vinginevyo hata yosso hao wa Zanzibar
wakitoshana nguvu na Mnyama, Wana Lamba Lamba wanaweza kuaga.
Kwa sababu hiyo, mechi za leo zinatarajiwa kuwa tamu na za
kusisimua kulingana na kwamba ndizo zitakazoamua timu za kusogea Nusu Fainali.
Jana zilichezwa mechi za Kundi B na Super Falcon iliilaza
Jamhuri ya Pemba bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Super Falcon ilipata bao hilo kupitia kwa Mbarouk Marshed
dakika ya 44, aliyefumua shuti kali na kujaa nyavuni.
Kwa matokeo hayo, Falcon inaongoza Kundi B, kwa pointi zake
tatu, mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa, ikifuiatiwa na Jamhuri yenye
pointi tatu pia, mabao matatu ya kufunga na mawili ya kufungwa. Lakini pointi
hizo Jamhuri ilivuna mbele ya Yanga, ambayo imeenguliwa.
Ikumbukwe kundi hilo, limebaki na timu tatu tu, nyingine
ikiwa ni Zanzibar All Stars baada ya kuondolewa kwa Yanga kwenye michuano hiyo
kwa kitendo chao kupeleka timu B, badala ya timu A.
Katika mechi za awali za Kundi A, Simba SC ilitoka sare ya
1-1 na Azam FC juzi.
Simba ilitangulia kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa
mshambuliaji wake iliyemsajili kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny
Mrwanda, lakini Azam ilisawazisha kupitia kwa George Odhiambo ‘Blackberry’
dakika ya 45.
Abdulhalim Humud alipewa kadi ya pili ya njano na kuwa
nyekundu dakika ya 52 na kutolewa nje, hivyo Azam kubaki pungufu ya mchezaji
mmoja uwanjani.
Katika mechi yake ya kwanza Jumatatu, Simba SC ilianza vyema
baada ya kuifunga Mafunzo mabao 2-1, wakati Azam ililazimishwa sare ya 1-1 na Karume
Boys.
0 comments:
Post a Comment