Na Mahmoud Zubeiry |
MWISHONI mwa wiki zilichezwa mechi mbili za kirafiki, watani
wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga wakimenyana na mabingwa wa
Uganda, Express ‘Red Eagles’.
Mechi ya kwanza Jumamosi, Yanga ilishinda mabao 2-1, wakati
mechi iliyofuata Jumapili, Simba ililazimishwa sare ya bila kufungana.
Katika mechi zote mbili, safu za ushambuliaji za klabu hizo
za Tanzania ziliongozwa na washambuliaji wazawa- upande wa Simba Abdallah Juma
na Christopher Edward na kwa Yanga Jerry Tegete na Simon Msuva.
Timu zote zilirundika viungo wengi- lakini angalau Yanga
ilicheza na washambuliaji wawili, Tegete na Msuva, lakini Simba alianza
Abdallah Juma pekee.
Yanga walicheza vema kipindi cha kwanza, ingawa kulikuwa
kuna mapungufu kidogo ambayo yanatokana na dhahiri klabu hiyo kutokuwa na
mwalimu kwa sasa.
Nasema mwalimu, kwa maana ya mwalimu wa kiwango cha juu- kwa
sasa bado ni mapema sana kwa Freddy Felix Minziro kuimudu timu kama Yanga.
Matarajio ya wana Yanga, kocha wao mpya kutoka Ubelgiji,
Thom Saintfiet atawasili leo kusaini mkataba na moja kwa moja kuanza kazi.
Simba, iliyoongozwa na kocha wake Mserbia, Milovan Cirkovick
kama kawaida ilicheza soka yake ya kugonga pasi nyingi na hawakuwa tishio mbele
ya safu ya ulinzi ya Waganda.
SIMBA WAMELAMBA DUME
Lakini bado ilitosha kujua kwamba Simba wamepata
mshambuliaji bora, ambaye kama watampa sapoti ya kutosha, atakuwa siyo tu
tegemeo la klabu yake, bali hata timu ya taifa.
Naomba nisema Abdallah anajua. Abdallah ana umbo zuri. Abdallah
Simba wamelamba dume, kama wataamua kuwekeza kwake.
Nasema kuwekeza kwa sababu, Abdallah ana mapungufu ambayo
yanahitaji kufanyiwa kazi ili baada ya miezi michache awe mshambuliaji ambaye
makipa watalala wanamuota.
Ni mrefu, lakini ni mwembamba sana kwa sababu hana mazoezi
ya kutosha ya kujenga mwili na lishe bora.
Katika eneo hilo, kijana anahitaji kuwekewa programu nzuri
ya mazoezi ya gym na lishe bora.
Anaujua mpira, ana maarifa ya kuwatoka mabeki- lakini kwa
alivyo sasa atakuwa akiwatoka akina Aggrey Morris tu, mbele ya mabeki madhubuti
wa Kaskazini au Magharibi, hatafua dafu.
Kwa nini? Hana mbinu za kutosha na uzoefu pia.
Vinauzwa wapi hivyo? Hakuna popote, bali vinapatikana kwa
njia moja kubwa, kupewa muda wa kuukusanya uzoefu uwanjani, huku kila baada ya
mechi kocha akimuambia mapungufu yake ayafanyie kazi.
Lakini haitakuwa vibaya pia kwa Simba wakiamua kumpa mmoja
wa washambuliaji wake nyota wa zamani kazi ya kuwanoa washambuliaji wao wa
sasa, akiwemo Abdallah ambaye katika taswira yake unaweza kumuona mshambuliaji
bora wa baadaye Tanzania.
Wenzetu katika klabu pamoja na kuwa na kocha Mkuu na
Msaidizi wake, wana makocha wa makipa, mabeki, viungo na washambuliaji pamoja
na wataalamu wa saikolojia.
Lakini sisi tunapenda kurahisisha mno- akiajiriwa Kocha Mkuu
na Msaidizi wake, ukimkuta kocha wa makipa ni bahati na zaidi hiyo imekuja
miaka ya karibuni katika klabu zetu.
Na ndiyo maana kila baada ya msimu vikosi vinajengwa upya
kwa kusajiliwa wachezaji wapya lukuki na inasikitisha miaka inakatika bado
hatujifunzi.
Haiwezekani kila unapowadia muda wa kusajili klabu ibomoe
benki kusajili lundo la wachezaji wapya- lazima ufike wakati tufikirie
kutengeneza timu.
Lazima tuendeshe mambo kitaalamu, tujifunze kuinua viwango
vya wachezaji wetu na si kuwatekeleza kama ilivyo sasa.
Huyu Abdallah kama angetaka kuibukia Simba, basi sasa hivi
zamani amekwishasahaulika katika soka ya nchi hii kama ilivyokuwa kwa Iddi
Mbaga Yanga.
Lakini amepitia klabu mbalimbali, ambako alivumiliwa hadi
kuonekana Simba.
