Mzee Akilimali katikati, Mhika kushoto na Chakupewa kulia |
HAMKANI si shwari tena ndani ya klabu ya Yanga ya Dar es
Salaam, kufuatia kuibuka mgogoro mwingine ndani ya klabu hiyo wa uongozi.
Nasema ni mgogoro wa uongozi, kwa sababu kinachoonekana ni
kuendelea kwa vita ya kumng’oa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Wakili Lloyd Baharagu
Nchunga.
Mjumbe wa kuteuliwa wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad
‘Magari’ alijiuzulu wiki iliyopita, akitoa sababu kutoridhishwa na mwenendo wa
uongozi.
Seif alitoa shutuma nyingi tu kwa Kamati ya Utendaji ya
Yanga- yaani kwa ujumla inaonyesha amekatishwa tamaa na hali ya mambo ndani ya
klabu.
Siku moja baadaye Mjumbe wa Kamati ya Mashindano na Usajili,
Abdallah Ahmad Bin Kleb naye alijiuzulu, akitoa sababu ambazo zinashibihiana na
za Seif.
Hatua hizi zinakuja katika wakati ambao, Yanga imeshindwa
kukonga nyoyo za mashabiki wake msimu huu, baada ya kukosa japo nafasi ya pili
kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu- lakini mbaya zaidi mwakani
haitacheza michuano ya Afrika, labda itokee bahati Simba SC ifanikiwe kuingia
hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Yanga inaweza kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la
Soka Afrika mwakani, iwapo itashika nafasi ya tatu mwishoni mwa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Lakini hiyo ni iwapo tu, Simba SC itafanikiwa kuingia hatua
ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hiyo ni kwa mujibu wa kanuni mpya za mashindano ya klabu
Afrika za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwamba nchi ambazo kwa sasa zina
nafasi moja moja za kuingiza timu kwenye michuano ya klabu, zitakuwa
zikiongezewa nafasi moja moja katika michuano ambayo klabu yake imefanikiwa kuingia
hatua ya makundi.
Kwa mfano mwaka huu Sudan imeshirikisha timu nne kwenye
michuano hiyo, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho, kwa sababu
msimu uliopita iliingiza timu zake kwenye hatua za makundi za michuano yote
hiyo.
Tanzania bado ina nafasi moja moja tu ambazo hadi sasa
tayari Simba na Azam zimejihakikishia kucheza kwa msimu ujao.
Simba SC imeonyesha dalili za kuifungulia njia Tanzania
kuingiza timu tatu kwenye michuano ya Afrika mwakani, moja Ligi ya Mabingwa na
mbili Shirikisho, baada ya kujiwekea mazingira mazuri ya kuingia kwenye hatua
ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Al Ahly Shandy mabao 3-0
katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo, kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam Jumapili.
Sasa Simba inahitaji sare yoyote au kufungwa si chini ya
mabao 2-0, ili kuungana na timu nane zitakazotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa
kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho.
Maana yake- Simba ikiitoa Al Ahly Shandy itacheza na timu
iliyotolewa Ligi ya Mabingwa ili kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi.
Lakini iwapo Simba itakosa nafasi ya kuingia Nane Bora,
Yanga nayo italazimika kusubiri hadi msimu ujao kupigania tiketi ya kucheza
michuano ya Afrika mwaka 2014.
Baada ya Seif na Bin Kleb kujiuzulu, kilichofuatia ni
viongozi wa Baraza la Wazee la klabu hiyo kujitokeza na kusema wanataka
kuchukua timu waihudumie, kwa sababu wameona Kamati ya Utendaji imeshindwa.
Wazee walisema wamezungumza na Mwenyekiti na amewakubalia,
lakini siku moja baadaye Nchunga akaibuka na kuwasuta.
Nchunga aliwaambia Baraza la Wazee la klabu hiyo, waliotaka
kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni, akisema wamuonyeshe
vielelezo vya vyanzo vyao vya mapato awape timu.
Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa
Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb,
wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari
kuachia ngazi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari makao
makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wakili
Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha mwishoni mwa
wiki ilikubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
Kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya
nao kikao na akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa
Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao vya fedha ili
ajue uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa
watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye
matatizo.
Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya
mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi
madaraka ya uongozi.
Tangu hapo Wazee kimya, hawajasikika tena na jana timu
ilitarajiwa kuingia kambini Bagamoyo kujiandaa na mpambano wa funga dimba Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC Mei 5,
mwaka huu.
Kitendo cha Nchunga kupeleka timu kambini Bagaamoyo,
kinaashiria Baraza la Wazee la klabu hiyo limekwama kuiteka timu kama
lilivyodhamiria, ingawa jana kulikuwa kuna habari kwamba Wazee walipanga
kukutana na Waandishi.
Ukifuatilia kwa kina unaweza kuona hapa kinachoendelea kina
chembechembe za ‘bifu’ la Nchunga na aliyekuwa Makamu wake Mwenyekiti Davis
Mosha.
Mosha alijiuzulu Machi mwaka jana baada ya kutofautiana na
Nchunga- na tangu hapo inaelezwa amekuwa msituni kuhakikisha Nchunga hakai
Yanga.
