![]() |
Wachezaji wa Azam |
BAADA ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja tangu kumalizika
kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wachezaji wa Azam FC
wameanza kuwasili mjini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame.
Meneja wa Azam FC, Patrick Kahemele ameiambia BIN
ZUBEIRY asubuhi hii kwamba,
kulingana na programu ya maandalizi, Azam FC wataanza
mazoezi Ijumaa wiki hii, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi maalum kwa mashindano
hayo yatakayofanyika mwezi ujao mjini Dar es Salaam.
Kahemele amesema wachezaji kutoka nje ya Tanzania watawasili
mapema wiki hii kwa maandalizi ya makazi kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo yatakayofanyika
kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi.
Alisema usajili kwa wachezaji ulikwishamalizika kabla ya
wachezaji kwenda likizo, hivyo wachezaji wote waliosajiliwa wataanza mazoezi isipokuwa
wale walioko kwenye timu zao za taifa, Tanzania, Uganda na Zanzibar, ambazo zipo
kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa wikiendi hii.
Alisema programu ya maandalizi ya Kombe la Kagame, itamalizika
siku moja kabla ya kuanza mashindano hayo na yatakapomalizika, wachezaji watapewa
mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi
Kuu.
Kahemele amesema maandalizi kwa ajili ya VPL yatahusisha pia
ziara ya nje ya nchi ya kujiandaa na msimu mpya, ingawa amesema nchi hiyo
itatajwa baadaye.
Kahemele alisema wachezaji wapya kiikosini Azam msimu huu ni
kiungo Mkenya George ‘Blackberry’ Odhiambo na kipa Deogratius Munishi kutoka
Mtibwa Sugar, wakati Aishi Salum, Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na
Joseph Kimwaga, wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili cha Azam FC kinaundwa; na makipa, Mwadini
Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi Salum na Jackson Wandwi, mabeki wa Ibrahim
Shikanda, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samir Haji Nuhu, Luckson Kakolaki, Said
Mourad, Joseph Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum
Abubakar, Abdi Kassim Sadalla, Ramadhani Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam,
Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima, Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche,
Mrisho Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati washambuliaji
ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco ‘Adebayor’.
Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada
ya kushika nafasi ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la Kagame
mwaka huu, wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa watetezi,
wakati Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.
Wakati huo huo: Kahemele amesema kwamba, Azam FC imepanga
kuifikisha klabu ya Simba kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), iliyo chini ya Mwenyekiti, Kamanda Mstaafu wa Polisi, kanda
maalum Dar es Salaam, Alfred Tibaigana iwapo itaendelea na mpango wa kumuiba
mchezaji wao, Jeba.
Simba na Azam zinamgombea mchezaji huyo chipukizi, ambaye
msimu uliopita alichezea Villa Squad Ligi Kuu kwa mkopo akitokea kwa wana Lamba
Lamba, lakini Wekundu wa msimbazi wanasema kinda huyo hana mkataba na Azam.
0 comments:
Post a Comment