Mussa Mudde anatua Msimbazi leo |
Na Prince Akbar
KIUNGO wa kimataifa wa Uganda, Mussa Mudde aliyesajiliwa na
mabingwa wa soka Tanzania, Simba SC kutoka Sofapaka ya Kenya, anatarajiwa
kuwasili leo kujiunga na wenzake kuendelea na maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, imeelezwa.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ‘Mr Liverpool’,
ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, mbali na Mudde kutarajiwa kutua leo, pia
mshambuliaji wao waliyemsajili kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny
Mrwanda ataanza mazoezi rasmi leo.
“Mazoezi yataendelea Sigara (TCC Chang’ombe) na pamoja na
kumtarajia Mudde, lakini pia mshambuliaji wetu wa zamani, Danny Mrwanda
aliyerejea kikosini, ataanza mazoezi kesho,”alisema jana usiku Kamwaga.
Katika mazoezi ya Simba SC juzi na jana uwanja wa TCC, beki
mpya wa klabu hiyo Masombo Lino, kutoka Daring Club Motema Pembe kutoka ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amekuwa kivutio kutokana na soka yake
baab kubwa.
Katika mazoezi yanayoendelea chini ya Kocha Mkuu wa klabu
hiyo, Mserbia Milovan Cirkovick, Masombo amekuwa akionyesha ni mzuri kwenye
kuzuia na kusaidia mashambulizi pia.
Mazoezi ya Simba yanaendelea leo kwenye Uwanja huo,
kujiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano
iliyopangwa kuanza Julai 14 hadi 29, mwakani.
Beki hilo la kati ambalo lilipiga soka ya uhakika mwaka jana
wakati Simba ilipokutana na DC Motema Pembe katika mechi ya mchujo kuwania
kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika lilitua jana Dar es
Salaam na leo imeelezwa limesaini mkataba.
Simba, mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara, wamemsajili beki huyo
kuziba pengo la beki wao hodari, Kelvin Patrick Yondan ambaye amehamia kwa
wapinzani, Yanga.
Wakati huo huo: Kamwaga amesema kuhusu kushiriki kwao au kutoshiriki
michuano ya Kombe la Ujirani Mwema, inayoandaliwa na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA)
wataamua leo.
“Tutakuwa na kikao kesho, lazima tupitie ratiba ya
mashindano hayo na tuangalie je haitatuathiri kwa ushiriki wetu kwenye Kombe la
Kagame, maana Kagame nayo inafanyika mwezi huu pia,”alisema Kamwaga.
0 comments:
Post a Comment