• HABARI MPYA

        Sunday, June 10, 2012

        NIYONZIMA HASTAHILI KUWANIA TUZO TANZANIA, MAFISANGO ANASTAHILI HATA KUSHINDA


        Na Mahmoud Zubeiry

        KAMATI ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania (TASWA) imemteua kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Fadhil Hakizimana Niyonzima wa Yanga, kuwania tuzo hizo katika kipengele cha mchezaji wa kigeni Tanzania.
        Kiungo huyo wa zamani wa APR na Rayon za Rwanda, atachuana na Kipre Tchetche wa Ivory Coast anayechezea Azam FC na Mganda Emmanuel Okwi wa Simba, kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa mwaka wa kigeni nchini ya TASWA.
        Hata hivyo, inashangaza katika orodha iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo, Masoud Saanan, hayumo kiungo aliyeng’ara zaidi msimu huu, kuliko mchezaji mwingine yeyote wa kigeni aliyecheza Tanzania, marehemu Patrick Muteesa Mafisango, aliyekuwa mwanasoka wa kimataifa wa Rwanda.
        Niyonzima 'aliyebebwa'
        Kwa upande wa wanasoka wazalendo, tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka inawaniwa na John Bocco, Aggrey Morris, wote wa Azam na Juma Kaseja wa Simba, wakati kwa wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje wanaoshindana ni Henry Joseph wa Kongsvinger ya Norway na Mbwana Samatta wa Tout Puissant Mazembe ya DRC.
        Kwa upande wa wanawake, Sophia Mwasikili anayecheza Uturuki, anashindana na Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omary wote wa Mburahati Queens, Fatuma Mustapha wa Sayari na Eto’o Mlenzi wa JKT.
        Unaweza kujiuliza kwa nini Mafisango hayumo naye ndiye mchezaji aliyeng’ara zaidi msimu uliopita, kuliko mchezaji mwingine yoyote wa kigeni na kubaki na labda tu.
        Labda kwa sababu amekwishafariki dunia. Labda Kamati ya Saanan, mwandishi mkongwe wa habari za michezo nchini ilipitiwa. Labda vyovyote utakavyofikiria.
        Mafisango anastahili zaidi kuingia kwenye kipengele cha tuzo hii kuliko Niyonzima, kwa sababu ambazo nitaziainisha.

        NANI ALIANZA KUCHEZA TANZANIA.
        Wakati Niyonzima anatua Yanga Julai mwaka jana akitokea APR, tayari marehemu Mafisango alikuwa mzoefu wa mitaa ya jiji la Dar es Salaam akiwa amechezea Azam FC kwa msimu mzima.
        Hadi kufikia Mei mwaka jana, Ligi Kuu inafikia tamati Mafisango alikuwa anakamilisha msimu mzima wa kucheza Tanzania.
        Wakati Niyonzima anachezea APR katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka jana kituo cha Morogoro, Mafisango alikuwa anaichezea Simba katika michuano hiyo hiyo kituo cha Dar es Salaam na kuifikisha fainali ya michuano hiyo walikofungwa na Yanga 1-0.
        Mafisango aling’ara kwenye michuano hiyo akiwa anachezea timu ya Tanzania, wakati Niyonzima licha ya kwanza hakuwa anachezea timu ya Tanzania, pia hakung’ara na timu yake haikufika popote.
        Kajula wa NMB akimkabidhi tuzo Mafisango (RIP) 
        Kwa mara ya kwanza Niyonzima alicheza Tanzania, Agosti mwaka kwenye Ngao ya Jamii, Simba na Yanga zilipokutana.
        Simba ilishinda 2-0 na Mafisango mwisho wa mchezo alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi na donge nono la Sh. 500,000 kutoka kwa benki wa NMB. Nakumbuka Imani Kajula wa NMB alimkabidhi mfano wa hundi uwanjani Mafisango, ishara kwamba siku hiyo alimfunika Haruna.

        NANI ANASTAHILI KWA MAFANIKIO:
        Kwa mwaka jana, Mafisango alibeba Ngao ya Jamii na tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi hiyo sambamba na Medali ya Fedha ya Kombe la Kagame, wakati Niyonzima aliambulia patupu.
        Mafisango akiwa amembeba Kaseja
        wakishangilia mafanikio ya mwaka jana
        Kuelekea kumalizia msimu, Niyonzima alimaliza kinyonge mno, timu yake ikikosa hata nafasi ya pili Ligi Kuu, ikifungwa 5-0 na watani wao Simba na kutolewa mapema kwenye michuano ya Afrika.
        Lakini Mafisango aliiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, yeye peke yake akifunga mabao 10 na aliifikisha hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika, bila kusahau aling’ara kwenye mechi ambayo Yanga walikula 5-0 Taifa.

        KIGEZO CHA NIDHAMU UWANJANI:    
        Mafisango alimaliza msimu bila kupewa kadi nyekundu zaidi tu ya kuwahi kushutumiwa na uongozi wa klabu yake kwa kuchelewa kambini, kiasi cha kufikia kutaka kuachwa safari ya Algeria kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho, lakini akasamehewa na kuendelea na kazi.
        Lakini Niyonzima alipewa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Alipewa kadi nyekundu na hilo lipo kwenye rekodi- haijalishi refa alimuonea au vipi.
        Unaweza kuona hapa- hata kwa kigezo cha nidhamu ya uwanjani, bado Mafisango anastahili kuwania tuzo hii.
        Labda Kamati ya Saananm ituambie kwa utaratibu wake, kwao mtu aliyefariki dunia hastahili tuzo.

        YAW BERKO ALIKUWA CHAGUO SAHIHI:

        Kuna masuala mawili- kuingia kwenye kuwania tuzo na kushinda tuzo- ukirejea mwaka jana ulikuwaje katika soka ya Tanzania na wachezaji wa kigeni walifanya nini, unapata jibu Yaw Berko alistahili kuingia tena kutetea tuzo yake. Kwa nini?
        Aprili mwaka jana aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara na Julai mwaka jana akaiwezesha Yanga kutwaa taji la Kagame, baada ya miaka 11 yaani tangu klabu hiyo ilipotwaa taji kwa mara ya mwisho mwaka 1999 mjini Kampala, Uganda marehemu Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ akiwa anacheza katika beki ya kati na ‘Meja’ Ally Mayay Tembele.
        Kumbuka mechi ya Ngao, ambayo Yanga ilifungwa 2-0, Berko alikuwa majeruhi na langoni alisimama Shaaban Hassan Kado. Alidaka vizuri mwaka jana- rejea mechi ngumu za Kagame dhidi ya Merreikh na St George pamoja na ya Simba, hadi watu wakawa wanasema, Yanga wamshukuru kipa wao.
        Sasa jiulize kwa nini asiingie huyu kuchuana na Okwi na Mafisango, kuliko Niyonzima?
        Nawasilisha.
        • Blogger Comments
        • Facebook Comments

        0 comments:

        Item Reviewed: NIYONZIMA HASTAHILI KUWANIA TUZO TANZANIA, MAFISANGO ANASTAHILI HATA KUSHINDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry