Willy akiwa Rais Jakaya Kikwete enzi za uhai wake |
MHARIRI wa Jamboleo, Willy Edward Ogunde amefariki dunia mjini Morogoro usiku wa kuamkia leo (saa 6.30) usiku.
Taarifa ya Neville Meena, Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, imesema kwamba Willy aliyewahi kuwa Mhariri wa gazeti la BINGWA, pamoja na wahariri wengine walikuwa mjini Morogoro ambako walikwenda kuhudhuria mkutano wa masuala ya sensa iliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Mara baada ya semina hiyo alikwenda kuwaona watoto wake na alikuwa huko hadi saa sita usiku alipomwita dereva wa pikipiki afike kumchukua kwa lengo la kurejea katika hoteli alikokuwa amefikia. Baada ya kutoka nje, na hatua sita hivi kabla ya kufika pikipiki ilipokuwa, alianguka.
Ndugu zake walimkimbiza hosipitali lakini walipofika na daktari kumpima, tayari alikuwa “amenyamaza” yaani amefariki dunia. Taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Dar es Salaam zinafanywa.
Tutamkumbuka daima kwa upole na unyeyekevu wake. Kweli Willy ametuacha, ni pigo kwa taaluma yetu, ni pogo katika Jukwaa la Wahariri. Poleni kwa familia ya Willy Edward Ogunde, pole kwa wahariri wote na pole kwa tasnia nzima ya habari. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
0 comments:
Post a Comment