Yanga wakijifua ufukweni |
Na Prince Akbar
SAA chache baada ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC
kuthibitisha kushiriki michuano ya Ujirani Mwema, inayoandaliwa na Chaam cha
Soka Zanzibar (ZAF), watani wao wa jadi, Yanga SC wameamua kujitoa.
Mapema leo, Ofisa Habari wa Simba SC, aliiambia BIN ZUBEIRY
kwamba watashiriki michuano hiyo, kufuatia
majadiliano baina ya uongozi, benchi la ufundi na Kamati ya
Ufundi ya Simba.
“Tumeamua kushiriki kwa sababu tumeona haitakuwa vema kujitoa
wakati watu wa Zanzibar wametupa heshima kubwa ya kutualika kwenye michuano
hii. Kombe la Ujirani Mwema lina maana kubwa kwa sasa kutokana na hali halisi
ya kisiasa na kijamii iliyopo visiwani humo kwa sasa,” alisema Kamwaga katika
taarifa yake, akimnukuu Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’.
Saa chache zilizopita, BIN ZUBEIRY imezungumza na Ofisa
Habari wa Yanga, Louis Sendeu ambaye amesema wao hawawezi tena kwenda kushiriki
kwa sababu wanahofia wachezaji wao kuumia kabla ya michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
“Mara nyingi tunapokwenda kwenye michuano ya Zanzibar,
wachezaji wetu huumia, hivyo tunahofia hilo lisijitokeze wakati tuna wiki mbili
tu kabla ya kuanza kutetea Kombe la Kagame,” alisema Sendeu.
Wakati michuano ya Ujirani Mwema inatarajiwa kuanza Jumapili
visiwani Zanzibar, Yanga ikipangwa kufungua dimba na Jamhuri ya Pemba jioni ya
siku hiyo, Kombe la Kagame linatarajiwa kuanza Julai 14, Yanga ikifungua dimba
na Atletico ya Burundi.
Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, awali
walisema watacheza michuano hiyo, wakati Simba walikataa kuthibitisha mapema
hadi wajadiliane.
Wapembuzi wa mambo wanasema timu hizo, zinaogopa kukutana
mapema kukiwa kuna uwezekano wa kukutana pia kwenye Kombe la Kagame, kutokana
na jinsi ambavyo CECAFA huchezesha ‘karata’ zake.
Yanga walikubali kushiriki awali, baada ya kuwasikia Simba
wakisema hawawezi kuthibitisha mapema na bila shaka taarifa za mabingwa wa
Kagame kujitoa kwenye michuano ya Ujirani Mwema ziliwavujia mapema Wekundu wa
Msimbazi ndio maana wakathibitisha kushiriki.
Na haitakuwa ajabu, Yanga ikisema imebadilisha uamuzi wake
na kuamua kushiriki michuano hiyo, Simba wakasikika wakisema wanajitoa.
0 comments:
Post a Comment