Thomas Ulimwengu, mshambuliaji wa Ngorongro |
CHAMA cha Soka Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki
kwa timu yao ya vijana na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya
Tanzania (Ngorongoro Heroes).
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, EFA
imeomba mechi hizo zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu kwa masharti maalumu.
Ikiwa zitachezwa Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia Ngorongoro Heroes kwa
malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya kufanyia mazoezi.
Amesema ikiwa mechi hizo zitachezwa Dar es Salaam,
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaigharamia timu ya Misri kwa
malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya mazoezi. Hivyo, amesema kila
timu itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho kwa timu yake.
“Sekretarieti ya TFF inafanya uchambuzi wa gharama ili kujua
ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi mechi hizo zichezwe”amesema.
Ngorongoro Heroes imeingia raundi ya pili ya michuano ya
Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria baada ya kuitoa
Sudan katika raundi ya kwanza.
Itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili Julai 28 mwaka
huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini
Nigeria.
0 comments:
Post a Comment