HATIMAYE wiki hii, Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd
Baharagu Nchunga ametangaza mwenyewe kujiuzulu wadhifa wake, baada ya vita
kubwa aliyokuwa akipigwa na wapinzani wake.
Nchunga anastahili sifa, ameonyesha yeye ni Yanga damu. Si mroho
wa madaraka. Ni mtu aliyeweka maslahi ya Yanga mbele. Huyu ni mfano wa kuigwa. Lakini
baada ya Nchunga kujiuzulu, pamoja na kwamba mfanyabiashara Yussuf Manji
ameahidi kuihudumia timu kwa mwaka mmoja, bado ipo haja sasa ya mustakabali wa
klabu hiyo kutazamwa kwa kina.
Nasema mustakabali wa klabu kutazamwa kwa kina, kwa sababu
imeonekana ni vigumu mno Katiba kumlinda kiongozi aliye madarakani, iwapo kundi
fulani litaamua kwa dhati kuingia msituni kumng’oa.
Mfano ni hii vita aliyopigwa Nchunga- ilikuwa kali na ikafikia
lazima aondoke kwa maslahi ya klabu. Alitengenezewa zengwe zito. Alipigwa kila
upande- hakuwa na namna yoyote zaidi ya kujinasua.
Walioongoza mapambano dhidi ya Nchunga, akina Ibrahim Akilimali,
Bakili Makele na wengine- ni wale wale ambao kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa
mstari wa mbele katika vurugu na migogoro kwenye klabu hiyo.
Kumbukumbu zipo, Bakili na Akilimali walishiriki kikamilifu
kumng’oa Mzee Rashid Ngozoma Matunda mwaka 1999 na hawa hawa walimtia kashikashi
nzito Wakili Imani Omar Madega, ingawa huyo walimshindwa.
Sioni kwa sababu gani hawa watakoma kwa mtu mwingine yeyote
atakayekuja baada ya Nchunga, kwa sababu wamekwishazoea. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kutoa mfano mmoja enzi za uhai wake kuhusu
ubaguzi.
Alisema dhambi ya ubaguzi ni sawa na dhambi ya kula nyama ya
mtu, ukishakula nyuma ya mtu, hutaacha utaendelea kula.
Naweza kuuleta mfano huu katika hii desturi ya mapinduzi kwenye
klabu ya Yanga- naona kuna dalili za kutosha itaendelea tu hata ije katiba ya
aina gani.
Tena watu hawa wamepiga hatua kubwa, kiasi cha kuona bora
Yanga ife, lakini kiongozi fulani ang’oke madarakani. Inasikitisha.
Mapendekezo ya Manji kuhusu mabadiliko ya Katiba hata yafanyiwe
kazi- lakini kuna uwezekano likaibuka kundi la kumpinga na kupambana naye
kikamilifu. Hiyo ndio tabia ya Yanga.
Kwa ‘uhuni’ aliofanyiwa Nchunga, hakuna hakika kama atatokea
mtu mwingine mwenye hekima na kujiheshimu kufikiria kuongoza Yanga- inatia
woga. Lakini kwa nini ifikie huko, kweli tutegemee kuiona Yanga bora na ya kisasa
bila mtu mwenye hekima na upeo mkubwa?
Kwa Nchunga, dalili niliziona tangu wakati wa uchaguzi uliomuweka
madarakani mwaka 2010 kwamba hatakaa kwa raha Yanga na kwa wasomaji wa makala
zangu tangu naandikia magazeti, watakuwa wanakumbuka nilisema sina uhakika hata
kama atamaliza muda wake madarakani.
Yametimia. Njia nzuri ya kuwateka wananchi ni kuwaridhisha
tu na hiyo ndio demokrasia. Nchunga alitakiwa ashinde uchaguzi wa Yanga, bila
kuwapo mizengwe na wale ambao hawakwenda ukumbini kwa ajili ya kumpigia kura,
wakubali kwamba huyo ndiye chaguo la wana Yanga.
Lakini kwa picha iliyojitokeza siku ile, hata yule ambaye
alikwenda maalum kwa ajili ya kumpigia kura Nchunga, aliondoka na picha kwamba
kiongozi huyo amepita kimizengwe. Hiyo peke yake ni mbaya sana.
