Kikosi cha Yanga cha ubingwa |
Na Prince Akbar
BAADA ya kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, wachezaji wote wa Yanga walipewa mapumziko kuanzia Jumapili hadi Alhamisi, wote wanatakiwa kuripoti mazoezini kuanza maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kocha Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji amesema atakayechelewa atakuwa anamtafuta ubaya.
“Tunaanza tena mazoezi Alhamisi, kujiandaa na Ligi Kuu, nimeambiwa wachezaji hapa huwa hawazingatii hilo, lakini wakati wanaondoka niliwasistiza na tayari wanajua msimamo wangu katika suala la nidhamu, kwa hivyo atakayekosa Alhamisi, atakuwa ananitafuta ubaya,”alisema Tom.
Tayari Tom amekwishatoa msimamo wake kuhusu michuano ya Bank ABC Super 8 iliyopangwa kuanza Agosti 4 hadi 18, ikishirikisha timu nane, nne za Zanzibar na nne za Bara, kwamba hayuko tayari kuingiza timu yake, kwani anahofia kuwaumiza wachezaji wake.
Yanga iliifunga Azam 2-0 na kutwaa Kombe la Kagame mara mbili mfululizo, baada ya mwaka jana kutwaa taji hilo pia kwa kuifunga Simba SC 1-0 mjini Dar es Salaam pia.
Kwa Tom kuiwezesha Yanga kutwaa hilo, ameendeleza rekodi ya Yanga kutwaa taji hilo, ikiwa chini ya makocha wa kigeni watupu.
Mwaka 1975, Yanga ilitwaa taji hilo ikiwa inafundishwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), 1993, Yanga ilitwaa taji hilo ikiwa inafundishwa na kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ (sasa marehemu), ambao wote baadaye walichukua uraia wa Tanzania.
Mwaka 1999, Yanga ilitwaa taji hilo ikiwa inafundishwa na Raoul Jean Pierre Shungu kutoka DRC na mwaka jana, Watoto hao wa Jangwani, walitwaa taji hilo wakiwa chini ya kocha Mganda, Sam Timbe.
MAKOCHA WALIOLETA KAGAME YANGA:
Mwaka Kocha Alipotokea
1975: Tambwe Leya DRC
1993 Nzoyisaba Tauzany Burundi
1999 Raoul Shungu DRC
2011 Sam Timbe Uganda
2012 Tom Saintfief Ubelgiji
0 comments:
Post a Comment