Nizar Khalfan, moja ya silaha mpya Yanga |
KLABU bingwa Afrika Mashariki na Kati, Yanga kesho asubuhi inatarajiwa
kuanza mazoezi ya ufukweni katika ufukwe wa Coco Beach, Dar es Salaam ili
kuwajengea stamina wachezaji wake.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia BIN
ZUBEIRY asubuhi hii kwamba baada ya programu ya mazoezi ya ufukweni, wachezaji
hao watapelekwa gym na baada ya hapo wataingia kambini moja kwa moja wiki ijayo.
Yanga inajiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Julai
14 hadi 29, mwaka huu ikishirikisha timu nyingine mbili za Tanzania, bingwa wa
Ligi Kuu, Simba SC na washindi wa pili, Azam FC.
Tayari wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga wamekwishaanza
mazoezi Uwanja wa Kaunda, akiwemo kipa wa Simba, Ally Mustafa ‘Barthez’, Said
Bahanuzi na Juma Abdul, wote kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro na Nizar Khalfan
aliyekuwa akichezea Philadelphia Union ya Marekani.
Wachezaji wa zamani ambao hadi sasa wamekwishafika Jangwani
ni Juma Seif ‘Kijiko’, ambaye kulikuwa kuna tetesi anakwenda Simba, Hamisi
Kiiza, Kenneth Asamoah, Yaw Berko, Shamte Ally, Jerry Tegete, Stefano Mwasyika,
Godfrey Taita, Athumani Iddi ‘Chuji’, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Idrisa Senga, Omega Seme na Ibrahim Job.
0 comments:
Post a Comment