TANGU aondoke Mangara Tabru (sasa merehemu) katika klabu ya
Yanga 1976, hapana shaka Imani Mahugila Madega ndiye Mwenyekiti pekee
aliyefanikiwa kukaa madarakani hadi kumaliza muda wake, akiitisha uchaguzi na
kumkabidhi madaraka kiongozi mwingine, Wakili mwenzake, Lloyd Baharagu Nchunga (pichani kushoto),
Mei 18, 2010.
Kuna dalili za kutosha kabisa, Nchunga ameshindwa kuvunja
rekodi ya Madega na kwa hali ilivyo wakati wowote anaweza kutangaza mwenyewe
kujiuzulu, kwa nia nzuri tu ya kuinusuru Yanga.
Wanachama wanaodai idadi yao ilifika 700 wa Yanga walikutana
Jumapili makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es
Salaam na kufikia uamuzi wa kumng’oa madarakani Mwenyekiti, Wakili Lloyd
Bahargu Nchunga.
Mapinduzi haya yaliongozwa na Mzee Ibrahim Akilimali, ambaye
kihistoria nilishasema siku nyingi ni mzee kinara wa migogoro na mvuruga amani
klabuni, aliyetukuka.
Huyu alishiriki mapinduzi ya kumng’oa marehemu Rashid
Ngozoma Matunda na akashiriki kumnyima amani Madega katika utawala wake, ingawa
alichemsha. Mzee huyu alijaribu kugombea Uenyekiti wa Yanga dhidi ya Dk Jabir Idrisa
Katundu mwaka 1993, lakini akajitoa mapema kwa sababu alikuwa hakubaliki.
Kweli, kwa sasa Nchunga ameshindwa kumudu kuongoza Yanga kwa
ufanisi, na hiyo ni kwa sababu ya kukosa ushirikiano kutoka kwa Wajumbe wenzake
wa Kamati ya Utendaji na wadau wengine wa klabu, wakiwemo hao wanaojiita wazee
na wafadhili.
Lakini ukirejea uchaguzi uliomuweka madarakani Nchunga
Jumapili ya Mei 18, mwaka 2010, alishinda Uenyekiti baada ya kupata kura 1,437, akiwaangusha wapinzani wake wanne, Francis
Kifukwe aliyepata kura 370, Mbaraka Igangula aliyepata kura 305, Abeid Falcon
aliyepata kura 301 na Edgar Chibura aliyeambulia kura 65 katika kura 2,220
zilizopigwa, wakati kura 23 kati ya hizo ziliharibika.
Kura 370 za Kifukwe na 305 za Igangula kwa pamoja
wakichanganya, bado hawawezi kufikia kura za Nchunga- ina maana alishinda kwa
kishindo. Inakuwa rahisi kuhisi watu hawa 700 waliokutana Jumapili ni wale wale
700 waliomnyima kura Nchunga PTA Mei 18, 2010.
Lakini kwa sababu hiki ni kipindi kigumu ambacho Yanga
inatakiwa kujipanga upya baada ya msimu mbovu uliopita, tena uliotokana na
Nchunga kuhujumiwa na wapinzani wake, hakuna njia nzuri zaidi ya Wakili huyo
kuchukua maamuzi magumu kwa maslahi ya klabu. Wala Nchunga hataonekana mjinga-
bali ataonekana jasiri na mwenye mapenzi ya kweli kwa klabu.
Alifanya kosa kubwa kuteua waliokuwa wapinzani wake kwenye
uchaguzi katika Kamati zake- hao ndio waliomuumiza. Alifanya kosa kushindwa
kuwa bega kwa bega na waliomsimika madarakani wamsaidie. Sasa anavuna matunda
ya makosa yake. Aliwaamini sana watu wa Yanga, hakuwajua vizuri. Wengi wapo kwa
ajili ya maslahi yao binafsi na ni wanafiki sana.
Inapofikia hapa, namkumbuka marehemu Syllersaid Salmin
Kahema Mziray; aliwahi kusema Simba na Yanga zikifa na watu wengi watakufa kwa
sababu maisha yao yote wanazitegemea hizo klabu- kwa Jangwani ndio hao Al
Shabaab. Riziki yao inatokana na migogoro.
Kama nitapata fursa ya kukutana na Nchunga, nitamuambia
ajiuzulu Yanga. Atakuwa amechukua uamuzi wa kijasiri na busara na ataheshimika
daima milele. Sasa waingie hao Al Shabaab na walipe kisasi cha 5-0 za Simba. Tena
wapewe miaka minne.
