Wachezaji wa Simba SC, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege usiku huu |
KIKOSI cha Simba SC kilichokuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara
mechi mbili za kirafiki kimerejea Dar es Salaam usiku huu kwa ndege ya Shirika
la ATC na kesho kinatarajiwa kuendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe,
kwa ukamilifu zaidi, kwa maana ya wachezaji wote kuanza kazi.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kuwasili Uwanja
wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 2:40 usiku huu, Kocha Msaidizi wa Simba
SC, Hamatre Richard alisema kwamba ziara ilikuwa nzuri na timu ilicheza vizuri mechi
zote.
Hamatre ambaye ni Mganda aliwasifia wachezaji wapya wakiwemo
kipa Hamadi Waziri na viungo Kiggi Makasy na Salim Kinje kwamba walionyesha
kiwango kizuri na anaamini wataisaidia timu msimu huu.
Aliwasifia pia wachezaji vijana waliopandishwa kutoka timu B
kwamba walionyesha soka safi na anaamini watafika mbali. Lakini katika ziara hiyo
Hamatre pia alivutiwa na kiwango cha hali ya juu, kilichoonyeshwa na kiungo
Uhuru Suleiman.
“Uhuru alikuwa Nahodha wa timu katika ziara yetu na kwa
kweli alicheza vizuri mno mechi zote na alifunga bao zuri sana Mwanza,”alisema Hamatre.
Mapema usiku wa kuamkia leo, Kocha Mkuu wa Simba SC, Milovan
Cirkovick aliwasili kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa mapumziko, tayari kwa
maandalizi rasmi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Simba, mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame, 1975, 1991,
1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara ya mechi mbili za
kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa
mashabiki wao wa huko.
Katika ziara yao hiyo, Simba ilicheza mechi ya mwisho jana
Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na
kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba
mabao 2-0.
Katika mchezo wa jana, kiungo mpya wa Simba SC, Kiggi
Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu ajiunge nayo mwezi huu
kutoka kwa mahasimu, Yanga.
Hata hivyo, bao hilo la Kiggi lilidumu kwa dakika 20 tu,
kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai Wekundu na hadi kipyenga
cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi
29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu tatu, mbali na Simba watakuwepo
mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu,
Azam FC.
Kiggi Makassy baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege |
Salim Kinje |
Nahodha wa Simba Kanda ya Ziwa; Uhuru Suleiman akiwa na kijana wake Samir Nasiri aliyekuja na mama yake kumpokea |
Viongozi; kutoka kulia Ofisa Habari, Ezekiel Kamwaga, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Pamba, Ibrahim Maestro na Meneja Nico Nyagawa. Hawa wamevuna pointi nne Kanda ya Ziwa. |
0 comments:
Post a Comment