KIUNGO chipukizi wa Simba SC, Shomary Kapombe amesema kwamba
mafanikio anayoyapata hivi sasa ni changamoto nzuri kwake na hatalewa sifa,
badala yake ataongeza juhudi ili afike mbali kisoka.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY usiku wa jana katika
ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Kapombe alisema kwamba amefurahi mno kutwaa
tuzo mbili, Mwanamichezo Bora Anayechipukia na Mwanamichezo Bora wa Jumla wa
mwaka Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), lakini
hatalewa sifa.
“Nimefurahi kwa kweli, ila kwangu hii ni kama changamoto na
ninawaahidi Watanzania kwamba sitalewa sifa na nitajitahidi nifike mbali,”alisema
Kapombe.
Kiungo huyo anayeweza kucheza kama beki wa kati na kulia pia,
alisema kwamba ndoto zake kwa sasa ni akitoka Simba akacheze Ulaya na kulingana
na mafanikio yake ya sasa akiwa bado mdogo Kapombe alisema anaamini atatimiza
ndoto zake.
“Naamini nitafika mbali, kwa sababu siri ya mafanikio ya
mchezaji ni bidii ya mazoezi na kusikiliza mafundisho ya walimu wake, nami nitazingatia
hilo,”alisema mfungaji huyo wa bao la kusawazisha katika ushindi wa 2-1 wa
Tanzania dhidi ya Gambia Jumapili, ikitoka nyuma kwa 1-0 katika mechi ya
kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia 2014.
Kapombe amemaliza
msimu mmoja tu Simba SC tangu asajiliwe kutoka Polisi ya Morogoro,
lakini kwa sasa tayari ni tegemeo la klabu yake na timu ya taifa. Kijana anacheza
kwa bidii na ana kipaji, kiasi kwamba hata kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars,
Kim Poulsen anamtabiria kufika mbali.
“Kapombe ni kati ya wachezaji wangu ambao nina matumaini
watafika mbali, namtakia kila heri na nampongeza kwa mafanikio yake,”alisema
Poulsen alipozungumza na BIN ZUBEIRY usiku wa jana.
Pamoja na kukesha Diamond Jubilee usiku wa jana, lakini Kapombe
ameondoka na kikosi cha Taifa Stars alfajiri ya leo kwenda Msumbiji kwa ajili
ya mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya
Afrika mwakani Afrika Kusini dhidi ya wenyeji Jumapili, Tanzania ikitakiwa
kushinda au sare ya mabao yasiyopungua 2-2 ili isonge mbele, kufuatia awali
kulazimishwa sare ya 1-1.
0 comments:
Post a Comment