Na Mahmoud Zubrity |
HADI
kufika mwaka 1975, klabu za Simba na Yanga zilikuwa tayari zina majengo mazuri,
magari na hadhi kubwa- na wakati huo waliokuwapo waliotabiri miaka 20 baadaye
klabu hizo zitakuwa mbali zaidi kimafanikio.
Hayakuwa
mafanikio ya kiuchumi tu, bali hata soka- hicho ndio kipindi ambacho Simba na
Yanga zilikuwa moto wa kuotea mbali katika michuano ya Afrika.
Yanga
ilicheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 1969 na
1970, mara zote ikitolewa kwa mbinde na Asante Kotoko ya Ghana, wakati Simba
ilifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika na kutolewa na Mehallal El Kubra ya
Misri mwaka 1974.
Simba
na Yanga ziliendelea kuwa tishio kisoka na kipindi hicho ilishuhudiwa zikifanya
ziara za mafunzo Ulaya na Amerika.
Ilitabiriwa
miaka 20 baadaye, mambo yatakuwa mazuri zaidi kwenye klabu hizo, lakini kutoka
mwaka 1975 hadi leo sasa ni miaka 35 imepita, hali ikoje Simba na Yanga?
Ni
mbaya, mbaya kabisa, majengo yamechakaa, magari hakuna tena zaidi ya yale ya
msaada kutoka TBL, yanayotokana na mkataba wao wa udhamini. Yanga ambayo
ilikuwa juu zaidi kwa kuwa na mabasi, majengo zaidi ya matatu, Uwanja wa
Kaunda, sasa imebaki na jengo moja ambalo lilifanyiwa ukarabati hivi karibuni
na Yussuf Manji, pale Jangwani, japokuwa tayari limeanza kuharibika.
Uwanja
wa Kaunda umechoka, umechakaa kwa sababu hauna matunzo na haufai kwa matumizi,
zaidi Yanga wanautumia kwa mazoezi ya kuwachangamsha tu wachezaji kama kipindi
hiki wanaanza kukusanyika, lakini siku mbili zijazo utasikia wako Loyola.
Hakuna
taarifa za uhakika kuhusu majengo mengine ya klabu kama lile la Mtaa wa Mafia,
lile la Tandale na ile nyumba ya NHC ambayo awali aliishi Profesa Victor
Stanslescu, baadaye Tambwe Leya, kabla ya Charles Boniface Mkwasa. Leo Yanga
inaingia gharama kuwapangia nyumba makocha wake, wakati wana nyumba yao
waliyopangishiwa na NHC pale Fire, wamepokonywa?
Najaribu
kutafakari hali ndani ya Yanga ingekuwaje kama asingejitokeza Manji mwaka 2006
na kujitolea kwa hali na mali kuisaidia klabu hiyo, kwa kweli sipati jibu mambo
yangekuwaje.
Aliingia
baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist
Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na
baadhi ya waandishi wa habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha
harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya
klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
Katika
kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji
naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo,
amekuwa akiilea Yanga na sasa ameamua kabisa kuwa Mwenyekiti.
Wafadhili
wamekuwa wakiingia na kutoka kwenye klabu hizi tangu miaka ya 1990 na wamekuwa
wakisaidia mno, angalau Simba wamekuwa wakitumia vizuri fursa ya ufadhili,
lakini kwa Yanga zaidi wamekuwa wakiwageuza ‘mabuzi’ tu wafadhili wao.
Zama
za ufadhili wa Azim Dewji, Simba ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993,
zama za ufadhili wa Mohamed Dewji, Simba ilicheza hatua ya makundi ya Ligi ya
Mabingwa Afrika mwaka 2003, ikiitoa Zamalek iliyokuwa inashikilia taji. Haya
sasa, Yanga watuambie walifanya nini wakati wanafadhiliwa na Abbas Gulamali kwa
pamoja na Murtaza Dewji au wakati huu wanaogelea kwenye bwawa la fedha za
Manji, wanafanya nini?
Narejea
nyuma miaka ile Yanga iko chini ya Mwenyekiti Mangara Tarbu namna ilivyopata
mafanikio ya haraka ya uwanjani na kiuchumi kama Simba ilipokuwa chini ya akina
Mwenyekiti Dumelezi na Katibu Mkuu Said Mpolaki, naona kabisa kizazi kipya kimeshindwa
kuzivusha katika hatua nyingine klabu hizi.
Binafsi
sijali kujiongezea watu wa kunichukia kwa kuandika ukweli juu ya soka ya nchi
hii na sitarudi nyuma; wamepita watu wengi ndani ya miongo hii miwili, lakini
hakuna chochote kilichofanyika na kila siku kinachojitokeza ni afadhali ya
waliokuwapo.
Umefika
wakati serikali iingilie kati kuziokoa hizi klabu, kwani ni rasilimali za taifa
hizi iwapo zitatumika vizuri. Zitatoa ajira kwa vijana, zitachangia pato la
taifa kwa kodi, ikiwa tu zitakuwa chini ya usimamizi imara wenye tija.
Leo
Waingereza wamekubali timu zao zimilikiwe na wageni na sasa timu zote kubwa
zinamilikiwa na wageni, lakini kwa sababu wenyewe haswa wenye timu wanachotaka
ni furaha, wanaangalia mambo ya msingi mawili; klabu inanufaika kiuchumi,
inapata mafanikio uwanjani? Inatosha.
Manchester
United, ama Chelsea FC, au Arsenal hata Liverpool, hazina makomandoo. Hazina
ombaomba wa kuomba fedha viongozi. Hazina watu wanaolilia wapewe nafasi ya
kuuza tiketi wala kusimama milangoni. Zina watu ambao wanataka ushindi na
kusikia klabu inaigiza fedha.
Hata
kwetu Tanzania, mashabiki wa kweli wa timu hizi ni wale wanaonunua tiketi
kwenda uwanjani kushangilia timu zao. Wanachotaka ni ushindi na kusikia klabu
zao zinapata mafanikio na kuwa sawa na klabu nyingine zilizopiga hatua kubwa
kiuchumi na kisoka Afrika.
Lakini
inasikitisha kuona miongo miwili imekatika Simba na Yanga zinazidi kutumbukia
kwenye dimbwi la umasikini wa soka na uchumi, kwa sababu gani tusiwakumbuke
akina Mangara na Dumelezi, waliozijengea klabu hizi misingi imara ya kisoka na
uchumi? Wakubwa wa leo wanabadilisha suti na magari ya Kijapani, lakini klabu
zinanuka uvundo, zinatia kichefuchefu. Wapo kwa ajili ya kusaka umaarufu tu,
hawana cha maana wanachofanya.
Angalau
sasa Manji anaingia pale Yanga, naamini atasababisha mabadiliko makubwa na nitafurahi
Mohamed Dewji naye akigombea Uenyekiti Simba katika uchaguzi ujao, kwa sababu
atasaidia mno kuimarisha klabu hiyo na upinzani wa jadi wa klabu hizo, ambao ni
chachu ya msisimko wa soka yetu. Alamsiki!
0 comments:
Post a Comment