Na Mahmoud Zubeiry |
YANGA inasifiwa kufanya usajili mzuri kwa ajili ya msimu
ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, miongoni mwa wachezaji iliyowasajili
wakiwemo Kelvin Yondan, Ally Mustafa ‘Barthez’ kutoka Simba na Frank Damayo
kutoka JKT Ruvu.
Kulingana na hali halisi ya uwezo wa wachezaji hao kwa sasa,
hususan Yondan, wenyewe wanamuita Vidic na Damayo, mashabiki wa Yanga
wamesuuzika mno na nafsi zao. Wanaamini wachezaji hao na wengineo, wataifanya
timu yao iwe tishio msimu ujao.
Yanga sasa wana ndoto nyingi sana juu ya timu na japokuwa
mwakani hawatashiriki michuano ya Afrika, lakini wanaona kabisa wamekwishatetea
Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Yanga tayari wa ndoto za kulipa zile 5-0 walizopigwa na
watani wao wa jadi, Simba msimu huu. Wanaota kurejesha ubingwa wao wa Ligi Kuu
na kwa ujumla heshima yao katika soka ya Tanzania, waliyoipoteza msimu uliopita.
Kwa ujumla wana matumaini makubwa sana, hasa wakizingatia
Mwenyekiti wao atakuwa Yussuf Manji, Makamu wao Mwenyekiti Clement Sanga na
Wajumbe kama Abdallah Bin Kleb, Peter Haule na wengineo- wana Yanga, wana
matumaini makubwa sana na kikosi chao kipya.
Lakini pamoja na ukweli huo, kuna mambo ambayo wana Yanga
wanatakiwa wayatambue, kubwa ni kwamba; Kusajili wachezaji wazuri ni suala moja
na kuwa na timu nzuri ni suala lingine.
Yanga wamefanikiwa mtihani wa kusajili wachezaji wazuri, na
sasa wanatakiwa wapitiE katika zoezi gumu zaidi la kutengeneza timu nzuri ya
ushindani kwa mashindano ya ndani na nje.
Bahati nzuri, Yanga wana muda wa kutosha kwa sababu msimu
wote ujao utakuwa wa kutengeneza tu timu yao kwa kuwa hawashiriki michuano ya
Afrika- hivyo kama watafanikiwa kufuzu na mtihani huo pia, tegemea kabisa Yanga
ya 2014 itakuwa tishio hadi Afrika.
Lakini hiyo timu nzuri inatengenezwaje? Kwanza kuwa na
mwalimu bora, atakayepeta fursa na wasaa mzuri na wa kutosha wa kuwaandaa
wachezaji. Haitoshi tu kusajili wachezaji wazuri na kisha unawakabidhi kwa
msimamizi wa mazoezi, ni hatari kwa vipaji vyao.
Yondan mazoezini Yanga |
Yanga wanatakiwa kutengeneza sera nzuri za benchi la ufundi,
ambalo litakuwa na nguvu na kuheshimiwa na wachezaji, tofauti na ilivyo hivi
sasa, mchezaji anamuheshimu Seif Magari, anamdharau Freddy Felix Minziro.
Yanga inatakiwa kuwa wazi kwa wachezaji wake, kuwaambia
imewasajili kwa ajili ya kufanya kazi na wasilewe sifa na kuanza kupandisha
mabega juu, uwanjani hawajitumi, matokeo yake wanarudi kule kule, kwenye
kununua mechi.
Haiwezekani, usajili huu wa Yanga naomba niseme mapema
ulikuwa makini mno, tofauti na usajili wa miaka miwili, mitatu iliyopita na
timu iliyopewa jukumu hilo, ililifanikisha kwa umakini wa hali ya juu.
Kwa sababu hiyo basi, wachezaji lazima wacheze soka
uwanjani, watengeneze matokeo mazuri kwa uwezo wao. Wadumishe viwango vyao, ili
waendelee kuwapo timu ya taifa. Lakini kubwa na la msingi ni mashabiki wa Yanga
kuwa na subira kabla ya kupata timu nzuri.
Yanga watawaona wachezaji wao wazuri katika Kombe la Kagame
na watafanya sana vitu adimu binafsi na ikibidi, kweli watatetea hadi Kombe
lao- lakini kuwa na timu nzuri kwa maana ya timu inayocheza soka ya kuelewana,
iliyotokana na mafundisho, wana Yanga wanatakiwa kuwa na subira.
Kama watapata mwalimu mzuri, naamini akipata fursa na wasaa
mzuri na wa kutosha, kuanzia mzunguko wa pili Yanga itakuwa inacheza ‘kitenisi’
cha kutisha- ila kama ubabaishaji utaendelea na hakutakuwa na sera nzuri za
benchi la ufundi, mafunzo, nidhamu na kujali maslahi ya wachezaji, basi wachezaji
hawa Desemba tu wataonekana hawafai. Alamsiki!
Wachezaji wa Yanga mazoezini, Jerry Tegete kushoto na Godfrey Taita |
0 comments:
Post a Comment