Washiriki |
Na Princess Asia
MCHEZA sinema maarufu kutoka Marekani Deidre Lorenz leo amezipamba mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon zilizotimua vumbi kuanzia saa mbili za asubuhi kutoka klabu maarufu ya Moshi hadi Rau madukani. Lorenz alikuwa mmoja wa wakimbiaji zaidi ya 200 kutoka katika nchi za Marekani, Canada, Uingereza, India, Australia, Brazil na Tanzania.
Kushiriki kwa mcheza sinema huyo maarufu wa sinema za Santorini Blue (ambayo ilitegenezwa kwenye fukwe za mahaba za kisiwa cha Santorini nchini Ugiriki), Perfect Strangers, The Big Fight na nyingije nyingi imezifanya mbio za Mt. Kilimanjaro Marathon kuwa na hadhi ya kipekee katika mbio za marathon hapa Afrika.
Mbio hizi zilizoanzishwa na Marie Frances kutoka katika jiji la matajiri la Bethesda nje kidogo ya jiji la Maryland kule Marekani zimetimiza miaka 22 toka zianzishwe mwaka 1991. Mt. Kilimanjaro Marathon zilizishwa baada ya balozi wa zamani wa Tanzania nchini Misri kumwomba Marie Frances kuja Tanzania na kuanzisha mbio zenye hadhi ya kimataifa. Mt. Kilimanjaro Marahon zimeshawahi kushinda tuzo mbalimbaliza kimataifa zilizotolewa na Wonders of the World Magazine ambalo lina wasomaji zaidi ya miloioni 5 na kuzipa nafasi ya pili na wakati gazeti maarufu duniani la Forbes lilizipa nafasi ya kwanza kati ya mbio zinazojulikana kama Seven Continental Races.
Kutokana na kuutangaza mji wa Moshi kwa kiwango kikubwa kimataifa Manispaa ya Moshi ilimpa barabara inayojulikana kama Marie Frances Boulevard pamoja na funguo za Manispaa ya Moshi na Cheti ya ukazi wa kudumu.
Mkimbiaji kutoka jiji la Arusha Getuni Tsekewey aliibuka kidedea wa mbio za kilometa 42 kwa kukimbia kwa saa 2 na dakika 26 nukta 30 wakati Nicodemus Hiiti kutoka Kilimanjaro alikuwa wa 2 kwa kukimbia saa 2 na dakika 38 nukta 20 naye Shauri Habiye kutoka Arusha alikuwa wa tatu kwa kukimbia saa 2 na dakika 38 nukta 24.
Wengine ni Samwel Lucian kutoka Kilimanjaro aliyenyakua nafasi ya 4 kwa kukimbia kwa saa 2 dakika 38 nukta 47 wakati Petro Gimanya wa Kilimanjaro alitimka kwa saa 2 dakika 57 nukta 18 na kushika nafasi ya 5.
Katika mbio za Marathon upande wa wanawake Banuelia Brighton alitimua vumbi na kushika nafasi ya kwanza kwa saa 3 dakika 06 nukta 01 wakati Flora Yada alimfuatia kwa mbali kwa kukimbia kwa saa 3 dakika 38 nukta 08.
Kwa upande wa mbio za nusu marathon wanariadha kutoka Arusha walinyakua nafasi zote. Peter Sule alikimbia kwa saa 1 dakika 07 nukta 42 na kuwa wa kwanza, Mohamed Duley alishika namba mbili kwa kikimbia kwa saa 1 dakika 07 sekunde 98 wakati Said Hassan alitimka kwa saa 1 dakika 10 sekunde 25 na kuwa wa tatu.
Nusu marathon kwa wanawake kulikuwa na mkimbiaji mmoja tu ambapo Farida Guse wa Arusha alikimbia kwa saa 3 dakika 22 sekunde 22.
Mbio za kilometa 10 (10K) ziliwashirikisha wageni tu ambapo kwa upande wa wanaume Sander Markos kutoka Marekani alishika nafasi ya kwanza kwa kukimbia kwa saa 1 dakika 01 sekunde 20 na Malcom Frazer pia kutoka Marekani alikimbia kwa saa 1 dakika 20 sekunde 22 na kuwa wa pili.
Kwa upande wa wanawake mbio za kilometa 10 (10K) kwa wageni Cindy Johanson kutoka Kanada alikuwa wa kwanza kwa kukimbia kwa saa 1 dakika 12 sekunde 22, Marika Johson alishika nafasi ya pili kwa kukimbia kwa saa 1 dakika 20 sekunde 48, Talia Peter kutoka Marekani alikuwa wa tatu kwa kukimbia kwa saa 1 dakika 26 sekunde 04.
Naye mcheza sinema maarufu kutoka Marekani Deidre Lorenz alimaliza mbio za kilomita 42 na kufanya kuwa mbio za tatu za marathon alizowahi kukimbia baada ya zile za New York Marathon mwaka 2010 na 2011.
Lorenz aliondoka na ndege ya shirika la Ethiopia Airlines kurudi kwake "The Big Apple" kama linavyojulikana jiji la New York la Marekani ambapo hufanya shughuli zake za kucheza sinema.
0 comments:
Post a Comment