KIUNGO wa Azam FC aliyecheza kwa mkopo msimu huu, African
Lyon ya Dar es Salaam, Suleiman Kassim ‘Selembe’ amesema kwamba Coastal Union
ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, ndizo ambazo hadi sasa zimeonyesha nia ya
kumsajili, ila anapenda kukabiliana na changamoto kubwa zaidi, kama za Simba au
Yanga.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY visiwani Zanzibar leo
asubuhi, Selembe (pichani kushoto) alisema kwamba klabu yake, Azam FC imeonyesha nia ya kumuacha
aende klabu yoyote itakayomtaka na sasa naye anasikilizia timu ambayo
itamalizana naye.
“Kwa kweli hadi sasa naweza kusema Coastal Union na Mtibwa
ndizo ambazo zimeonyesha nia haswa ya kunisajili, ila mimi mwenyewe niko tayari
kukabiliana na changamoto zozote, hasa zile kubwa kubwa, kama Simba au Yanga
hivi, niko tayari,”alisema.
Selembe ni kati ya viungo wazuri kwa sasa nchini, ambaye ameyumba
kidogo baada ya Azam kumpeleka kwa mkopo Lyon, kiasi cha kufikia kutemwa katika
kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa sasa, fundi huyo wa soka yuko kwenye kambi ya timu ya
Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya Kombe la Dunia ya nchi zisizo wanachama wa
FIFA nchini Uzbekistan, michuano itakayoanza Juni 4, mwaka huu na Zanzibar
Heroes inatarajiwa kuondoka Juni 2 nchini.
0 comments:
Post a Comment