KATIKA sheria 17 za soka, sheria ya kwanza
ni Uwanja. Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linatoa uzito mno katika
suala la Uwanja.
Kwa nini Uwanja? Katika akili ya kawaida,
kama tunataka kucheza soka, jambo la kwanza na la msingi kutilia mkazo ni
Uwanja.
Ndiyo, ni hivyo. Lakini je, viongozi wa
klabu zetu kongwe nchini Simba na Yanganao wana frikra kama hizo? Sidhani.
Wakati tumekaribia mno kwenye kilele cha sherehe za miaka yetu 50 ya Uhuru,
Simba na Yanga zinafurajia kuwapo kwa zaidi ya 75 na ushehe tangu kuanzishwa
kwake.
Wakati huo huo, nchini kuna klabu nyingine
za soka zinakimbiza siku ili angalau zitimize muongo mmoja tu tangu kuanzishwa
kwake.
Ila leo akija mgeni na kutambulishwa kwa
klabu zote nchini, zikiwemo ambazo zina miaka zaidi ya 75 tangu kuanzishwa
kwake na zile change, itakuwa vigumu kumshawishi akubaliane na hali halisi.
Mpokee mgeni na uanze kumtembeza- anzia
Mtaa wa Msimbazi, muonyeshe makao makuu ya klabu ya Simba, ajionee lile jingo
chakavu na lile pembeni yake ambalo halijaisha.
Mtoe hapo mpelekea makutano ya mitaa ya
Twiga na Jangwani- muonyeshe makao makuu ya klabu ya Yanga- ajionee eneo kubwa
linaloweza kuwa la kifahari siku moja tu, akipatikana mtu wa kuliendeleza.
Baada ya hapo, mpeleke Mbagala, eneo la Chamazi
ambako kuna makao makuu ya Azam FC na muonyeshe Uwanja mpya mdogo na wa kisasa
mithili ya viwanja vingi ambavyo vipo nchi za Scandinavia barani Ulaya.
Mkutanishe na Patrick Kahamele, amtembeze
kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya soka klabu, ikiwemo soka ya vijana.
Mkutanishe na wenye timu wampe mipango yao
ya baadaye- tena iliyo katika maandishi na mikakati ya utekelezaji wake.
Baada ya hapo mpe wasifu wa hizo klabu
kwamba Simba na Yanga zipo tangu nchi hii haijapata Uhuru na Azam haina hata
miaka mitano tangu ianzishwe.
Lazima atashangaa. Lazima atastaajabu. Hii
nini maana yake? Viongozi wa Simba na Yanga bado hawajajitambua. Bado
hawajatambua soka inahitaji vipaumbele gani na kama hivyo ndivyo.
Inaonekana dhahiri viongozi wa Simba na
Yanga hawana dira wala mipango na watu wa aina hiyo, kutoka mikononi mwao ni
vigumu mno klabu hizo kupiga hatua, hata ndogo ndogo tu za kimaendeleo.
Ukubwa wa majina ya Simba na Yanga na
umaarufu wake, pekee ni mtaji mkubwa wa kuendesha klabu hizo, ambao
inasikitisha hadi haujatumiwa na viongozi wa klabu hiyo kuzinufaisha klabu
hizo.
Bado inasikitisha kuona hadi kesho,
kitegauchumi kikubwa cha Simba na Yanga ni ‘bakuli’- yaani kutembea kwa
matajiri na wafanyabiashara kuomba misaasa.
Kwa sasa Yanga wana mgogoro na chanzo ni
hali mbaya ya kifedha ndani ya klabu, kama ilivyoanishwa na Wajumbe wawili
waliong’atuka, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Bin Kleb na wakati Fulani ilibidi
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aende kumbembeleza Yussuf
Manji arejeshe ufadhili wake kwenye klabu hiyo.
Dhahiri, Nchunga aliamua kufanya hivyo
baada ya kuona mambo ni magumu na klabu haiwezi kujiendesha bila msaada.
Lakini Nchunga labda tu awe hajui historia
ya klabu yake- ni klabu ambayo hadi mwaka 1975, ikiwa haina ufadhili wowote,
tayari ilikuwa ina majengo yake mawili, dogo Mtaa wa Mafia na hilo kubwa la
Jangwani, ambalo linaambatana na Uwanja wa Kaunda.
Ilikuwa ina mabasi yake ambayo mengine
yalikuwa yanatumika kwa shughuli za klabu na mengine yanatumika kibiashara.
Kadhalika kwa Simba, hadi 1975 ilikuwa ina
jengo lake wakati huo likiwa la kifahari na linalong’ara na kuupendezesha Mtaa
wa Msimbazi- miaka hiyo Mwenyekiti wa Simba Alhaj Ismail Aden Rage aliwahi
kufika Dar es Salaam na kujaribu kutaka kuichezea klabu hiyo, lakini kiwango
chake kidogo hakikumpa nafasi, aliishia kujaribiwa kwenye mechi kadhaa.
Simba ilikuwa ina mabasi pia- na haikuwa na
mfadhili yoyote, zaidi ya ujanja na fikra za viongozi wa klabu hiyo.
Unaweza kuona kabisa hali ilivyo leo Simba
na Yanga ukilinganisha na miaka hiyo, maana yake haziendelei zaidi ya kudumaa.
Wengi wanaamini elimu kubwa ndio msingi wa maendeleo- sahihi kabisa. Leo
viongozi wa Simba na Yanga ni wenye elimu za viwango vya juu na wana taaluma.
Rage Mhasibu na Nchunga Mwanasheria.
