Kikosi cha Yanga |
YANGA inaendelea vizuri na maandalizi yake ya pambano la
funga dimba Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi wiki hii, huku wachezaji
wa timu hiyo wakisema hawataki kumuona kambini Kiromo Hotel, Bagamoyo, kocha
Mserbia Kostadin Bozidar Papic.
Yanga inaendelea na program za mazoezi ya asubuhi na jioni chini
ya kocha Fred Felix Isaya Kataraia Minziro ‘Majeshi’ kwenye Uwanja wa Mwanakalenge,
Bagamoyo na wachezaji wana ari kubwa ya ushindi.
Wachezaji wote wanaonekana wana ‘hasira’ kweli za kuua mnyama
Jumamosi na wanajifua kwa bidii.
Yanga ambayo imepoteza matumaini hata ya kupata nafasi ya pili
msimu huu, baada ya kuzidiwa kete na Simba na Azam zinazochuana kuwania ubingwa,
itaingia kwenye mechi hiyo kusaka ushindi kwa ajili ya kulinda heshima tu.
Lakini kwao, wataingia huku sala za Azam zikiwa upande wao,
kwani wakifanikiwa kumfunga Simba na Azam ikashinda mechi ya mwisho dhidi ya
Kagera Sugar, itakuwa bingwa kwa wastani wa mabao.
Lakini Yanga wanaingia kumenyana na Simba ambayo iko vizuri
na ina morali ya hali ya juu, ikitoka kuifunga Al Ahly Shandy ya Sudan mabao
3-0 kwenye mechi ya kwanza, hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba yenyewe imeweka kambi visiwani Zanzibar kujiandaa na
mchezo huo, ambao kwao sare tu itawatosha kutawazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu
msimu huu.
Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, Simba ililala 1-0 mwaka
jana bao pekee la Mzambia Davies Mwape- lakini awali Yanga ilifungwa kwenye
mechi ya Ngao ya Jamii 2-0 mabao ya Mzambia Felix Sunzu na Haruna Moshi ‘Boban’,
ikitoka kushinda 1-0 katika fainali ya Kombe la Kagame, bao la Mghana Kenneth
Asamoah.
Papic kwa sasa yuko Dar es Salaam tangu baada ya mechi dhidi
ya Kagera Sugar, Yanga ikilala 1-0, ikitoka kufungwa na Toto African 3-2.
Yanga ilicheza mechi mbili zaidi na kushinda 3-0 dhidi ya Polisi
Dodoma na 4-1 dhidi ya JKT Oljoro bila Papic, ambaye kibali chake cha kufanya
kazi nchini kimemaliza muda.
Yanga imeamua kupuuza kumkatia kibali kingine Papic kwa
sababu haina mpango wa kuendelea na msimu unafikia tamati Jumamosi na imejenga imani
juu yake beki wake wa zamani, Minziro.
0 comments:
Post a Comment