MABINGWA wa Ligi Kuu ya Bara mwaka 1988, Coastal Union ya
Tanga wanatarajiwa kufanya ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Uturuki,
Julai mwaka huu, huku habari zaidi zikisema wamemsajili kiungo wa kimataifa wa
Tanzania, Shaaban Mussa Nditi (pichani kushoto) aliyewahi kuwika Simba SC.
Msemaji wa Coastal Union, maarufu kama Wagosi wa Kaya,
Edward ‘Edo’ Kumwembe ameiambia BIN ZUBEIRY jioni ya leo kwamba wapo
kwenye mchakato wa ziara hiyo na utakapokamilika watatoa ratiba kamili.
Ingawa Edo, ambaye pia ni Mwandishi wa Habari na Mchambuzi
wa soka katika gazeti la Mwanaspoti, hakusema ziara hiyo imefadhiliwa na nani,
lakini habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani
ya klabu hiyo yenye maskani yake Barabara ya 13, Tanga zimesema ni mchezaji wao
wa zamani, Kassa Mussa.
Kiungo huyo hodari wa zamani wa Mkoa wa Tanga, aliyekuwemo
kwenye kikosi kilichochukua ubingwa wa Bara 1988, kwa sasa anaishi Uturuki
ambako inaelezwa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kimaisha.
Tayari Coastal imekwishaanza mchakato wa kuunda kikosi ‘baab
kubwa’ cha msimu ujao na habari zaidi zinasema wako mbioni kumsajili kiungo wa
zamani wa Simba, Mkenya Jerry Santo wakati wachezaji wengine ambao viwango vyao
vimeshuka kama Ben Mwalala, Mkenya pia na Ramadhan Wasso, Mrundi, wamekwishaonyeshwa
mlango wa kutokea.
Coastal inatarajiwa kutengeneza ‘bonge la mshituko’ kwa
wapenzi wa soka nchini katika usajili wao, kutokana na harakati zao za chini
chini za usajili wanazofanya, ikiwemo kumsajili kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaaban
Mussa Nditi.
Wengine ambao tayari wamenasa kwenye rada za Coastal ni
mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Nsa Job Mahenya ambaye msimu huu
alichezea Villa Squad iliyoshuka daraja.
0 comments:
Post a Comment