16 Juni, 2012 - Saa 21:24 GMT
NAHODHA wa Ugiriki, Giorgios Karagounis, alifunga bao ambalo liliwashangaza mashabiki wengi wa soka wanaofuatia mechi za Euro 2012, kwa kufanikiwa kuiondoa Urusi katika mashindano hayo kwa bao hilo moja.
Hivyo basi Ugiriki, mabingwa wa mwaka 2004, wameingia robo fainali ya mwaka huu, na kuwa miongoni mwa timu nane zilizosalia katika michuano hiyo.
Katika mechi ya Jumamosi iliyochezwa wakati mmoja na ile kati ya Czech na Poland ili kuepuka timu kupanga matokeo, Urusi iliweza kuutawala mchezo vyema, kabla ya Karagounis kuitumia vyema nafasi iliyojitokeza, kufuatia kosa la mchezaji wa Urusi, Yuri Zhirkov, na kuiandikishia Ugiriki bao kupitia mkwaju wa chini kwa chini.
Awali Urusi walidai penalti ambayo mwamuzi aliikataa, baada ya Roman Shirokov kulalamika alisukumwa na Karagounis.
Karagounis baadaye katika mechi hiyo pia alidai walistahili penalti, lakini mwamuzi akalikataa ombi hilo.
Mkwaju wa freekick wa Giorgos Tzavellas ulikaribia kuiwezesha Ugiriki kufunga tena, lakini mechi ikamalizika kwa bao 1-0.
0 comments:
Post a Comment