SIMBA na Yanga zipo kwa zaidi ya miongo saba
sasa, zikiwa ni klabu ambazo zilianzishwa wakati ambao wananchi wakiamini kwa
kiasi kikubwa mambo ya kijadi, imani za kishirikina.
Tangu enzi hizo, Simba na Yanga hazishuki
dimbani bila kufanya mambo ya kijadi, yaani kuloga. Mwanzoni wachezaji wa Simba
na Yanga walikuwa wanapelekwa makaburini usiku wa manane, wanaogeshwa dawa
maarufu kama Kombe, wanasomewa dua kali za kinga kama albadir.
Waganga walikuwa wanakwenda uwanjani kuweka
dawa, wanatangulizwa kwenye njia ambazo wachezaji watapita kuelekea uwanjani.
Wakati mwingine waganga wa klabu wakihisi kuzidiwa ujanja na waganga wa klabu
pinzani, walikuwa wakiamuru klabu ziingie uwanjani kwa kuruka ukuta.
Hadi leo, Simba na Yanga zimeendelea kuuenzi
utamaduni huu, timu haishuki dimbani hivi hivi. Lazima yafanywe mambo kwanza na
kwa sababu wanaamini mambo haya, wamekuwa wakiwalipa fedha nyingi waganga.
Tatizo moja tu, timu ikifungwa, mganga hafuatwi,
bali lawama huwaangukia wachezaji na makocha. Wachezaji huambiwa wamehujumu
mechi au kocha huambiwa uwezo wake mdogo.
Kwa nini mganga haambiwi amehujumu au uwezo
wake mdogo?
Miongoni mwa matukio ya kihistoria katika
imani hizo kwenye mechi za watani wa jadi, ni lile la Agosti 10, mwaka 1974
kwenye Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, wakati Saad Ali alipogongana na kipa
wa Yanga, Elias Michael na kukimbizwa hospitali ya Bugando mjini Mwanza, ambako
alipata fahamu siku ya pili yake na kuuliza matokeo yalikuwaje katika mchezo
ambao Yanga ilishinda 2-1.
Wakati Elias Michael aliyekuwa akiitwa Nyoka
Mweusi anagongana na Saad, nyuma yao alikuwapo Gibson Sembuli, mtambo wa mabao
wa Jangwani enzi hizo. Michael (sasa marehemu) naye hakuweza kuendelea na
mchezo, kwani aliumia mkono na kutoka nje, nafasi yake ikichukuliwa na Muhiddin
Fadhil, wakati huo timu zilikuwa hazijafungana.
Nafasi ya Saad ilichukuliwa na Adam Sabu,
ambaye baada ya kuingia tu aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 16. Yanga
ilisawazisha bao hilo dakika ya 87 kupitia kwa marehemu Gibson Sembuli, na hadi dakika 90 zinakamilika matokeo
yalikuwa 1-1.
Huo ulikuwa mchezo wa fainali wa kumtafuta
bingwa wa nchi, hivyo ni sawa na zege halilali, lazima mshindi apatikane, hivyo
ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza na katika dakika ya saba tu, Sunday
Manara aliyekuwa akiitwa Computer, aliifungia Yanga bao la ushindi.
Jambo la kustaajabisha, eneo ambalo alianguka
Saad, paliota kichuguu, ambacho uongozi wa Uwanja wa Nyamagana pamoja na
kuking'oa mara kwa mara kimekuwa kikiota tena na tena.
Tukio lingine la ushirikina, ni baada ya Yanga
kufungwa 6-0 na Simba Julai 19, mwaka 1977, wachezaji wa Yanga walidai kwamba
waliogeshwa maji ya maiti badala ya Kombe. Yaani mtu aliyekwenda kuchukua dawa kwa
mganga, aliigeuka Yanga na akaisaliti kwa kuwapa maji ya maiti.
Lakini mwaka 1981, wachezaji wa Yanga
walimgomea Mwenyekiti wao wakati huo, Juma Shamte kuamka kwenda kwenye kambi
nyingine Bagamoyo kutoka Kibaha walipokuwa wamejificha. Shamte aliwafuata
wachezaji na kuwaambia kambi hiyo 'imeonwa' hivyo kwa kuhofia kufungwa, wahamie
Bagamoyo.
Wakati huo Yanga ilikuwa haijaifunga Simba kwa
miaka sita tangu ilipoifunga mara ya mwisho mwaka 1875, mabao 2-0 visiwani
Zanzibar kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Lakini wachezaji wenye msimamo, akina Charles
Kilinda, Charles Alberto na marehemu Juma Mkambi, waliwaongoza wenzao kugoma kuhama
kambi usikuwa wa manane. Walimuambia Shamte, aende na wakifungwa potelea mbali,
lakini muda ule, walihitaji kupumzika tu.
Lakini ilipowadia siku ya mchezo, Septemba 5
mwaka 1981, Juma Shamte alisuuzika na roho yake kwa bao pekee la Juma Mkambi
'Jenerali' aliyemtungua Omar Mahadhi kwa kichwa akiunganisha krosi ya Salehe
Hijja dakika ya 42.
Hamisi Kinye siku hiyo alidaka kwa uhodari
mkubwa na kukwamisha juhudi za wapachika mabao wa Simba, akina Nico Njohole,
Thuwein Ally, Adam Sabu na George 'Best' Kulagwa.
Mabeki wa Simba walikuwa Yussuf Ismail Bana,
Mohamed Kajole (sasa marehemu), Daud Salum "Bruce Lee', Mohamed Bakari
'Tall' na Athumani Juma Kalomba (sasa marehemu). Lakini pamoja na wakali hao, Yanga
ikiongozwa na kocha Ray Gama ilivunja mwiko wa kutoifunga Simba kwa miaka hiyo
sita.
Imani za kishirikina zimeendelea kuenziwa hadi
leo, ingawa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha
viongozi wa klabu hizo kuachana nazo.
Katika mechi ambayo Yanga ilishinda 1-0,
Uwanja mpya wa Taifa, Oktoba 26 mwaka 2008, mashabiki waliona kitendo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali kuingia na mchezaji wake, Mussa Hassan Mgosi
na kwenda kuweka vitu vyao kwenye lango ambalo Yanga walianzia, lakini
hawakuona nini kilitokea kambi ya Yanga, New Africa Hotel, mchezaji Boniphace
Ambani aligoma kufanyiwa ndumba na waganga waliopelekwa kwa ajili ya kuilogea
timu.
Alisema yeye mganga wake ni Yesu Kristo,
hawezi kufanya hivyo na kweli Ambani kwa nguvu za amuaminiye, alitoa pasi ya
bao pekee kwenye mchezo huo, ambao hakuumaliza kutokana na kuchanika nyama za paja.
Ukisikia Simba inakwenda Zanzibar kuweka
kambi, siyo kwamba inafuata mazingira mazuri, la hasha, bali wanakwenda kwa
wataalamu wanaowaamini katika mipango ya ndumba za ushindi. Kadhalika Yanga
ukisikia wanakwenda Bagamoyo, si kwamba wanafuata mazingira mazuri, bali
wanakwenda kwa wataalamu wao wa 'juju'. Ni kwamba, huwezi kuzitenganisha hizi
klabu na ndumba, ni sehemu ya jadi yao.
0 comments:
Post a Comment