Jaji Mkwawa akiwanoyesha Waandishi wa Habari Katiba mbili tofauti za Yanga. ya 2011 kulia na 2010 kushoto leo makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam. |
Na Prince Akbar
MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu ya Yanga ya Dar es
Salaam, Jaji John Mkwawa amemtaka Mgombea Uenyekiti wa klabu hiyo katika uchaguzi
utakaofanyika Julai 15, mwaka huu, Yussuf Mehboob Manji kufika kesho saa 4:00
asubuhi makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar
es Salaam kusikiliza pingamizi lake.
Jaji Mkwawa amesema hayo mchana huu katika Mkutano na
Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa
Habari kuhusu masuala mbalimbali kuelekea uchaguzi huo, zaidi pingamizi dhidi ya
wagombea na ufafanuzi wa Katiba itakayotumika.
Jaji Mkwawa alisema kwamba, baada ya kupokea pingamizi dhidi
ya wagombea Uenyekiti, Manji na Sarah Ramadhani, Makamu Mwenyekiti, Yono
Kevella, Clement Sanga na Ally Mayay amewataka wagombea hao na watu
waliowawekea pingamizi kujitokeza katika usikilizwaji wake kesho.
Lakini Jaji Mkwawa amesema Kamati yake inaweza kusikiliza na
kuamua kuhusu mapingamizi hayo bila ya kuwepo waliowekewa au walioweka, ila tu
amesistiza ni vema wakawepo ili watetee hoja zao.
Aidha, kuhusu tamko la mwanachama Abeid Abeid ‘Falcon’
kutaka ufafanuzi wa Katiba ipi itatumika katika uchaguzi huo, Jaji Mkwawa
alisema itatumika Katiba ya mwaka 2010 iliyowasilishwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) Juni 17, mwaka huo.
Amemtoa wasiwasi Abeid kwamba katiba ya 2011 iliyokuwa na
matatizo kiasi cha kupingwa mahakamani na wanachama wa klabu hiyo haitatumika.
Lakini pia, Mkwawa amesema pamoja na kwamba uchaguzi huu unakuja
baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji, wakiwemo Mwenyekiti na Makamu
wake kujiuzulu, Wajumbe waliojiuzulu kutoka kwenye uongozi huo wanaruhusiwa
kugombea.
Jaji Mkwawa akisoma pingamizi la Abeid Falcon |
Maana yake pingamizi dhidi ya Nahodha wa zamani wa Yanga,
Ally Mayay Tembele ‘Meja’ halina nguvu tena.
Aidha, kuhusu wagombea kusaidia klabu katika masuala
yanayohusu fedha katika kipindi hiki kigumu, Jaji Mkwawa amesema hayana matatizo
yakifanyika katika taratibu zinazoeleweka.
Baada ya kusikiliza pingamizi kesho, Jaji Mkwawa amesema usaili
utafanyika Juni 22 na Uchaguzi wa Yanga utafanyika Julai 15 kama ilivyopangwa,
siku moja baada ya kuanza kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la
Kagame, michuano ambayo, Yanga ni bingwa wake mtetezi.
0 comments:
Post a Comment