Ndiyo, nasema hivyo na wala sihofii chochote kwa sababu
uvumi huo umeenea sana. Inadaiwa Mosha yuko msituni anataka kumuonyesha
Nchunga.
Lakini kama ni kweli, basi vita hii ya Mosha na Nchunga
itaifikisha wapi Yanga zaidi ya kuiharibia tu?
Hao Wazee wa Yanga wadaiwa kutumiwa na inadaiwa ni kawaida
yao kutumiwa hadi imefikia wakati wanajivunjia heshima mbele ya wana Yanga.
Kama ni kweli, wanatumiwa, Wazee wa Yanga wanapaswa
kujitambua na kusimamia wajibu wao- kama watu wanaoaminika kuwa na hekima na
busara, ambavyo mwisho wa siku vitakuwa suluhisho la matatizo sugu ndani ya
klabu.
Lakini itakuwa ajabu wao wakiwa ndiyo chanzo cha matatizo
ndani ya klabu.
Inawezekana kweli kama wengi wanavyoamini Nchunga ana
matatizo, lakini basi watu wasipambane naye bila kujali wanaiumiza aje klabu.
Walisema wahenga vita ya mafahari wawili, ziumiazo nyika na
katika vita hii ya Mosha na Nchunga inayoumia ni Yanga.
Binafsi nawapenda wote na sipendi huu ugomvi wao wa kitoto,
zaidi napenda wamalize tofauti zao na wakae pamoja kuongoza Yanga.
Mosha ni mwana Yanga mzuri, kijana, mtoto wa mjini, ‘ananuka
fedha’, jasiri na mpambanaji. Nchunga ni kichwa- ana akili sana, hekima, busara
na subira. Zaidi ni mwa mwasheria angavu.
Lakini pamoja na sifa hizo, wote wana mapungufu yao ya
kibinadamu ambayo mimi na wewe msomaji pia tunayo.
Mzee Ibrahim Akilimali namfahamu siku nyingi sana-
nilikutana naye kwa mara ya kwanza kwenye uchaguzi wa Yanga mwaka 1993 katika
ukumbi wa Uwanja wa Ndani wa Taifa, ambao Dk Jabir Katundu aliibuka mshindi
kwenye nafasi ya Uenyekiti na George Mpondela ‘Castro’ Katibu Mkuu.
Siku hiyo, Akilimali alitaka kugombea Uenyekiti, lakini
alipofika ukumbini akaona jinsi ambavyo Dk Katundu anaungwa mkono akataka
kubadilisha nafasi pale pale, agombee Umakamu- wasimamizi wa Uchaguzi
wakamuambia utaratibu huo hauwezekani mzee, amua kujitoa au kuendelea kugombea
nafasi hiyo hiyo.
Namheshimu huyu mzee, tena sana, mzee Hashim Mhika huyu Best
wangu sana- na wazee wote wa Yanga ni rafiki zangu, hadi wale ambao wamejiweka
mbali na klabu kwa sasa akina Yussuf Mzimba.
Nataka niwaambia wazee wa Yanga, wasikubali kuendeshwa na
watoto wao akina Mosha Nchunga. Mzee Akilimali lazima ajue, anapotumiwa (haimaanishi
anatumiwa) kwa uasi na Mosha au Nchunga, basi anajishushia thamani yake.
Wazee wa Yanga wasimamie wajibu wao kama Wazee ili
waheshimiwe na waogopwe na vijana. Lakini inapofikia hadi Yanga Bomba
wanawadharau wazee kama ilivyo sasa, hiyo ni mbaya sana.
Na wana Yanga wasikubali kudanganywa- kama kosa lilifanyika
katika uchaguzi kwa Joel Bendera na Ridhiwani Kikwete kuuvuruga uchaguzi na
hatimaye akachaguliwa mtu ambaye hakuwa chaguo la wengi, suluhisho lake si
kumhujumu akiwa madarakani.
Nawakumbusha wana Yanga waliokuwapo kwenye uchaguzi siku
ile, Yussuf Manji hakuwa anamkubali Nchunga, lakini alipoona kwamba ni mtu
aliyetayarishwa lazima awe, akakubali na akamuunganisha na Francis Kifukwe na
Mbaraka Igangula, washirikiane katika kuijenga Yanga.
Nchunga hatakaa milele Yanga, lakini Yanga itaendelea kuwapo
hata baada ya kizazi hiki. Na kama kweli unaipenda Yanga, kwa nini uihujumu kwa
sababu humpendi Nchunga? Sioni mantiki ya huu unaitwa mgogoro unaoendelea sasa
Yanga- naona ni vyema Wazee wa Yanga wakasimamia wajibu wao, wawakutanishe
Nchunga na Mosha wamalize tofauti zao, wakae pamoja madarakani kuongoza timu.
Naamini, yakiisha ya Nchunga na Mosha- hata matatizo ya Seif
na Bin Kleb yataisha pia.
Kaulimbiu ya Yanga ni daima mbele, nami nasema yaliyopita si
ndwele, ni juu yao sasa Wazee na akina Nchunga na Mosha kusuka au kunyoa.
Wasalaam.
0 comments:
Post a Comment