Na Prince Akbar
KAMATI ya Uchaguzi ya klabu ya Yanga ya Dar es Salaam,
imewaengua wagombea wawili, Jamal Kisongo na Abdallah Sharia katika uchaguzi
Mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Julai 15, mwaka huu baada ya usaili
uliofanyika leo makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani.
Katibu wa Kamati hiyo, Francis Kaswahili, ameiambia BIN
ZUBEIRY usiku huu kwamba Kisongo na Sharia walioomba nafasi za Ujumbe
wa Kamati ya Utendaji, wameenguliwa kwa sababu hawakufika kwenye usaili bila ya
taarifa yoyote.
Kaswahili alisema Kamati ya Uchaguzi, chini ya Mwenyekiti
wake, Jaji John Mkwawa imepitisha wagombea 27 katika nafasi tatu, Ujumbe
wagombea 20, Makamu Mwenyekiti watatu na Uenyekiti wane.
Wagombea wakisubiri muda wa kuingi chumba cha usajili, kushoto ni Abdallah Bin Kleb |
Mapema juzi, Kamati hiyo ambayo Makamu wake Mwenyekiti mtoto
wa rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Ridhiwani,
ilimuengua mgombea mmoja wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Ally Mayay
Tembele, kwa sababu hakufika kusikiliza
pingamizi alilowekewa.
Wagombea Uenyekiti waliopitishwa baada ya zoezi hilo
lililodumu kwa siku nzima leo Jangwani ni Yussuf Mehboob Manji, John Jambele,
Edgar Chibura na Sarah Ramadhani, wakati wagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti waliopitishwa
ni Ayoub Nyenzi, Yono Kevela na Clement Sanga na wote watafanyiwa usaili leo.
Katika nafasi nne za Ujumbe waliopitishwa ni Lameck
Nyambaya, Ramadhani Mzimba ‘Kampira’, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Said, Edgar
Fongo, Beda Simba, Ahmad Gao, Mussa Katabaro, George Manyama, Aaron Nyanda,
Abdallah Bin Kleb, Omary Ndula, Shaaban Katwila, Jumanne Mohamed Mwammenywa,
Abdallah Mbaraka, Peter Haule, Justin Baruti.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, Mfanyabiashara
Muzamil Katunzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eliakhim Masu walichukua
fomu za kugombea Ujumbe lakini wakashindwa kurudisha, wakati Isaac Chanzi pia
hakurudisha fomu ya Makamu Mwenyekiti hivyo moja kwa moja hao hawamo katika
kinyang’anyiro.
Uchaguzi huo, unaokuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya
Utendaji katika uongozi uliokuwa madarakani, akiwemo Mwenyekiti Wakili Lloyd
Baharagu Nchunga na Makamu wake, Davis David Mosha kujiuzulu utafanyika Julai
15, mwaka huu Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment