![]() |
Van Basten |
UNAPOMTAJA
Marcel ‘Marco’ van Basten, unamaanisha mmoja wa wachezaji waliowahi kung’ara na
timu ya taifa ya Uholanzi, ambaye hadi leo bado anaheshimika katika kizazi cha
zama za kati za soka la kuvutia la nchi hiyo.
Van
Basten alizaliwa Oktoba 31, 1964 mjini Utrecht, Uholanzi na kuanza kusakata
soka kwenye timu ya mtaani kwao ya EDO, alipokuwa na umri wa miaka saba na
mwaka uliofuata akahamia UVV Utrecht, alikodumu kwa miaka 10 kabla hajacheza
kwa muda kwenye klabu ya Elinkwijk.
Amejijengea
heshima kuwa mmoja wa washambuliaji wakali zaidi wa Uholanzi, akiwa mchezaji wa
timu ya taifa ya nchi hiyo miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990, akiwa pia
mchezaji wa AFC Ajax na AC Milan ,
ambaye sasa ni kocha.
Amepachika
nyavuni mabao 277 akiwa kwenye soka la juu, huku akikutwa mara kwa mara na
majeraha yaliyokuwa yakimkabili. Baadaye alikuwa kocha wa AFC Ajax na timu ya
taifa.
Akicheza
soka la kiufundi na mashuti makali, van Basten alitajwa kuwa mwanasoka bora wa
Ulaya kwa miaka mitatu (1988, 1989 na 1992) na mwaka 1992 akawa mwanasoka bora
wa dunia.
Kwenye
upigaji kura kumsaka mwanasoka bora wa karne ulioendeshwa na gazeti moja la
Ufaransa, van Basten alikamata nafasi ya 25 huku akiwa nafasi ya nane kwa nchi
hiyo.
Machi
2007, Sky Sports ilimtangaza van Basten kama
mwanasoka bora namba moja miongoni mwa waliolazimika kuachana na soka mapema.
Alisajiliwa
na AFC Ajax msimu wa 1981–82 na alicheza mechi ya kwanza na timu hiyo Aprili
1982 na kufunga bao lake la kwanza kwenye ushindi wa mabao 5–0 dhidi ya NEC.
Alicheza
mashindano ya Ulaya msimu wa 1982–83, akipambana na mfungaji bora wa Ulaya
wakati huo, Wim Kieft, kwenye nafasi ya ushambuliaji na kufunga mabao tisa
kwenye mechi 20 za ligi. Kieft alihama msimu uliofuata na kumwachia namba ya
kudumu van Basten.
![]() |
Van Basten |
Alikuwa
mfungaji bora wa ligi kuanzia msimu wa 1983–84 hadi 1986–87, akifunga mabao 117
kwenye mechi 112. Msimu wa 1985–86 aliweka kimiani mabao 37 kwenye mechi 26 za
ligi, ikiwa ni pamoja na mabao sita ya mechi dhidi ya Sparta Rotterdam na
matano dhidi ya Heracles Almelo na kushinda kiatu cha dhahabu cha Ulaya. Pia
alifunga bao la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Washindi Ulaya kwenye mechi
dhidi ya Lokomotive Leipzig mwaka 1987.
Mwaka
1988, Silvio Berlusconi wa AC Milan alimsajili pamoja na magwiji Ruud Gullit na
Frank Rijkaard. Katika msimu wa kwanza, Milan
ilishinda kombe la Scudetto baada ya miaka nane, lakini van Basten,
akisumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, alicheza mechi 11 tu.
Msimu
wa 1988–89, van Basten alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya akiwa maefunga
mabao 19 kwenye Serie A na mawili kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Ulaya
(Klabu Bingwa) dhidi ya Steaua Bucureşti.
Msimu
uliofuata aliongoza tena ufungaji kwenye Serie A na kuisaidia Milan kutetea taji la Ulaya kwa kuichapa SL
Benfica kwenye mechi ya fainali, lakini ikapokonywa taji la Italia, Scudetto na
Sampdoria msimu uliofuata.
Baada
ya van Basten kukosana na kocha Arrigo Sacchi, Berlusconi akamtimua kocha huyo
na kumpa kazi Fabio Capello msimu uliofuata na kuifanya Milan imalize ligi bila
kufungwa, huku van Basten akifunga mabao 25 na kuipa taji la Italia timu hiyo
na yeye kuwa mwanasoka bora tena.
Novemba
1992, alikuwa mchezaji wa kwanza kupachika mabao manne kwenye mechi ya Ligi ya
Mabingwa siku walipopambana na IFK Göteborg ya Sweden .
Timu
hiyo iliendeleza rekodi ya kutofungwa msimu wa 1992–93 na kucheza mechi 58 zaidi
kabla ya kupata kichapo cha kwanza. Soka la van Basten lilikuwa la hali ya juu
msimu huo na kupata tena uanasoka bora wa Ulaya, hivyo kufikia rekodi ya
magwiji, Johan Cruyff na Michel Platini kushinda tuzo hilo mara tatu.