Lakini viongozi wa Yanga wa miaka hiyo, hawakuwa
na elimu kubwa, ila mambo waliyoyafanya yanawafanya thamani yao iwe juu kuliko
hawa waliokaa shule muda mrefu.
Dunia ya leo ni nyepesi mno kwa mtu ambaye
kweli anataka maendeleo. Taasisi kubwa kama zilivyo Simba na Yanga hivi sasa
zinakopesheka na mabenki ni mengi mno nchini ambayo yanaweza yakazipa mikopo
klabu hizo zifanye miradi yao ya maendeleo.
Yanga wana Uwanja wa Kaunda ambao wanaweza
kuuboresha, ukawa Uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kukusanya hata watu 20, 000
katika mechi moja na kuujingizia fedha nyingi.
Hivi kweli Yanga wamekwishazungumza hata na
mdhamini wao tu Kilimanjaro Beer juu ya kuwasilisha programu ya kuuendeleza
Uwanja wa Kaunda?
Naamini, TBL watakuwa tayari kutumia kuta
za Uwanja wa Kaunda kujitangaza kibiashara- iwapo Yanga watawasilisha mapendekezo
ya mradi yaliyosimama.
Watu 20,000 kila wiki mara mbili
wanamiminika Uwanja wa Kaunda kutazama mechi- au watu wasiopungua 5,000 kila
siku kwenye mazoezi ya kikosi cha kwanza- ni kiasi gani TBL itakuwa inanufaika?
Lakini Yanga nayo itakuwa inapata kiasi cha
fedha?
Azam ‘walilaani’ kweli Uwanja wa Taifa
ulipofunguliwa, kwani yale makato ya Uwanja waliyokuwa wanayapata kila mechi
ambayo SImba au Yanga ilicheza Chamazi yaliota mbawa. Sasa tunataka nini ili
kujua umuhimu wa kuwa na Uwanja?
Lakini si TBL tu, yapo makampuni mengine
ambayo yanajua soka ina wapenzi wengi na yanaweza kunufaika kwa kuwekeza huko,
je Yanga wamekwishayafikia?
Mradi wa ujenzi barabara ya Jangwani
inalifanya eneo hilo liwe mjini kabisa na kuuweka sokoni zaidi Uwanja wa Yanga-
je Nchunga na viongozi wenzake wanafikiria nini?
Azam wamejenga Uwanja wao Mbagala na
tumeshuhudia msimu huu mashabiki wa Simba na Yanga wakienda kuzishangilia timu
zao kwenye Uwanja huo, inakuwaje Simba wanashindwa kujenga Uwanja nje ya mji
japokuwa walishindwa kuwa na eneo mjini?
Soka ni biashara kubwa ambayo mtaji wake
mkuu ni Uwanja- ndio maana klabu zote Ulaya hata ndogo zina viwanja vyake.
Ulaya itaendelea kuwa kioo chetu daima.
Wanachokifanya Rage na Nchinga kwa sasa ni
kitu ambacho hata Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu) na Hassan Daalal
walikifanya klabu yao.
Uongozi wa staili ya kusajili wachezaji,
kuweka timu kambini, kuisafirisha mikoani kucheza mechi na kukusanya mapato ya
milangoni, hata yule mwanachama wa Simba mlemavu anayeitwa Kipukuswa au Soud
Tall wa Yanga wanaweza kuufanya.
Nani atashindwa? Lakini Rage na Nchunga
wanapaswa kujitambua sasa na kuhakikisha wanafanya kitu ambacho kitawafanya
wakumbukwe na kuwa sehemu ya historia ya klabu hizo.
Wasome historia ya Simba na Yanga na baada
ya hapo waache blah blah na usanii, ni mambo ambayo yamekwishapitwa na
wakati.
Waonyeshe wanajiamini na kutumia ukubwa wa
majina ya klabu hizo na umaarufu wake kuzipatia mafanikio klabu hizo.
Ona sasa Azam inayowaacha ‘uchi’- timu ya juzi
tu, lakini ina mipango. Na hapa kisingizio kisiwe Bakhresa ana fedha hapana,
ana mipango na malengo, kwani wapo wenye fedha waliojaribu kuwekeza kabla yake,
mfano Mohamed Dewji, Alex Kajumulo na Merey Balhaboub na wakafeli.
Bado naamini Simba na Yanga kila moja ni
tajiri kuliko Bakhresa, ila sasa hazina watu wenye kuweza kuchimba dhahabu,
kusafisha na kuiingiza sokoni. Na kwa mtaji huu, zitaendelea kuwa za
kubahatidha tu- mfano Simba mwaka huu wanafanya vizuri Afrika, baada ya hapo
hadi miaka 10 tena baadaye.
Ndiyo- nani asiyejua mafanikio ya Simba ni
ya kubahatisha? Walikuwa wana mipango gani mwanzoni mwa msimu hata tuseme
wanavuna walichopanda? Weka unazi kando- jadili hili kwa kina, ukirejea ule
usajili wa kubahatisha bahatisha- ambao chupuchupu umtupe nje ya kikosi Emmanuel
Okwi msimu huu, ambaye sasa ndiye anaibeba timu?
Au tumesahau jamani, huyu mchezaji si
alikwenda Afrika Kusini na klabu ilikuwa tayari kumuuza kwa kumuona hana manufaa,
ila alipokwama kwa sababu alikuwa hajamaliza mkataba, akaambiwa arejee
kikosini.
Umefika wakati sasa tuweke unazi kando ili
kuzisaidia SImba na Yanga- zinatia kichefuchefu, tunazipenda basi tu!
0 comments:
Post a Comment