// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MWAMEJA NA KASEJA KATI YAO YUPO KIPA BORA WA KIHISTORIA SIMBA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MWAMEJA NA KASEJA KATI YAO YUPO KIPA BORA WA KIHISTORIA SIMBA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Tuesday, May 01, 2012

    MWAMEJA NA KASEJA KATI YAO YUPO KIPA BORA WA KIHISTORIA SIMBA

    Juma Kaseja
    JUMA Kaseja alijiunga na Simba SC mwaka 2003, akitokea Moro United na aliidakia klabu hiyo hadi msimu wa 2009, aliposaini Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja.
    Baada ya makataba wake kwisha, hakuongezewa mwingine na mara moja Simba ikamsajili tena.
    Kaseja kwa mara ya kwanza Simba alisajiliwa msimu ambao Mohamed Mwameja alikuwa amestaafu, tena kwa heshima kubwa.
    Mwameja alijiunga na Simba SC mwaka 1992, akitokea Coastal Union ya Tanga na alikutana na makipa hodari kama Iddi Pazi ‘Father’ na Mackenzie Ramadhan katika msimu wake wa kwanza.
    Mwaka huo huo, 1992, Mwameja aliipa Simba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame katika fainali zilizofanyika visiwani Zanzibar, wakimfunga mtani wa jadi, Yanga kwa penalti.
    Alikaa Simba hadi 1996 alipokwenda Reading ya England na katika kipindi chote hicho pamoja na Pazi na Mackenzie kuondoka, lakini aliletewa makipa wengine wakali kama Steven Nemes, Joseph Katuba (marehemu), Often Martin, Issa Manofu na Bahatisha Ndulute, lakini hakuna kati yao aliyempiku mtoto huyo wa Kitanga, iwe Simba au timu ya taifa. Alibaki kuwa Tanzania One.
    Mwishoni mwa mwaka 1998, Mwameja alirejea kutoka Reading na kujiunga na benchi la ufundi sambamba na aliyekuwa kocha, Mohamed Kajole ‘Machela’ sasa marehemu.
    Aliikuta Simba iko vibaya na imepoteza hadhi yake, kiasi cha kukosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika kwa miaka miwili mfululizo, 1998 na 1999.
    Msimu wa 1999, Mwameja alisaini Simba, wakati timu ikisajili chipukizi kibao kama Prosper Omella, Miraj Juma, Thabit Mjengwa, Athumani Machuppa, Athumani Macheppe, Wilfred Kidau, Renatus Njohole, Henry Freeman, Edward Kayoza, Mussa Msangi (marehemu) na wakongwe wachache waliokuwa Sigara kama Athumani Jumapili Chama na Mrisho Moshi ‘Beckham’.
    Mwishoni mwa msimu, Mwameja aliandika barua ya kujiuzulu ambayo kwa utundu wangu, niliipata nakala yake na hadi leo ninayo kwenye maktaba yangu.
    Mtibwa Sugar ilikuwa bingwa mwishoni mwa msimu na Yanga ikawa ya pili- Simba ikakosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika na mwaka 2000 pia.
    Mwaka 2000, Simba ikamchukua aliyekuwa kocha wa Yanga, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ (sasa marehemu) wakati huo akiwa Majimaji ya Songea baada ya kuifanya timu hiyo kuwa tishio na kutwaa ubingwa wa Muungano 1998.
    Tauzany ambaye sasa ni  marehemu, alisajili wachezaji kibao wa Majimaji kama Doyi Moke na kuchukua nyota wengine kama Suleiman Matola kutoka Kagera Shooting (sasa Kagera Sugar) na hadi mwisho wa msimu, hawakufua dafu katika ligi ya Bara, Mtibwa ilikuwa bingwa, Yanga ya pili na Kajumulo WS ya tatu, hivyo kukosa hata tiketi ya kushiriki Ligi ya Muungano.
    Lakini Simba ilikuwa inashiriki Kombe la FAT, ambalo bingwa wake alikuwa anacheza Kombe la Nyerere lililokuwa likishirikisha na timu za Zanzibar kutafuta timu ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Washindi.
    Marehemu Super Coach, Syllersaid Kahema Mziray akapewa timu kuiongoza kwenye Kombe la FAT na ndipo akamrejesha Mwameja kikosini.
    Meja alidaka hadi kuiwezesha Simba kubeba Kombe la FAT, wakiifunga Yanga kwa penalti kwenye fainali.
