|
TIMU ya Simba iliwasili Dar es Salaam jana, ikitokea Sudan ilikotolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF), huku wachezaji wa timu hiyo wakiomba radhi mashabiki kwa kilichotokea na kusema kuwa mawazo yao sasa wanaelekeza kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti la Habari Leo, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, wachezaji hao walisema hawakutarajia kama wangetolewa katika mashindano hayo, lakini soka ndivyo ilivyo, kwa hiyo hawana budi kukubali matokeo na kuwaomba mashabiki nao waikubali hali hiyo.
“Tumefungwa, ndivyo soka ilivyo, tulipambana kadri ya uwezo wetu lakini imeshindikana, tunawaomba radhi mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla kwa matokeo hayo.
“Binafsi nimeumia sana, lakini hatuna jinsi, lazima tukubali na sasa tujipange kwa michuano ya Kombe la Kagame ili kuwapa raha mashabiki wetu,” alisema nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja.
Kwa upande wake mshambuliaji Haruna Moshi ‘Boban’, alisema asiyekubali kushindwa si mshindani na mara nyingi mikwaju ya penalti si jambo la kulipa nafasi kubwa kwani lolote linaweza kutokea.
“Tujipange kwa mashindano mengine. Inauma lakini lazima tukubali tumeshindwa,”
alisema Boban kauli ambayo pia ilizungumzwa na beki mahiri wa timu hiyo Amir Maftah.
Mshambuliaji Emmanuel Okwi kwa upande wake alisema hajui kwa nini walishindwa kuibuka na ushindi katika mechi hiyo, lakini aliwasifu wapinzani wao kwamba walijiandaa vizuri na walicheza kwa kuelewana.
Kocha Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic alisema vijana wake walijitahidi kadri ya uwezo wao, lakini wapinzani wao walikuwa vizuri na kwamba walitumia makosa waliyoyafanya kuweza kuibuka na ushindi.
Alisema kulikuwa na udhaifu katika safu ya ulinzi, ambao lazima ufanyiwe kazi na kwamba ana matumaini watajipanga vizuri kwa mashindano mengine.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema licha ya kutolewa, lakini wachezaji wake walipambana na si busara kuwaona kama watu walioshindwa kutetea nchi yao na kuongeza kuwa wanastahili pongezi.
Beki wa kati wa timu hiyo, Victor Costa alisema matokeo ndiyo yamekuwa hivyo na watajipanga kwa mashindano yajayo ya Kombe la Kagame.
Meneja wa timu hiyo Nico Nyagawa, alisema pamoja na mambo mengine lakini pia wachezaji wake walichanganyikiwa kisaikolojia kutokana na vitendo walivyokuwa wkaifanyiwa na wenyeji wao tangu walivyofika Sudan kwa kushindwa kupewa huduma zinazostahili.
Mashabiki kadhaa wa Simba walijitokeza uwanjani jana kuilaki timu hiyo, huku wakipiga ngoma na kuwaimbia nyimbo za kuwasifu wachezaji.
Simba Jumapili ilipigwa kumbo katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Al Ahly Shendi ya Sudan kwa penalti 9-8 baada ya Simba kufungwa mabao 3-0 katika dakika 90 za kawaida.
Kutokana na hali hiyo timu hizo zikalazimika kupigiana penalti kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, ambapo Simba ilishinda mabao 3-0, hivyo matokeo kuwa sare. Penalti za Simba zilipotezwa na Patrick Mafisango na Juma Kaseja.
Simba ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliokuwa wamebakia katika michuano inayoandaliwa na CAF kwa ngazi ya klabu.
Wawakilishi wengine wa Tanzania ambao tayari wameshatolewa ni Yanga iliyotolewa na Zamalek ya Misri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mafunzo iliyokuwa ikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika na kutupwa nje na Maqulmano ya Msumbiji.
Nayo Jamhuri ya Pemba ilitolewa michuano ya Kombe la Shirikisho na Hwangwe FC ya
Zimbabwe.
0 comments:
Post a Comment