23 Juni, 2012 - Saa 15:06 GMT
KOCHA wa zamani wa timu ya soka ya Ireland ya Kaskazini, Alan McDonald, amefariki ghafula akiwa na umri wa miaka 48.
McDonald, ambaye alikuwa ni meneja wa timu ya Glentoran wakati ilipochukua ubingwa wa ligi ya Ireland mwaka 2009, alizimia alipokuwa akicheza golf Jumamosi asubuhi.
McDonald, aliyekuwa mchezaji wa kati katika soka, alizaliwa mjini Belfast, na alikuwemo katika timu ya Ireland ya Kaskazini ambayo ilitoka 0-0 dhidi ya England katika mechi ya mwaka 1985, na kuiwezesha nchi yake kufuzu kwa michuano ya Kombe la Dunia.
Aliichezea timu ya Ireland ya Kaskazini mechi 52.
Alifanikiwa kuifungia timu bao moja, wakati walipocheza dhidi ya Denmark mwaka 1986.
Habari za kifo chake ni pigo kubwa kwa wapenda soka katika Ireland ya Kaskazini.
Alikuwa na biashara ya kuuza tuzo mbalimbali za michezo mjini Bangor, biashara ambayo awali ilikuwa ikiendeshwa na mchezaji mwenzake katika timu ya taifa, Billy Hamilton.
McDonald alicheza zaidi ya mechi 400 katika timu ya mjini London ya QPR, na ni kati ya wachezaji waliokuwa katika timu iliyofika fainali ya Kombe la Ligi mwaka 1986, waliposhindwa na Oxford United magoli 3-0.
Kisha baadaye aliichezea Charlton kwa mkopo, na vilevile Swindon Town.
Baada ya kustaafu alikuwa msaidizi wa kocha wa timu ya Ireland ya Kaskazini ya vijana chini ya umri wa miaka 21.
Wakati Ireland ya Kaskazini ilipofuzu kuingia michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1986, alipata nafasi ya kucheza dhidi ya Algeria, Uhispania na Brazil.
0 comments:
Post a Comment