Na Prince Akbar
WACHEZAJI 13 wameripoti kwenye mazoezi ya Simba SC jioni
hii, wakiwemo Kiggi Makassy aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu, Yanga ingawa
mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Davis
Mrwanda hakutokea.
Mashabiki wengi wa Simba walifika mapema Uwanja wa TCC Chang’ombe,
Dar es Salaam jioni hii kuwashuhudia wachezaji wao, kiu zaidi ikiwa kumuona
mpachika mabao wao wa zamani, aliyerejea kikosini Mrwanda, lakini Meneja wa Simba,
Nico Nyagawa akaiambia BIN ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo ni
miongoni mwa waliotoa udhuru.
Waliohudhuria ni pamoja na Salim Kinje, Abdalllah Juma, William
Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun Athumani, Haruna Shamte, Amri Kiemba,
Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu Mbivayanga na Abdallah Seseme.
Mazoezi hayo yaliongozwa na Kocha wa Mazoezi ya Viungo,
Mganda Hamatre Richard kwa sababu Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovick bado
anakula sikukuu kwao.
Simba itaendelea na program ya mazoezi kwa jioni tu wiki hii
na Nyagawa amesema anatarajia idadi ya wachezaji itakuwa ikiongezeka taratibu
wiki hii, wakiwemo wachezaji waliokuwa na timu ya taifa Msumbiji nao pia wanatarajiwa
kuungana na wenzao wakirejea kutoka nchini humo.
Mrwanda ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea
Simba, ambao hauna kipengele cha kumruhusu kuuvunja kabla haujamalizika naye
anatarajiwa kuanza maozezi wakati wowote wiki hii.
Mrwanda, awali ilielezwa anataka kusaini mkataba ambao
wakati wowote akipata timu nje, aondoke, lakini kwa mujibu wa mkataba aliosaini
Simba ni kwamba akipata timu italazimika kumnunua kutoka kwa Wekundu wa
Msimbazi, au isubiri hadi amalize mkataba.
Habari za uhakika, kutoka ndani ya Simba SC ambazo BIN
ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mrwanda ameridhika na mkataba huo na
ameahidi kufanya vitu baab kubwa Msimbazi.
Kwa upande mwingine, Simba SC imeamua kumtema kiungo Salum
Machaku kwa makubaliano maalum ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba. Simba
ilitaka kumtoa kwa mkopo Machaku, lakini mwenyewe akasema bora aachwe moja kwa
moja.
Tayari Simba imemsajili kiungo wa Yanga, Kiggi Makassy
kuziba nafasi ya Machaku. Machaku sasa ameingia kwenye mazungumzo na Yanga.
Simba SC inajiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Timu nyingine za Tanzania zitakazoshiriki michuano hiyo ni mabingwa watetezi, Yanga na washindi wa pili wa Ligi Kuu Azam FC.
Azam pia wameshaanza kujifua kwenye Uwanja wao wa Chamazi, wakati Yanga wanatarajiwa kuanza kesho Uwanja wao wa Kaunda, Jangwani, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment