Na Princess Asia
ILALA imeendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya Copa
Coca-Cola baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuchapwa mabao 4-0 na
mabingwa watetezi Kigoma katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers
ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mabao yote katika mechi hiyo ya kundi A yalifungwa kipindi
cha kwanza huku Ramadhan Salum akipiga hat trick (mabao matatu). Alifunga mabao
hayo dakika ya 13, 43 na 45. Bao la pili kwa washindi lilifungwa dakika ya 19
na Athuman Rashid.
Wakati Kigoma imeshinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza
mpaka sasa katika kundi hilo, Ilala imepoteza mechi zote tatu ilizocheza. Ilala
imefungwa na Arusha, Kigoma na Lindi wakati mechi yake inayofuata itakuwa Juni
30 mwaka huu dhidi ya Kusini Pemba.
Nayo Kilimanjaro imeendelea kufanya vizuri katika kundi lake
la D baada ya leo asubuhi (Juni 28 mwaka huu) kuitandika Shinyanga mabao 3-0
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Mabao ya Kilimanjaro ambayo hadi sasa imeshinda mechi mbili na
kutoka sare moja yalifungwa na Adam Soba dakika ya 11 na 46 wakati la tatu
lilifungwa dakika ya 81 na James Henry.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi (Juni 28
mwaka huu), Temeke na Mtwara zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Tamco mkoani
Pwani. Ali Makalani alianza kuifungia Temeke na baadaye Adam swaleh
akaisawazishia Mtwara.
Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani ulishuhudia Morogoro na
Kaskazini Pemba zikitoka sare ya bao 1-0. Amin Kassim aliifungia Kaskazini
Pemba dakika ya 51, na Morogoro wakasawazisha dakika ya 75 kupitia kwa
Mutalemwa Katunzi katika mechi hiyo ya kundi B.
Mechi zitakazochezwa leo jioni (Juni 28 mwaka huu) ni Lindi
vs Arusha (Tanganyika Packers), Manyara vs Mjini Magharibi (Nyumbu), Kinondoni
vs Mbeya (Tamco) na Kusini Unguja vs Pwani (Karume).
Kesho (Juni 29 mwaka huu) ni mapumziko, na michuano hiyo
itaendelea tena Juni 30 mwaka huu kwenye viwanja vyote vinne
0 comments:
Post a Comment