Nyosso |
KLABU ya Yanga ya Dar es Salaam inataka kuchukua wachezaji
watatu kutoka Simba, ambao mikataba yao inaisha karibuni- hao ni mabeki Juma
Jabu, Juma Nyosso na kiungo Uhuru Suleiman.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani
ya watu ambao wamepewa jukumu la kufanya usajili Yanga, zimesema kwamba
wachezaji wote hao wamekwishafanya nao mazungumzo na wamefikia mwafaka, ingawa
bado hawajasaini.
“Fedha itatoa haraka, watasaini, kwa sababu tunatengeneza
timu ya kucheza Kombe la Kagame,” kilisema chanzo chetu kutoka Yanga.
Aidha, Yanga pia ipo kwenye mpango wa kusajili washambuliaji
wawili ‘pacha’ wa timu ya taifa ya Rwanda, Meddie Kegere na Olivier Karekezi,
ambao waling’ara sana kwenye Kombe la CECAFA Challenge mwaka jana Dar es
Salaam, Amavubi ikifungwa na The Cranes kwenye fainali.
“Mazungumzo na hao wachezaji wa Rwanda yalikwishafanyika
siku nyingi na tumekuwa tukiwasiliana nao kwa kipindi chote hiki, mambo
yanaendelea vizuri na watakuja hapa,”kilisema chanzo kutoka Yanga.
Kiunganishi kuu cha wachezaji wa Rwanda na Yanga ni mfanyabiashara,
Abdallah Ahmed Bin Kleb ambaye amewekeza nchini humo. Bin Kleb ndiye aliyemsajili
kwa fedha yake, kiungo ‘baab kubwa’ wa APR, Haruna Niyonzima msimu uliopita.
Fungu la usajili wa wachezaji Yanga linatoka kwa mfadhili wa
klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji ambaye ameteua Kamati Maalum kusimamia Usajili
pamoja na ajira ya kocha mpya, atakayerithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar
Papic aliyetupiwa virago ‘kiaina’.
Uhuru |
Jabu |
Baaada ya Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga
kujiuzulu, klabu hiyo sasa ipo chini ya Baraza la Wadhamini na Sekretarieti ya
klabu chini ya Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame na wamepania
kutetea taji hilo, ili kupoza hasira za mashabiki wao baada ya msimu mbaya
uliopita, wakipoteza ubingwa wa Ligi Kuu, sambamba na kukosa hata nafasi ya
kucheza michuano ya Afrika, ikiwa ni pamoja na kufungwa 5-0 na wapinzani wao wa
jadi, Simba katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu.
0 comments:
Post a Comment