Kikosi chas Azam FC |
Prince Akbar
KLABU ya Azam FC leo inacheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya mabingwa mara nne, Yanga SC, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam inakuwa klabu ya pili kihistoria, nje ya Simba na Yanga
kucheza fainali ya michuano hiyo, baada ya Moro United mwaka 2006, ambayo
ilifungwa 2-1 na Polisi Uganda, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mbele ya rais
Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa anakimbiza mwaka wake wa kwanza tangu aingie Ikulu.
Hii timu ambayo inakimbiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake
mwaka 2004 na ipo kwenye mwaka wa tano tangu ianze kucheza Ligi Kuu mwaka 2008.
Kocha Muingereza, Stewart Hall wa Azam FC iliyoitoa AS Vita
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuingia fainali, kwa kuifunga
mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na John Bocco ‘Adebayor’ na Mrisho Ngassa, anasema
kwamba Yanga ni timu nzuri na fainali hiyo itakuwa ‘classic’, yaani baab kubwa.
Katika miaka yake mitano ya kucheza Ligi Kuu, nuru ilianza
kumulika kwenye anga zao mapema mwaka huu walipotwaa Kombe la Mapinduzi na
baadaye Aprili, wakakata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika,
wakiwapiku vigogo, Yanga.
Katika dunia ya leo, ambayo napokea mageuzi kisoka, hususan
barani Afrika, timu kama Berekum Chelsea ya Ghana ikisumbua katika Ligi ya
Mabingwa, kuna dalili za kutosha Azam inaelekea huko.
Azam FC, kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar, nayo ilianzishwa
na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya
Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said
Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya
kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka
2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia
jina la Mzizima FC.
Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa,
aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na
kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam
Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika.
Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo
timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11,
mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi
mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King,
aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa
zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na
Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka
Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje
ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu
hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’.
Wakati Azam inapigana kwenye Ligi Daraja la kwanza ili
kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa ina wakongwe kama Shekhan Rashid na Suleiman
Matola, viungo wa zamani wa klabu ya Simba.
Malengo makuu ya Azam ni kuifanya timu iwe ya kulipwa,
wachezaji wakihudumiwa vizuri, chini ya makocha bora, nao waweze kufanya vizuri
na kuitangaza kimataifa timu hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla.
Aidha, kwa kuwa inataka kutambulika kimataifa, ina kitengo
maalumu cha soka ya vijana, kilicholenga kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na
kuwakuza katika misingi na maadili ya mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya.
Mmoja kati ya mabosi wa Azam, Yussuf Bakhresa, ni wakala wa
wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye
anaweza kuwafanya yosso wa klabu hiyo waende Ulaya moja kwa moja.
Kikosi cha kwanza cha Azam Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na
wafuatao; Kassim Kilungo, Said Bakar Nachikongo, Abdul Azizi Hamza, Shaaban
Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’,
Salum Machaku, Shekan Rashid Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo,
Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo, Said Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson
Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou
Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu, John Faustin Mabula,
James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John Nyangwe, Abubakar
Pawasa na Vladimir Niyonkuru.
Azam pamoja na kumilikiwa na kampuni ya bilionea, zaidi ya
basi lake ‘kali’, haina uwanja wake, Azam Complex, uliopo Chamazi, Mbagala, Dar
es Salaam, ambao kwa msimu huu imeshuhudiwa hadi vigogo, Simba na Yanga
wakiutumia kwa mechi zao za Ligi Kuu.
Kwa sasa Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hal. Naam,
hao ndiyo Azam FC, wana Lamba Lamba.
Hivi karibuni, Azam watafanya ziara ya kujiandaa na msimu
mpya Falme za Kiarabu na inawezekana wakaondoka baada tu ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayofikia tamati leo mjini
Dar es Salaam.
Malengo ya Azam ni kutwaa Kombe la Kagame leo na kuhakikisha
mwakani wanacheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho- pamoja na kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara. Hao ndio Azam, wanaoelekea anga za Berekum Chelsea
ya Ghana.
Mashabiki wa Azam FC |
0 comments:
Post a Comment