Shadrack Nsajigwa |
ALIYEKUWA nahodha wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Shadrack Nsajigwa, amesema roho yake ipo kwatu kwa kutoitwa katika kikosi hicho, lakini akiomba wadau waheshimu mchango wake alipokuwepo.
Juzi Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi Kanda ya Afrika kati ya Taifa Stars na Ivory Coast mapema mwezi ujao, ambapo Nsajigwa ni miongoni mwa wachezaji ambao hawakuitwa.
Majina mengine maarufu yaliyoachwa ni beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ , Nizar Khalfan, Danny Mrwanda, Henry Joseph na Shaaban Kado.
Akizungumza na Habari Leo, Dar es Salaam jana, Nsajigwa alisema kutoitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars ni jambo la kawaida, kwani kila kukicha vipaji vinaongezeka, lakini anahitaji kuheshimiwa kwa mchango wake alioutoa kwa Taifa.
“Nimetumikia Taifa langu kiasi cha kutosha, hivyo Watanzania wanatakiwa kuniheshimu, kwa mchango wangu, “ alisema Nsajigwa na kuongeza kuwa hilo halimnyimi usingizi maana hawezi kuita wachezaji wote Tanzania.
Aliwaomba wachezaji walioitwa na Poulsen kujituma na kuchukua mazuri waliyoyafanya wao wakiwa kwenye kikosi hicho na kuacha mabaya, ambayo hayawezi kusaidia Stars.
Pia aliwataka wachezaji wakongwe waliopo kwenye kikosi hicho, kuwapa ushirikiano chipukizi walioitwa kwenye kikosi hicho kwa mara yao ya kwanza.
Hata hivyo Nsajigwa alishangazwa na klabu yake ya Yanga kuwa na mchezaji mmoja kwenye timu hiyo ambaye ni Nurdin Bakari.
“Eti Yanga ina mchezaji mmoja kwenye timu ya taifa? Kweli tulichoka,” alisema Nsajigwa.
Wachezaji waliotangazwa juzi na Poulsen kuunda kikosi hicho ambacho kitaingia kambini leo na timu zao katika mabano ni makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar).
Mabeki ni Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).
Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Jonas
Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba- U20), Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu- U20).
Washambuliaji ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan Singano (Simba-U20), Simon Msuva (Moro United- U20), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Haruna Moshi (Simba) na John Bocco (Azam).
0 comments:
Post a Comment