Ila bado Abdallah anakabiliwa na changamoto kubwa hadi
kujihakikishia yeye ni mshambuliaji wa Simba- kwani Felix Sunzu mwenye namba yake
hajarejea. Akirudi Sunzu, akaendelea kuwa kauka nikuvae (kila mechi anacheza
yeye), ina maana mwisho wa msimu Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ atasajili kipya kipya
na Dullah atatolewa kwa mkopo sijui wapi.
Bado kuna Danny Mrwanda, ambao wote anatakiwa kupambana nao
ili kucheza- zaidi ya hapo haitakuwa ajabu naye akifuata nyayo za Mohamed
Kijuso.
Nawaambia kitu kimoja Simba, wawekeze kwa huyo kijana na
baada ya msimu mmoja tu watakuwa na lulu kikosini.
Lakini kwake pia Abdallah, anatakiwa kujitambua, kuwa na
malengo ya kufika mahali fulani. Asijione kuvaa jezi nyekundu yenye nembo ya
Kilimanjaro Beer ndio amemaliza. Hapana, na akiona amemaliza na kweli ataisha
mapema na kusahaulika kabisa.
Siku zote tatizo la wachezaji wengi wa Tanzania ni
kutojitambua na kukosa malengo pia na ndiyo maana hawafiki mbali, wanabaki tu
kushikana uchawi wenyewe kwa wenyewe, eti wanalogana.
Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Kaburu akimfuatilia gym Abdallah Juma. Programu hii inatakiwa kuendelea kwa kijana huyu pamoja na kuhakikisha anapatiwa lishe nzuri. |
Abdallah kama atakuwa na nia ya kucheza zaidi ya Simba,
akijiwekea mikakati anaweza kutimiza ndoto zake, lakini kama anaona hapo
amefika, basi atafika kweli.
TEGETE TUNAUJUA ANAJUA, MSUVA HAKUNA UBISHI…
Nirejee kwa Yanga, safu yao ya ushambuliaji iliongozwa na
Tegete aliyefunga mabao yote mawili na Msuva.
Binafsi najua kama Tegete anajua na kuyumba kwake msimu
uliopita kulitokana na matatizo ya kifamilia yaliyokuwa yanamkabili.
Hapa ndipo unapoonekana umuhimu wa kuwa mtaalamu wa
saikolojia kikosini. Tunaona wanamichezo wakubwa duniani, ambavyo hupoteza
mwelekeo kutokana na matatizo ya kifamilia.
Tiger Woods, mchezaji gofu bora kihistoria duniani, aliyumba
mno mwaka juzi alipokuwa katika matatizo ya aina hiyo- kadhalika Wayne Rooney,
hivyo hata wachezaji wetu nao ni binadamu kama akina Ryan Giggs.
Lakini unaweza kuona Tegete sasa akili imetulia anafanya
mazoezi kwa juhudi na anajutia muda alioupoteza.
Naamini Tegete amerudi kama tu ilivyo kwa Athumani Iddi
‘Chuji’- lakini pia niseme, Yanga imelamba dume kwa Msuva. Dogo anajua na hii inaashiria
kwamba akina John Bocco, Mbwana Samatta, Hussein Javu wana changamoto nzuri
sana ya kukomaa kutetea namba zao timu ya taifa.
Kama Samatta, Bocco na Javu ndio washambuliaji wa Taifa
Stars na wakati huo huo, Abdallah Juma, Tegete na Msuva wanafanya vizuri-
dhahiri kocha Kim Poulsen atakuwa anakenua tu.
Kuwa na washambuliaji wasiopungua watano wa kiwango cha
kimataifa- ni jambo la kujivunia kwa kocha yeyote wa timu ya taifa duniani.
Nimalizie kwa kusema; wakati umefika klabu za Tanzania
kuliko kukimbilia wachezaji wa kigeni, kwanza zifikirie kuwekeza kwa wachezaji
wetu wazawa.
Hata wakati ule Taifa Stars ina washambuliaji tishio kibao, akina
Fumo Felician, Kitwana Suleiman wote kutoka Pamba, Edward Chumila, Malota Soma
wote wa Simba, Said Mwamba ‘Kizota’, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ wa Yanga,
kutoka Tanga alikuwa anakuja Razack Yussuf
‘Careca’ na Juma Mgunda wakati huo ni kwamba kazi ilifanyika.
Kulia ni Tegete, anayemfuatia Msuva, wakipongezwa na Nizar Khalfan kwa kazi nzuri |
Viongozi wa klabu walikuwa hawaendi kutafuta wachezaji nje
ya nchi- walikuwa wanawatengeneza hapa hapa. Mwaka 1992, katika Kombe la
Challenge Bara ilikuwa ina timu mbili, Victoria 92 na Kakakuona iliyofika
fainali.
Hata leo hiyo inawezekana, ikiwa klabu zitaamua kuwekeza
wachezaji wazawa. Haitoshi tu kumsajili mchezaji na kumuingiza katika timu,
lazima awekewe mipango ya kuendelezwa na bila hivyo tutaendelea kubahatisha
bahatisha tu kama ilivyotokea kwa Samatta. Wasalaam, Bin Zubeiry!
0 comments:
Post a Comment