![]() |
Kempes enzi zake |
WENGI wanaamini vipaji vya wanasoka wa zamani huwezi kuviona
katika dunia ya leo, hasa upande wa washambuliaji, ingawa wanasoka wa siku hizi
wanavuna fedha nyingi kuliko wakali wa enzi hizo.
Vyombo vya habari vinawapamba sana ,
lakini bado wapembuzi yakinifu wanaamini hawawezi kufanya mambo kama yaliyowahi kufanywa na magwiji wa enzi hizo.
Lionel Messi ni mzuri na ndiye mwanasoka bora wa dunia,
lakini kumbuka vitu vya Diego Maradona na toa jibu la swali; nani mkali kati ya
Waargentina hao?
Kutoka taifa hilo hilo wanalotoka wakali
hao wawili, amewahi kutokea mwanasoka mwingine mkali ambaye dunia haipaswi
kumsahau, huyo si mwingine zaidi ya Mario Alberto Kempes.
Mkali huyo alizaliwa Julai 15, 1954 Bell Ville, Córdoba, ni
mwanasoka wa zamani wa Argentina .
Baba yake Mario naye alikuwa mchezaji, hivyo alimvutia kucheza soka kuanzia
akiwa mdogo. Akiwa na miaka saba, alianza kucheza soka katika timu za watoto na
alipotimiza miaka 14 alijiunga na klabu ya La Cuarta de Talleres. Alijipatia
umaarufu zaidi alipochezea klabu ya Valencia
na kuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Argentina kilichoshinda michuano ya
Kombe la Dunia mwaka 1978.
Kempes alikuwa na majina ya utani kama El
toro na El Matador. Katika kipindi chake cha kwanza na Valencia
alishinda tuzo ya ufungaji bora kwa kufunga mabao 24 msimu wa 1976-77 na mabao
28 msimu wa 1977-78. Maisha yake ya soka yalianzia katika klabu ya mjini kwao
ya Instituto kabla ya kujiunga na Rosario Central, ambako alifunga mabao 85 katika
mechi 105, akidhihirisha kwamba yeye ni mfungaji mbao wa hatari, jambo
lililomsaidia ajiunge na Valencia, akiwa Valencia alishinda taji la Copa del
Rey, Kombe la Washindi barani Ulaya na taji la UEFA Super Cup. Alikuwa
akijulikana na kwa tabia yake ya kujituma zaidi awapo uwanjani, alikuwa na
tabia ya kupiga mashuti akiwa nje ya eneo la hatari pia uwezo wa kukimbia na
mpira kuingia golini, na hakuwa na hakuwa na tabia kama washambuliaji wengine
ya kukaa ndani ya eneo la hatari bali alikuwa akizunguka kila upande. Wengi
walikuwa wakipata tabu sana
kumkaba kutokana na staili yake ya uchezaji.
![]() |
Kempes akishangilia moja ya mabao yake enzi zake |
Kabla ya Kombe la Dunia la mwaka 1978, Kempes alikuwa ndio
mchezaji pekee wa Argentina
aliyekuwa akicheza nje ya nchi katika kikosi Kocha César Luis Menotti, kipindi
hicho alikuwa akicheza Hispania katika klabu ya Valencia
wakati wachezaji wengine wote katika kikosi cha Argentina walikuwa wakicheza
nyumbani. Kocha alimuelezea wakati akitaja kikosi kwa ajili ya michuano ya
Kombe la Dunia la mwaka 1978 kwa kusema, “Ana nguvu, uwezo wa kuchezea mpira,
anajua kutengeneza nafasi na anapiga mashuti makali. Ni mchezaji atakayeongeza
kitu katika kikosi na anaweza kucheza kama
mshambuliaji wa kati.”
