Na Mahmoud Zubeiry |
JANA Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki
na Kati (CECAFA), Leodegar Chillah Tenga alitangaza rasmi kwamba michuano ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame itafanyika kuanzia Julai
14 hadi 29, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Beki huyo wa zamani wa kati wa kimataifa wa Tanzania,
alisema hayo katika Mkutano na Waandishi wa Habari, Ofisi za Shirikisho
Tanzania (TFF) na kutoa sababu ya kuchelewa kutangaza mashindano hayo yataanza
lini, kwamba ni pilika za kutafuta wadhamini.
Tenga aliyewika Yanga na Pan African enzi zake, alisema hadi
jana walikuwa hawajapata wadhamini na kwa sababu hiyo wameamua kufanya
mashindano hayo bila udhamini. Tenga aliyekuwamo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980, amesema wamekubaliana Wajumbe
wa CECAFA kwa kuwa mashindano hayo hayana udhamini, basi timu zote zijigharamie
usafiri wa kuja na kuondoka Dar es Salaam.
Tenga amesema CECAFA itagharamia malazi na usafiri wa ndani
kwa timu zote, wakati marefa watagharamiwa kila kitu kuanzia usafiri wa kuja
kutoka nchini mwao na wa ndani pia.
Tenga amesema kwamba anafurahi Tanzania kuwa mwenyeji wa
michuano hii kwa mara nyingine, kwani pamoja na kupata fursa ya kuuhamasisha
mchezo wa soka nchini, lakini pia inatoa fursa ya kwa timu nyingi za Tanzania
kushiriki.
Wakati mchakato wa michuano hiyo, ukiwa umefikia katika
hatua hii, inasikitisha kwamba mabingwa watetezi, Yanga hadi leo hawajaanza
maandalizi yoyote.
Frank Damayo, mmoja wa waliosajiliwa Yanga |
Tayari Simba na Azam zimeanza kujifua, japokuwa wachezaji
wake wengi wapo timu ya taifa, Taifa Stars- ingawa hiyo ni faida pia kwao.
Nawashangaa Yanga; nasema hivyo bila kusita, kwa sababu
pamoja na kumaliza msimu vibaya, waliingia kwenye mgogoro ambao mwisho wa siku
ulisababisha Mwenyekiti wa klabu hiyo, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga akajiuzulu
sambamba na wajumbe kadhaa.
Baada ya hapo, TFF kwa kuona safu ya uongozi haitimii,
ikaamuru wafanye uchaguzi wa kuziba mapengo Julai 15, mwaka huu.
Wakati Nchunga anaachia ngazi, alisema timu itakuwa chini ya
Baraza la Wadhamini kwa mujibu wa Katiba, ambalo lingefanya kazi kwa
kushirikiana na sekretarieti. Ajabu, hadi leo Baraza ka Wadhamini halijajitokeaa
kusema limepokea au kutopokea majukumu hayo.
Zaidi ya hapo, tunasikia zoezi la usajili Yanga linaendelea
japokuwa timu haina kocha, kwa sababu Freddy Felix Minzito alikwishatangaza
kugoma kufanya kazi hadi alipwe malimbikizo ya mishahara na posho zake za msimu
uliopita.
Mapema tu, kabla ya mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu,
aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Bozidar Papic ‘alifukuzwa
kiaina’, yaani baada ya kumaliza mkataba wake hakuongezewa na hakupewa fursa ya
kuendelea kuwa kambini na timu.
Kwa sasa Yanga wapo kwenye mchakato wa usajili pamoja na
kuajiri kocha, huku vyanzo vikisema wagombea uongozi wenye machungu zaidi na
klabu hiyo ndio wanaendesha mchakato wa kusaka kocha na wachezaji wapya wa
kuimarisha kikosi kipya na Marcio Maximo, Mbrazil aliyewahi kuinoa Taifa Stars
anatajwa kupewa nafasi kubwa ya kuajiriwa Jangwani.
Kwa mazingira ambayo yanaikabili Yanga kwa sasa huwezi
kustaajabishwa na hali hii, lakini jambo la kushangaza tu ni kwamba, ni kwa
nini hadi leo Yanga hawajaanza kujifua kama wenzao Simba SC na Azam?
Kelvin Yondan, amesajiliwa Yanga |
Nchunga alisema timu anaikabidhi Baraza la Wadhamini, je kwa
nini hadi leo Baraza hilo limekuwa kimya?
Sawa, lakini kama wagombea uongozi Yanga katika uchaguzi wa
Julai 15 wanasajili wachezaji, kwa nini hawafikirii kuhusu maandalizi?
Kuwa na wachezaji bora pekee bila ya kuwaandaa vizuri kwa
mashindano haitoshi kukufanya uwe na timu bora ya kukuletea mataji. Je, Yanga
hawajui hilo? Tatizo moja tu, Yanga karibu wote wamejiwekea utamaduni wa
kutokubali ukweli,
Ukiwaambia ukweli wanakuchukia, bila kufanya tathmini juu ya
nini kipo mbele yao. Leo Simba na Azam wanajifua, Yanga bado wamelala, hivi
kweli wana Yanga watarajie furaha au majonzi katika Kagame? Nawasilisha!
0 comments:
Post a Comment