Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti, Frank Sanga |
Sanga akiwa na Nahodha wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira |
HIVI sasa timu za soka ziko katika mapumziko na huku zikihaha kufanya usajili wa kuimarisha vikosi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Kama kawaida kipindi cha usajili huwa kina vituko vingi, kutokana na ukweli kuwa masuala ya fedha zaidi ndiyo yanayoendelea. Yaani usajili wa timu nyingi haufanywi kwa kuzingatia matakwa ya kocha bali kwa kutilia mkazo mapenzi ya mfadhili wa timu. Timu zinatakiwa kuandaa bajeti kubwa za usajili na pia wachezaji nao watakuwa wanasaka timu na donge nono. Tunapenda kushauri timu zinazoshiriki kwenye ligi hiyo kufanya usajili makini ili kupandisha kiwango chao cha Ligi Kuu. Inasikitisha kuona katika miaka ya karibuni, ligi imekuwa na ushindani baina ya timu za Simba , Yanga pia Azam, ambayo imeibuka siku za karibuni. Timu kama za Mtibwa na Kagera Sugar ambazo zina miundombinu, ungetegemea kuwa zingetoa ushindani lakini viongozi wake wanakosa malengo ya kupandisha viwango vya timu zao. Kutokana na ukweli kuwa zina miundombinu kama ya viwanja na pia timu hizo zinamilikiwa na makampuni lakini zimegeuka kuwa wasindikizaji tu wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Pia msimu ujao kutakuwa na lundo la timu za majeshi ya ulinzi na usalama, ambazo kwa rasilimali walizonazo ungetegemea zitatoa ushindani mkali lakini wapi. Katika nchi nyingi duniani, taasisi za jeshi huwa ndiyo chachu ya maendeleo ya michezo lakini kwa Tanzania ni hadithi tofauti. Angalia timu maarufu za soka za jeshi FAR ya Morocco, APR ya Rwanda, 105 FC ya Gabon, Chapungu ya Zimbabwe na BDF ya Botswana. Timu kama JKT Ruvu imejizolea sifa ya kuzikamia Simba na Yanga, lakini inapokutana na timu nyingine basi inafanya vibaya na kujikuta mara nyingi haikamati nafasi za juu za ligi. Inashangaza kuona licha ya kuwepo kwa makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwepo katika nchi nzima lakini bado timu za jeshi hilo zimekuwa zikiboronga kila mara. Viongozi wa michezo wa JKT wameshindwa kutumia vizuri mtandao mkubwa wa jeshi hilo ili kunoa vipaji na kutengeneza timu kali. Kuna mzaha mwingi unafanywa katika usajili na timu mbalimbali zinazoshiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara. Mathalani timu zilizopanda daraja zitakachofanya zitanyakua wachezaji wa timu ambazo zilishuka daraja. Ni mara chache kukuta timu inafanya utafiti wa kutosha na kusajili wachezaji wenye vipaji kutoka katika nchi nzima. Ndipo hapo unajiuliza hivi kweli mtu aliyezuia kufanyika kwa Michezo ya Majeshi alikuwa na matatizo gani? Mathalani mkoa wa Kigoma unasifika kwa miaka mingi unasifika kwa kutoa wachezaji wenye vipaji na maumbile yanayowafanya wawe wachezaji wazuri. Katika miaka ya nyuma, timu zilikuwa zinaweka mkazo katika kusaka wachezaji wa maeneo yao, kila mtu anakumbuka timu kama Mseto ya Morogoro, Pamba ya Mwanza, Tukuyu Stars, Majimaji ya Songea, Milambo ya Tabora, TPC na Ushirika za Moshi zilivyokuwa zimesheheni wachezaji kutoka katika maeneo yao. Sasa cha kushangaza ni kuwa unakuta timu ya Shinyanga imepanda daraja lakini itakuja kwa bidii zote kusaka wachezaji jijini Dar es Salaam. Tunashauri kuwa timu zifanye usajili makini ili kuhakikisha msimu ujao ligi inakuwa na mvuto na sio kuwa na mechi nyingi ambazo hazina msisimko. Mathalani kinachoendelea katika timu ya Yanga ni kama mchezo wa kuigiza kutokana na ukweli, kwani wako bize katika usajili pamoja na ukweli hawana viongozi wala kocha. Kuna ombwe la uongozi baada ya Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kujiuzulu, sasa timu iko chini ya sekretarieti na Baraza la Wazee. Utashangaa sasa wako bize wanasajili wakati bado hawajapata kocha na hata wakimpata hawatajua hata atatumia mfumo gani wa uchezaji. Ni vizuri kwa timu kusajili kwa kutumia matakwa ya kocha kwani huwezi kujua mfumo wa wachezaji anaotumia kama ni kushambulia au kujihami. Bahati mbaya ukiachia Simba na Azam, hakuna timu ambazo zina programu za kuandaa vijana yosso, ambao ndio msingi mzuri wa kutengeneza timu kali. Ukiwa na timu nzuri ya watoto na ukifanya usajili makini kwa vyovyote vile kutaimarisha ligi kwani kama soka maridadi inapigwa watu watajaa uwanjani kutokana na ukweli kuwa Watanzania wanapenda soka. Pia kuna fasheni ya kusajili wachezaji wa kigeni, klabu pia zinatakiwa kuleta mastaa wa kigeni wanaotoa changamoto kama tulivyoshuhudia kwa Emmanuel Okwi na Felix Sunzu wa Simba, Hamisi Kiiza na Yaw Berko wa Yanga, Kipre Bolou na Kipre Tcheche wa Azam, Salamsasa Obinna wa African Lyon na Enyinna Darlington wa Toto African, ambao wamefanya vizuri kwenye ligi iliyomalizika. Tusiruhusu ligi kuwa dampo la wachezaji wa kigeni bali tuwe na mipango madhubuti ya kukuza vipaji kuanzia chini. SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI |
0 comments:
Post a Comment