Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga kushoto akizungumza na Waandishi wa Habari asubuhi ya leo TFF, kulia ni Katibu wake, Nicholaus Musonye |
KUTOKANA na kukosekana kwa mdhamini wa mashindano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame- klabu zitakazoshiriki michuano hiyo iliyopangwa
kuanza Julai 14 hadi 29, mwaka huu zimetakiwa kujigharamia nauli za kuja Dar es
salaam na kurudi nchini mwao.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Michezo Afrika Mashariki
na Kati (CECAFA), Leodegar Chillah Tenga amesema leo katika Mkutano na
Waandishi wa Habari, Ofisi za Shirikisho Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam kwamba
wamechelewa kutangaza mashindano hayo yataanza lini, kutokana na pilika za
kutafuta wadhamini.
Tenga amesema hadi sasa hawajapata na kwa sababu hiyo
wameamua kufanya mashindano hayo bila udhamini. Tenga amesema wamekubaliana
Wajumbe wa CECAFA kwa kuwa mashindano hayo hayana udhamini, basi timu zote zijigharamie
usafiri wa kuja na kuondoka Dar es Salaam.
Tenga amesema CECAFA itagharamia malazi na usafiri wa ndani
kwa timu zote, wakati marefa watagharamiwa kila kitu kuanzia usafiri wa kuja
kutoka nchini mwao na wa ndani pia.
Tenga amesema kwamba anafurahi Tanzania kuwa mwenyeji wa
michuano hii kwa mara nyingine, kwani pamoja na kupata fursa ya kuuhamasisha
mchezo wa soka, lakini pia inatoa fursa kwa timu nyingi za Tanzania kushiriki.
Alisema kwamba wanafanya mazungumzo na Televisheni ya
kulipia ya Super Sport na nyingine za nyumbani, ziweze kurusha mashindano hayo
moja kwa moja. Lakini Tenga amesema mazungumzo yanaendelea na baadhi ya wadhamini,
waweze kuchangia japo kidogo gharama za maandalizi.
Katika michuano ya mwaka huu, Tanzania itawakilishwa na timu
tatu, mabingwa watetezi, Yanga, na wawakilishi Simba SC, mabingwa wa Tanzania
na Azam FC ambao ni washindi wa pili.
Kwa upande wake, Katibu wa CECAFA, Nichalaus Musonye amesema
wamepata maombi ya klabu kutoka nje ya ukanda huu, Vita Club ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Dymanos ya Zimbabwe na Blomomfontein na Platinum
za Afrika Kusini kuomba kushiriki michuano hiyo, hata hivyo kukubaliwa
itategemea na idadi ya timu za ukanda huu zitakazothibitisha ushiriki wake.
0 comments:
Post a Comment