Sasa kosa hilo linataka kujirudia- staili iliyotumika kumng’oa
Nchunga si nzuri na watu wengi hawajaridhika nayo, maana yake hakuna demokrasia
pale. Hata huyo anayekuja baada yake, hakika hawezi kukaa kwa raha Yanga.
Zaidi, aliyofanyiwa Nchunga yamewakera watu wengi tu na
yeyote atakayekuja baada yake, ataonekana alikuwa nyuma ya mpango huo haramu. Watu
hawawezi kusahau, kwamba ili kumuondoa Nchunga madarakani, ilibidi Yanga
ifungwe 5-0 na Simba. Matusi makubwa hayo kwa wana Yanga.
Dhambi hii peke yake, itamuhukumu yeyote atakaytekuja baada
ya Nchunga. Lakini hata Nchunga naye hajajiuzulu kwa kupenda, amelazimika
kutokana na hekima na busara yake kumtuma kufanya hivyo, ili kuinusuru klabu.
Marehemu baba yangu alikuwa Yanga mzuri sana, na alifariki
mwaka 2001 akiwa ana umri wa 98. Nakumbuka aliwahi kuniambia; “Tangu ule
mgogoro uliomkimbiza Mzee Mangara, klabu yetu haijawahi kutulia na sijui kama
haya yataisha,”.
Wakati huo anasema hivyo ilikuwa kipindi ambacho kuna
mgogoro wa kumuondoa madarakani Matunda. Marehemu baba yangu alikuwa Yanga yule,
ambaye starehe yake kufungwa Simba tu, hata timu ifungwe ligi nzima, lakini
yeye anataka mnyama auwawe tu.
Nakumbuka miaka ya 1990, wanachama fulani walikwenda kumuangukia
mzee Mangara na wakamrejesha Jangwani, lakini umri ulikuwa umekwishaenda sana. Hata
alipofariki dunia, alizikwa vizuri na wana Yanga.
Lakini bado kuna maneno ya pembeni pembeni yanazungumzwa
kwamba Yanga ina laana ya waasisi wake, akina Mangara. Najua hapa kuna baadhi hawatanielewa,
acha nizame ndani kidogo;
Mwaka 1975, Yanga ilitwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa
Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame, ikiifunga Simba kwenye fainali
mabao 2-0 visiwani Zanzibar. Wafungaji wa mabao hayo walikuwa wale wale wauaji
wa fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa mwaka 1974, Uwanja wa Nyamagana mjini
Mwanza, Sunday Manara na Gibson Sembuli (marehemu), katika ushindi wa 2-1, bao
la Simba likifungwa na Adamu Sabu (sasa marehemu).
Lakini kwa sababu wachezaji wengi waliitumikia Yanga tangu
miaka ya 1960, Mangara akawasilisha mchakato wa mapinduzi katika timu, akiamini
wachezaji walipo wamezeeka, ila hakueleweka kwa sababu timu ilikuwa ina matokeo
mazuri.
Kipindi hicho wakongwe wa Yanga walikuwa akina Elias Michael
'Nyoka Mweusi', Muhidini Fadhili na Patrick Nyaga, wote makipa, mabeki Boy Iddi
Wickens, Athumani Kilambo 'Baba Watoto', Badi Saleh, Hassan Gobbos, Omar
Kapera, viungo Abdurahman Juma, Abdurahman Lukongo, Sunday Manara 'Computer',
Leonard Chitete, na washambuliaji Gibson Sembuli, Kitwana Manara 'Popat' na
Maulid Dilunga.
Wakati huo huo, kulikuwa kuna kundi la vijana wanategenezwa
pale Yanga, akina Juma Pondamali, Mohamed Rishard ‘Adolph’, Mohamed Yahya ‘Tostao’,
Leodegar Chilla Tenga, Jellah Mtagwa, Juma Matokeo, Kassim Manara na wengineo,
maarufu kama Watoto wa Dk Victor Stanslescu, ambao ilikuwa ndio warithi mikoba
ya wakongwe.
Lakini pamoja na ubishi huo, baada ya kushindwa kutetea
Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki mjini Mombasa, Kenya, uliibuka mgogoro
mkubwa na wa kihistoria ndani ya klabu hiyo.
