Milovan Cirkovick |
Na Princess Asia
WAKATI Kocha Mkuu wa Simba SC, Milovan Cirkovick amewasili
alfajiri ya leo kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa mapumziko, kikosi cha mabingwa
hao wa Ligi Kuu kinapanda ndege ya ATC saa1:00 usiku wa leo mjini Mwanza,
kurejea Dar es Salaam kuungana na mwalimu hiyo kwa maandalizi ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’
ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi hii
kwa simu kutoka Mwanza kwamba timu ikifika itaendelea na mzoezi Uwanja wa TCC, Chang’ombe, Dar es
Salaam chini ya Profesa Milovan, aliyetua kwa ndege ya shirika la ndege la
Uturuki saa 8:45 usiku wa jana.
Simba, mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame, 1975, 1991,
1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara ya mechi mbili za
kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa
mashabiki wao wa huko.
Katika ziara yao hiyo, Simba ilicheza mechi ya mwisho jana
Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na
kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba
mabao 2-0.
Katika mchezo wa jana, kiungo mpya wa Simba SC, Kiggi
Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu ajiunge nayo mwezi huu
kutoka kwa mahasimu, Yanga.
Hata hivyo, bao hilo la Kiggi lilidumu kwa dakika 20 tu,
kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai Wekundu na hadi kipyenga
cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi
29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu tatu, mbali na Simba watakuwepo
mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu,
Azam FC.
0 comments:
Post a Comment