MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meckysadik amewataka
wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuhakikisha
wanadumisha viwango vyao kama wachezaji wa nchi nyingine, badala ya desturi
iliyozoeleka ya wachezaji wa nchi hii ‘kufulia’ mapema kisoka.
‘Bosi’ huyo wa Jiji la Dar es Salaam, ameyasema hayo mchana
wa leo kwenye hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, Kariakoo katika hafla fupi
ya kuwaaga wachezaji wa Taifa Stars na kuwakabidhi bendera kwa ajili ya mchezo
wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani
nchini Afrika Kusini, dhidi ya Msumbiji Jumapili mjini Maputo.
“Nawaomba mjitahidi kudumisha viwano vyenu kama ilivyo
wachezaji wa wenzetu, wanacheza mpira kuanzia wana miaka 18 na wanaendelea hadi
wakifika miaka 30, sasa naomba na nyinyi iwe hivyo, siyo kama ilivyo sasa,
mchezaji wa Tanzania anaibuka, baada ya mwaka mmoja au miwili anapotea,”alisema.
Pamoja na hayo, kuelekea mchezo huo na Msumbiji Jumapili,
ambao Stars inatakiwa itoke sare ya 2-2 au zaidi ili kusonga mbele, baada ya
awali kulazimishwa sare ya 1-1 na Mambas mjini Dar es Salaam, Mkuu huyo wa Mkoa
amewataka Stars wakapiganie ushindi.
“Mimi huwa sipendi haya mambo ya kupigiana mahesabu, siyo
mazuri. Kama sasa hivi kwenye Euro 2012 kuna timu zinapigiana mahesabu, kwa
sababu zimelingana kila kitu. Mimi ninataka mkashinde, kapiganieni ushindi,”alisema
Meckysadik.
Mapema, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar
Chillah Tenga aliwaambia wachezaji wa Taifa Stars kwamba, mwanafunzi mzuri ni yule
anayeendelea kujifunza kila siku kwa juhudi na si yule anayejiona tayari amejua
na kubweteka.
Kwa sababu hiyo, Tenga akawataka Stars wakacheze kwa juhudi
zaidi Msumbiji na si kujiona wamefuzu baada ya kuifunga Gambia, mabao 2-1
Jumapili katika mchezo wa Kundi C, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe
la Dunia mwaka 2014.
Kwa upande wake, kocha wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulesen
amesema kwamba wanaelekea kwenye mchezo mgumu, lakini watapigana kwa juhudi kupata
ushindi, ili kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya makundi katika kuwania tiketi
ya Afrika Kusini 2013.
Poulsen ambaye huo, utakuwa mchezo wake wa nne tangu aanze
kazi akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen baada ya awali kuiongoza
timu hiyo katika sare ya 0-0 na Malawi Dar es Salaam, kichapo cha 2-0 kwa Ivory
Coast mjini Abidjan na ushindi wa 2-1 na Gambia, amesema vijana wake wanaendelea
kuimarika kila kukicha na ana matumaini nao makubwa.
Anasikitika tu jana kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’
aliumia mazoezini, ingawa amesema anaendelea na matibabu na wataenda naye
Msumbiji.
Kwa upande wake, Nahodha Juma Kaseja alisema kwamba wanatambua
ugumu wa mchezo huo kwao, lakini watakwenda kupigana ‘kufa na kupona’. Kaseja amesema
kwamba soka siyo tufe kwamba kila siku liko vile vile, bali inabadilika na sasa
timu yao imebadilika mno na Watanzania watarajie matokeo mazuri Jumapili.
0 comments:
Post a Comment