Kikosi kamili cha Azam 2012, Bocco wa kwanza kabisa kushoto mstari wa nyuma kabisa |
Na Prince Akbar
MSHAMBULIAJI wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amewapoza
mashabiki wa klabu hiyo kwa kuanza na sare ya 1-1 na Mafunzo ya Zanzibar katika
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kwa kusema kwamba
wamejifunza kutokana na na makosa na sasa watapigana kufa na kupona katika mchezo
ujao dhidi ya Tusker ya Kenya.
Bocco ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, mashabiki wa Azam
wanatakiwa kutulia na kuendelea kuiunga mkono timu yao na matokeo mazuri
yanakuja.
“Kwa kweli tumeumia sana kwa sare hii, sisi kama wachezaji
tumesikitika zaidi kuwaumiza mashabiki wetu ambao walitarajia tutashinda, tena
ushindi mnono, lakini jamaa walikamia sana na mchezo ulikuwa mgumu kwa kweli.
Ila tunawaahidi mashabiki wetu, tumejifunza kutokana na
makosa na sasa mechi ijayo na Tusker waje kuona nini tutafanya, yaani akili
hiyo ni ya kila mchezaji, tutapigana kwa nguvu zetu zote ili kujenga imani kwa
mashabiki wetu,”alisema Bocco, mfungaji bora wa Ligi Kuu.
Bocco ndiye aliyeifungia bao Azam katika mchezo huo wa jana
wa sare ya 1-1 na mapema tu alisema anataka kuwa mfungaji bora wa michuano
hiyo.
Katika mchezo mwingine wa jana, URA ya Uganda iliichapa timu
nyingine ya Tanzania, Simba SC mabao 2-0, wakati juzi mabingwa watetezi, Yanga
nao walipigwa 2-0 na Atletico FC ya Burundi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Azam itarejea uwanjani Julai 21, kumenyana na Tusker FC ya
Kenya wakati Yanga itamenyana na Waw Salaam ya Sudan Kusini kesho, mechi
itakayotanguliwa na mchezo kati ya Atletico na APR ya Rwanda, iliyowafunga
Wasudan 7-0 katika mchezo wa kwanza.
Simba watacheza tena keshokutwa dhidi ya Ports ya Djibouti
iliyofungwa 7-0 na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika
mchezo wa kwanza, mechi ambayo itatanguliwa na mchezo kati ya Vita Club na URA
ya Uganda.
0 comments:
Post a Comment