Mshambuliaji wa Ujerumani Lukas Podolski atajiunga na Arsenal akitokea klabu ya Cologne kuanzia msimu ujao kwa ada ambayo haijafahamika.
Podolski mwenye umri wa miaka 26 alianza usakataji wa kandanda katika klabu ya Cologne mwaka 2002 na aliwahi kuichezea Bayern Munich miaka minne baadaye kabla ya kurejea katika klabu yake hiyo ya zamani mwaka 2009.
Mshambuliaji huyo ambaye ameshacheza mechi za kimataifa 95, alisema: "Nina furaha sana kujiunga na Arsenal na Ligi Kuu ya England. Ni moja ya vilabu vikubwa barani Ulaya ikiwa na historia kubwa.''
"Kuna wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu katika Arsenal na mtindo wao wa uchezaji unavutia sana."
Aliongeza: "Nimefanya uamuzi huu sio dhidi ya FC Cologne lakini ni kwa sababu ni nafasi kubwa kwangu.
"Haukuwa uamuzi rahisi kwangu, kwa Cologne, mashabiki wetu na jiji lote kwa ujumla wamekuwa ni muhimu sana kwangu."
Mshambuliaji huyo mzaliwa wa Poland ambaye amebakisha mwaka mmoja kabla ya kumaliza mkataba wake, ameshafunga mabao 18 ya ligi hadi sasa msimu huu kwa klabu yake ya Cologne ambayo inatapia roho kutoteremka daraja.
Aliongeza: "Mara zote imekuwa kama kuiweka FC Cologne kwenye moyo wangu. Hatuna budi kujifunga kibwebwe ili tusiteremke daraja katika Bundesliga."
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema: "Ni mchezaji wa kiwango cha juu, mmaliziaji mzuri na amethibitisha hayo katika klabu yake na timu ya taifa. Ni mchezaji mwenye nguvu na atatusaidia sana katika safu ya ushambuliaji."
Arsenal inajiimarisha katika safu ya ushambuliaji. Ingawa Robin van Persie ameshapachika mabao 28 ya ligi msimu huu na kuwa mpachika mabao wao hodari, anayefuatia kwa kufunga mabao katika Arsenal ni Theo Walcott ambaye hadi sasa ameshapachika mabao manane tu.
Podolski, ambaye ataungana na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa ya Ujerumani Per Mertesacker katika klabu ya Arsenal, aliichezea Ujerumani katika Kombe la Dunia mwaka 2006 na 2010 na bado atakuwemo katika kikosi kitakachoshiriki mashindano ya Euro 2012.
Ameshafunga mabao 43 kwa michezo 95.
Wenger alisema: "Hii rekodi bora zaidi na inaonesha ubora wake kama mchezaji."
Mwenyekiti mtendaji wa Cologne Claus Horstmann alisema: "Cologne ilikuwa imejiandaa kuongeza mkataba wa Lukas Podolski kwa kigezo cha muelekeo wa timu yake kufanya vizuri. Kutangazwa huku mapema kwa uhamisho wa Podolski kunatoa nafasi ya Arsenal kujiweka sawa mapema na kujiondolea mashaka kwa msimu ujao
0 comments:
Post a Comment