Wakati akiitwa kwenye kikosi cha timu hiyo, Kempes alikuwa
ametoka kuwa mfungaji bora katika ligi kuu ya Hispania (La Liga) kwenye misimu
miwili iliyopita na alikuwa amedhamiria kuwaonyesha mashabiki wa soka wa nchi
yake kwamba anaweza kufanya makubwa kwenye michuano mikubwa ya soka ulimwenguni.
Hata hivyo, mwaka 1974, akiwa na umri wa miaka 20 alishindwa kufunga bao hata
moja kwenye michuano hiyo iliyofanyika Ujerumani Magharibi na hata baada ya
mechi za hatua ya makundi kumalizika katika michuano ya Mwaka 1978 alikuwa bado
hajafunga bao hata moja katika michuano hiyo.
Katika maisha yake ya soka alifanikiwa kuichezea Argentina
katika michezo 43 na kufunga mabao 20. aliiwakilisha nchi yake katika michuano
mitatu ya Kombe la Dunia ile ya mwaka 1974, 1978 na 1982, na kuafanikiwa
kushinda michuano hiyo mwaka 1978 huku akifunga mabao sita katika michuano hiyo
yakiwemo mawili katika mechi ya fainali. Pia aliwahi kufunga mabao muhimu
katika maisha yake ya soka ngazi ya kimataifa.
Mwaka 1978 alishinda tuzo ya Mchezaji bora wa mwaka wa
Marekani Kusini, utoaji wa tuzo hiyo ulifanyikia Caracas , Venezuela .
Alitajwa katika orodha ya Pele ya wachezaji bora 125 ambao bado wapo hai Machi
2004.
![]() |
Kempes wa sasa |
Kempes alianza kufundisha soka kwa mara ya kwanza nchini Albania .
Wakati akifundisha klabu ya Lushnja ya Albania
aliweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza wa kigeni kusajili mchezaji wa kigeni
katika historia ya soka la Albania .
Maisha yake ya ukocha nchini Albania
hayakuwa marefu yalifikia tamati mwaka 1997. Mwaka uliofuata alipata kazi ya kufundisha
klabu ya Mineros de Guayana ya Venezuela .
Mwaka 1999, Kempes alihamia Bolivia
na kufundisha klabu ya The Strongest, kabla ya kujiunga na klabu ya Blooming mwaka
2000. Kabla ya hapo aliwahi kufanya kazi kama kocha msaidizi wa Héctor Núñez katika
klabu ya Valencia , pia
aliwahi kuwa kocha mchezaji wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Indonesia ,
Pelita Jaya. Alitangaza kustaafu soka mwaka 1996 akiwa na umri wa miaka 41.
Kwa sasa anafanya kazi kama
mchambuzi na mtangazaji wa soka katika kituo cha ESPN idhaa ya Kihispaniola. Huyo
ndiye Mario Alberto Kempes, mtambo wa mabao ulioipa Argentina Kombe la Dunia
mwaka 1978.
WASIFU WAKE:
JINA: Mario Alberto Kempes
KUZALIWA: Julai 15, 1954 (Miaka 56)
ALIPOZALIWA: Argentina
NAFASI: Mshambuliaji
TIMU ALIZOCHEZEA:
Mwaka Timu
1970–1973 Instituto
(Mechi 13, mabao11)
1974–1976 Rosario
Central (Mechi 107, mabao 85)
1977–1981 Valencia
(Mechi 142, mabao 95)
1981–1982 River
Plate (Mechi 29, mabao 15)
1982–1984 Valencia
(Mechi 42, mabao 21)
1984–1986 Hércules
(Mechi 38, mabao 10)
1986–1987 First Vienna (Mechi 20, mabao 7)
1987–1990 St.
Pölten (Mechi 64, mabao 24)
1990–1992 Kremser
SC (Mechi 39, mabao 7)
1995 Fernandez
Vial (Mechi 11, mabao 5)
1996 Pelita
Jaya
(Tangu mwaka 1973 hadi 1982, aliichezea Argentina mechi 43
na kuifungia mabao 20)
0 comments:
Post a Comment