    Mwaka 2001 jina la Simba SC likarejea kwenye kumbukumbu za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ilipopata tiketi ya kucheza Kombe la Washindi.
    Mwaka huo huo 2001, Mwameja akaipa Simba SC ubingwa wa Bara na mwaka 2002 japokuwa walipokonywa na Yanga ubingwa wa Bara, lakini Meja aliiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, katika fainali zilizofanyika visiwani Zanzibar, wakiifunga Prince Louis ya Burundi 1-0.
    Mwameja Mohamed
    Huo ndio ulikuwa msimu wa mwisho wa Mwameja Simba, akastaafu na mwaka 2003, akapatikana shujaa mpya wa kwenye milingoti Msimbazi, mtoto wa Kigoma, aliyekulia Morogoro, Kaseja.
    Mwaka 1992 hadi 2002 ni miaka 10, lakini Mwameja aliidakia Simba misimu nane tu kutokana na msimu ambao alikwenda Reading na msimu ambao alitemwa kabla ya kurejeshwa.
    Kaseja pia, akiwa Simba katika msimu wake wa kwanza tu aliifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Kagame nchini Uganda, ambako walifungwa 1-0 kwa tabu na wenyeji SC Villa.
    Msimu huo huo wa 2003, Kaseja aliiongoza Simba kuitoa Zamalek ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, miaka 10 tangu Mwameja aiongoze Simba kucheza fainali ya Kombe la CAF na kufungwa na Stella Abidjan.
    Kuanzia mwaka 2004, baada ya zama za Manyika Peter, Kaseja akawa Tanzania One na hadi leo- nani mwingine zaidi yake?
    Kaseja amepitia vipindi vigumu pia, kuna wakati mwaka 2007 alisimamishwa Simba kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, mambo ambayo yanakatisha tamaa na wakati mwingine yanaweza kukuondoa kwenye soka, lakini alisimama imara na alipomaliza kutumikia adhabu yake, ameendelea kuwa Simba One.
    Timu ya taifa, alipokuja Mbrazil Marcio Maximo alimtema kwa sababu hizo hizo za nidhamu na hakumrejesha hadi alipoondoka na kuajiriwa kocha mpya Mdenmark, Jan Bolrge Poulsen akamrejesha kikosini.
    Alirejea kwa kishindo mwaka 2010, akiiwezesha timu ya Bara kutwaa Kombe la Challenge ambalo Mwameja alilitwaa mara moja tu, 1994 nchini Kenya.
    Mwameja alitwaa mataji 16 akiwa na Simba, ambayo ni ubingwa wa Ligi Kuu (matatu) 1994, 1995 na 2001, Kombe la Nyerere (mawili) 1995 na 2000, Ligi ya Muungano (matano) 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, Kombe la Tusker (mawili) 2001 na 2002, Kombe la Kagame (manne) 1992, 1995, 1996 na 2002 na kucheza fainali ya CAF 1993.
    Kaseja hadi sasa amekwishatwaa mataji sita akiwa na Simba, ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2003, 2004,  2007 na 2010, jumlisha wa 2009 aliotwaa na Yanga, Kombe la Tusker 2003 na 2005 mawili pamoja la Kenya. Jumla Kaseja ana Medali nane za dhahabu kabatini kwake na anaelekea kutwaa Medali ya tisa msimu huu ya Ligi Kuu ya Bara na hatujui ataifikisha wapi Simba katika Kombe la Shirikisho.
    Kaseja bado ana misimu hata mitatu au zaidi ya kudaka kwa kiwango cha juu kama hataumia, au hatatatokea mkali zaidi yake Simba, ambaye imekuwa ikimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio.
    Tuhuma za kuihujumu Simba kwenye mechi za Yanga wote wawili zimewakumba- na Kaseja na Mwameja pamoja na kwamba klabu hiyo wamepitia makipa wengine hodari kama Omar Mahadhi, Athumani Mambosasa na Father Pazi kati yao unaweza kumpata kipa bora wa klabu daima.

    MAKALA HII NIMEANDIKA JIONI HII, NILIKUWA NIMEBOREKA, NIMEKOSA KAZI, NIKASHIKA KOMPYUTA ILI NIINGIE FACEBOOK, LAKINI GHAFLA LIKANIJIA WAZO KUHUSU WATU HAWA WAWILI... TOA MAONI YAKO, NANI AWE KIPA BORA WA KIHISTORIA SIMBA KATI YAO?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMEJA NA KASEJA KATI YAO YUPO KIPA BORA WA KIHISTORIA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top