Siku zote nasema migogoro hii ya Simba na Yanga, serikali
inaikumbatia, kwa sababu ukizama ndani ya historia ya timu hizi ni kama mali za
umma tu hazina mwenyewe. Hivyo kila mwenye kadi anajifanya ana sauti na
maamuzi, bila kuzingatia ana mchango gani.
Kwa misingi ya klabu hizi, ni vigumu kufa, ila migogoro
haitaisha, hasa Yanga- kwa sababu kuna kigogo pale ana azma yake na inaweza
kuwa nzuri, lakini njia anazotumia kutaka kuitimiza ndio shubiri kwa klabu hiyo.
Ni yule Yule aliyemnyima raha Madega katika utawala wake-
sasa amepiga hatua kubwa. Kujaribu kupambana na migogoro ya Yanga kwa kupambana
na akina Akilimali na Bakili Makele ni kazi bure- lazima litafutwe shina la
matatizo klabuni- hawa ni matawi tu.
Sitaki kuamini eti pale alipo Leonard Thadeo, Mkurugenzi wa
Michezo katika Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo au Leodegar Tenga,
Mwenyekiti wa TFF hawajui kiini cha mgogoro huu wa Yanga- kama hawajui wakiniita
nitawaleleza na kuwapa vielelezo au ushahidi, labda wakijua wataisaidia klabu
hiyo.
Kuyumba kwa Yanga au Simba ni kuyumba kwa maendeleo ya soka
ya nchi hii kwa ujumla pia- lakini pia Kilimanjaro Beer waliowekeza mamilioni
yao pale Jangwani wanaupokeaje mgogoro huu?
Tazama kwa sasa kikosi cha timu ya taifa kuna mchezaji mmoja
tu wa Yanga, hivi kweli kama klabu hiyo ingekuwa vizuri, leo sura ya Taifa Stars
ingekuwaje? Ni kiasi gani kwa sasa mchango wa Yanga unakosekana timu ya taifa? Huu
ni mfano mdogo tu.
Wanasema ni kidogo- japo mimi naona hakitoshelezi kulingana
na bajeti yao wanachokipata kutoka TBL, lakini kisingekuwepo hali ingekuwaje Yanga?
Kama hakuna msaada wa serikali, au TFF ina maana Nchunga
atasababisha matatizo makubwa zaidi Yanga- tu kwa kutokubali kujiuzulu katika
vita ambayo tayari amekwishashindwa.
Madega alishinda vita hiyo kwa sababu kwanza alikuwa mzoefu
wa siasa za Yanga na soka ya Tanzania kwa ujumla- akianzia kwenye ngazi za chini
za uongozi mwaka 2000. Lakini Nchunga alikuwa mchanga katika siasa za soka za
nchi na klabu hiyo kwa ujumla, nami nilijua hatafika mbali, hasa baada ya Davis
Mosha kujiuzulu.
Alikubali kuhitilafiana na Mosha na akaridhia ajiuzulu,
lakini hakuona athari zinazoweza kutokea mbele yake. Kama angekuwa ana Makamu
wake Mwenyekiti leo na wapo kitu kimoja, angalau leo kidogo angekuwa ana nguvu.
Kile kimkutano cha nyuma ya jukwaa la Mkutano wa Uchaguzi na
wagombea wenzake wa nafasi ya Mwenyekiti, leo ndio kinammaliza Nchunga. Alikubali
ushauri ambao hakuufanyia kazi kwanza. Ndio,
wahenga walisema mchawi mpe mwanao, lakini si katika dunia ya leo, anamuua
kweli na anakuambia macho makavu; “Kazi ya Mungu”. Utafanya nini?
Madega alisimama kidete kupigana, alisimamisha wachezaji
waliotumiwa na adui zake kuisaliti Yanga- alipambana na wazee, wafadhili na
wanachama bila woga wala kuwatazama usoni. Ndio maana aliwaaga wana Yanga, akipigiwa
makofi Mei 18, 2010 pale PTA tena akisema; “Mtanikumbuka”. Kweli, mimi ni mmoja
wa wanaomkumbuka leo.
Madega hakuwa mnafiki, ukimkosea alikuwa anakuchana, na kesho
mkikutana anakuwa wa kwanza kukusalimu. Ukikasirika shauri yako, ila yeye hakuwa
wa kulea maradhi. Lakini naye aliwindwa kwa mikakati mizito ang’olewe, wakashindwa.