Tatizo
la kifundo cha mguu lilirejea tena wakati wa mechi dhidi ya AC Ancona na
kumlazimisha kurejea kwenye mlolongo wa upasuaji. Alirejea kwenye mechi chache
za mwisho wa msimu kabla Milan
haijalitema taji la Ulaya kwa Olympique de Marseille.
Mechi
hiyo ya fainali ilikuwa ya mwisho kwake kuchezea klabu hiyo ya Italia. Miaka
miwili iliyofuata ilikuwa ni ya kusaka kurejea kwenye fomu, lakini hatimaye
akatangaza kustaafu mwaka 1995, akiwa na umri wa miaka 30 tu.
Baada
ya hapo alicheza soka ‘la ukubwani’ wakati wa mechi ya maonyesho ya Demetrio
Albertini kwenye Uwanja wa San Siro, Machi 2006 na kufunga bao la kichwa kabla
ya kutolewa mwanzoni mwa kipindi hicho cha kwanza.
Julai
22, 2006, alicheza mechi ya maonyesho wakati wa kuadhimisha miaka 11 ya Dennis
Bergkamp akiwa Arsenal, na hii ilikuwa ndio mechi ya kwanza kuchezwa kwenye
Uwanja wa Emirates, akichezea upande wa maveterani wa Ajax . Aliingia kipindi cha pili akiwa na Johan
Cruyff.
Pamoja
na umwamba wake uwanjani, akiwa amewahi kuifunga England kwa ‘hat-trick’,
akiifunga pia Ujerumani na Urusi wakati huo mabao yote yakiwa ya ushindi kwa
nchi yake kwenye mashindano ya kimataifa, lakini van Basten hakuwahi hata mara
moja kufunga bao kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Katika
nusu fainali ya Euro 1992, Uholanzi ilipoteza mechi kwa mikwaju ya penalti
dhidi ya Denmark ,
huku Peter Schmeichel akipangua shuti la penalti la van Basten.
Baadaye
alianza kazi ya ukocha, ingawa alipostaafu mwaka 1995 alisema asingethubutu
kugeukia ukocha. Lakini baadaye alisomea kazi hiyo kwenye chuo cha Royal Dutch
Football Association (KNVB) na akaanza kazi akiwa msaidizi wa mchezaji mwenzake
wa zamani, John van't Schip kwenye timu ya pili ya AFC Ajax mwaka 2003–04. Julai
2004 akatajwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uholanza, akisaidiwa na van't
Schip.
Alianza
kuonyesha misimamo mikali kama bosi kwa kuwatema wachezaji wenye majina makubwa
kama Clarence Seedorf, Patrick Kluivert, Edgar Davids na Roy Makaay, huku
akimweka benchi Mark van Bommel, kwa madai kuwa ama wamepitwa na wakati au
wameshindwa kuisaidia timu ya taifa.
Na
huenda kwa mara ya kwanza ndani ya miongo kadhaa, hakuna mchezaji tegemeo
kwenye timu ya taifa aliyeitwa kutoka klabu tatu kubwa; AFC Ajax, PSV na
Feyenoord huku akitaka kumwita mshambuliaji Salomon Kalou, lakini mamlaka za
uhamiaji zikamnyima uraia wa Uholanzi kabla Kalou hajakubali wito wa nchi yake,
Ivory Coast .
Ingawa
ilitinga fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 bila kufungwa, Uholanzi ilijikuta
ikichapwa bao 1–0 na Ureno na kutupwa nje wakati wa mtoano, kisha van Basten kukosolewa
kwa kumwacha Ruud van Nistelrooy (aliyeifungia Uholanzi mabao 28) kabla ya
mechi hiyo, na kumchukua Dirk Kuyt ambaye hakufunga hata bao moja kwenye
mashindano hayo.
Ingawa
maofisa wa soka walitaka van Basten aiongoze timu ya taifa hadi wakati wa
kusaka tiketi ya kwenda Afrika Kusini, mwenyewe aliingia mkataba wa miaka minne
na AFC Ajax Februari mwaka 2008, lakini ikiwa ni baada ya kuiongoza Uholanzi
kwenye Euro 2008 na kufungwa robo fainali na Russia ya Guus Hiddink. Aliachana
na Ajax Mei 2009, baada ya timu hiyo kushindwa kupata nafasi ya Ligi ya
Mabingwa.
WASIFU
WAKE:
JINA:
Marcel van Basten
KUZALIWA:
31 Oktoba 1964 (1964-10-31) (age 46)
ALIPOZALIWA:
Utrecht , Netherlands
KLABU
ALIZOCHEZEA:
Mwaka
Klabu
1982–1987
Ajax (Mechi 133, mabao 128)
1987–1993
AC Milan (Mechi 147, maba 90)
(Tangu
1983 hadi 1992, aliichezea Uholanzi mechi 58 na kuifungia mabao 24)
0 comments:
Post a Comment