Unakumbuka alivyompa vidonge Manji? Nitakukumbusha;
“Habari hizo alizosema Manji juu ya uongozi wangu ni uongo
mtupu, ukweli ni kwamba ujio wa Manji ndani ya Yanga unaonekana kama ni
ukombozi wa kifedha, lakini ukweli ni kuwa amekuja kwa lengo moja tu, la
kuiangamiza klabu ya Yanga kabisa na hatimaye kuunda kampuni ambayo kinadharia yeye
ndio atakayekuwa mmiliki mkuu.” Kauli hii aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007 baada
ya kutokea kutoelewana kati yake na mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji.
Bado, kuna nyingine pia alimpa Manji, ngoja niwakumbushe;
“Kwa mawazo yangu, fedha hizo zilitolewa (na Manji) kwa
lengo la kutugombanisha. Wachezaji wetu walicheza chini ya kiwango kwa kutambua
kuwa wanavuja jasho, lakini fedha wanapewa wengine wasiowajibika uwanjani,”.
Kauli hii aliitoa Oktoba 26, mwaka 2007 akijibu kauli ya
Yussuf Mzimba, aliyeutaka uongozi wake kueleza jinsi ulivyotumia shilingi
milioni 40 zilizotolewa na mfadhili wao, Yussuf Manji kwa ajili ya kuhakikisha
timu hiyo inawafunga watani wao wa jadi, Simba Oktoba 24 mwaka huo mjini
Morogoro. Manji pia aliwapa Sh. Milioni 10, wazee wa klabu hiyo chini ya
Mzimba, lakini Yanga ililala 1-0, kwa bao pekee la Ulimboka Mwakingwe.
Hata Yanga waliokuwa wanaamini Yanga bila Manji haiwezekani,
aliwapa kitu pia;
“Lakini pia ni vyema watu, hasa wanachama wa Yanga
wakafahamu kwamba, mtoto huzaliwa na kukua, huwezi kutegemea kusaidiwa kila
siku. Manji amefanya vitu vingi sana kwa klabu hii. Ametulea katika kipindi
kigumu, wakati Uwanja wa Taifa ulipokuwa umefungwa, tulichezea Morogoro ambako
fedha za kiingilio zilikuwa ni chache. Sasa tumehamia Dar es Salaam, timu
inafanya vizuri mashindano ya ndani na nje, wanachama wanahamasika kuja
kuishangilia na fedha zinapatikana. Tunaweza kusimama wenyewe,”.
Kauli hii aliitoa Februari 3, mwaka huu akizungumzia
mustakabali wa klabu hiyo
Hata TBL nao pia aliwapa kitu, unakikumbuka? Nitakukumbusha;
“TBL haina uwezo wa kuiingilia Yanga kwa kututaka tuajiri
Katibu Mkuu, makubaliano yetu ni kuajiri Mweka Hazina na tunatarajia kutangaza
nafasi ya kazi wakati wowote kuanzia sasa, atakayetimiza vigezo tutamuajiri.
Haya mambo si ya kukurupuka, nafasi kama ya Katibu Mkuu ni nyeti ambayo
mshahara wake hauwezi kuwa Sh200,000, hapa tutaongelea milioni kadhaa, sasa
bila kujipanga tutawezaje kumlipa?”
Kauli hii aliitoa Oktoba 3, mwaka 2008, kufuatia agizo la
wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kuwataka waajiri watendaji kama
ambavyo mkataba baina yao unaelekeza.
Hata hawa wazee nao aliwapasha; nitakukumbusha;
“Mwisho nasema kuwa sitokuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na
kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali
zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako
au fadhili timu nyingine. Wazee na wanachama wachache waroho wa Yanga kuweni
macho na msiwasaliti wazee wenzenu ambao walifanya juhudi kuifanya Yanga iwe na
jina kubwa, mkiendelea kufanya hivyo kwa hakika historia itawahukumu, uongozi
uko imara kutetea maslahi ya Yanga,”.
Kauli hii, Madega aliitoa Oktoba 11, mwaka 2007, kutokana na
wazee na wanachama wa klabu hiyo kumuunga mkono Manji katika mgogoro wake na
Madega.
Kwa staili hii Madega alikaa Yanga hadi mwisho wa muda wake
wa kuwa madarakani, lakini Nchunga ameonyesha hana ubavu huo- njia nzuri kwake
ni kuachia ngazi, wengi wanajua ngoma imemkalia vibaya hii na zaidi akiendelea
kuleta ubishi kwa kuwa analindwa na Katiba, atazidi kuiumiza timu.
Sasa Yanga wanataka kusikia anasajiliwa mchezaji gani hodari
wa kuunda kikosi imara cha kurejesha heshima msimu ujao, Nchunga bila msaada wa
wafadhili ambao hivi sasa ndio wako dhidi yake, hataweza. Namshauri, aachie
madaraka kuinusuru Yanga.
0 comments:
Post a Comment