Yanga ilianza vizuri tu katika kundi lake B, ikiifunga 2-1
Mseto SC ya Morogoro, kabla ya kuitandika Green Bufalloes ya Zambia 2-0, Bata
Bullets ya Malawi 3-1, iliongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Mseto, mabingwa wa
Tanzania mwaka 1975.
Katika Nusu Fainali, Yanga iliifunga 3-0 Express ya Uganda
wakati Mseto iliona cha mtema kuni kwa Luo, baada ya kutandikwa 5-0. Yanga
iliuacha ubingwa Mombasa, baada ya kulala 2-1 kwa Luo kwenye fainali.
Timu iliporejea nyumbani, mgogoro ukaibuka, wanachama
walikuja juu na kutaka kumpiga Mwenyekiti wao wakati huo, mzee Mangara, ambaye
aliokolewa kwa kutoroshewa mlango wa nyuma.
Vyanzo vinasema kwamba, wanachama walifika na bakora
Jangwani wakitaka kumchapa Mangara. Walikuwa wanataka hesabu za mapato na
matumizi ya klabu, lakini walikuwa wenye ghadhabu wakifanya fujo, hivyo ili
kuepuka balaa hilo, Mangara alitoroshwa na kuwaacha solemba waliokuwa
wanamsubiri nje wamchape bakora. Mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna
Yanga kwa miaka minne.
Kipindi hicho Yanga ilikuwa safi kiuchumi, ilikuwa ina
mabasi matano yaliyokuwa yakiingizia fedha klabu, Uwanja wa Kaunda uliojengwa
kwa mkopo wa Sh 500,000 wa Benki ya Nyumba (THB) ulikuwa bado mpya unavutia
watu wengi wakati wa mazoezi ya timu hiyo.
Yanga ilisaidiwa pia fedha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Abeid
Karume kiasi cha Sh milioni 2.7 kwa ajili ya ujenzi.
Aidha, Yanga ilikuwa ina mfadhili wake, aliyekuwa
akiwasaidia fedha nyingi, Shiraz Sharrif, ingawa naye baada ya mgogoro alihamia
Pan African, kwa sababu alikuwa ana imani na Mangara.
Kutokana na jinsi Mangara alivyoishi vizuri na wachezaji wa
klabu hiyo, alikuwa akiwapenda akiwafanya marafiki, basi wachezaji wote
waliamua kumfuata na kuachana na Yanga. Walifikia hatua hiyo, baada ya jitihada
za kushinikiza Mangara arejeshwe, ikiwemo kuandamana, kushindikana. Kwa jeuri,
Yanga nayo ilisema acha waende na itaunda timu mpya.
Hadi leo, ukiwauliza watu wa Yanga sababu za kugombana na
mzee Mangara, wapo watakaosema wanachama walikuwa wakorofi na wengine watasema
mzee huyo alikuwa akinufaika kwa kupitia mgongo wa Yanga.
Katika sakata hilo, wachezaji wakongwe waliokuwa Yanga ili
wasikae bure msimu wa 1976, walikwenda Morogoro kujiunga na klabu iliyokuwa
ikiitwa Nyota Afrika, wakafanikiwa kuipandisha daraja, wakati wachezaji
chipukizi awali walikwenda kujiunga na timu ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL),
iliyokuwa ikiitwa Breweries wakati huo.
Lakini baadaye wachezaji waliokwenda Nyota walirejea Dar es
Salaam kuungana na wadogo zao, kuanzisha timu iliyokuja kuwa tishio kwenye soka
ya Tanzania, Pan African. Timu hiyo ilianzishwa chini ya Mangara, aliyekuwa
Mwenyekiti wa kwanza klabu hiyo.
Mbali na Mangara, wengine walioasisi timu hiyo ni Omar
Muhajji, Sammy Mdee, Shiraz Sharrif, aliyekuwa mfadhili wa Yanga ambaye
alihamishia noti zake kwa klabu ya Mtaa wa Swahili.
Kihistoria huo ulikuwa mgogoro wa kwanza Yanga na tangu
wakati huo migogoro imekuwa sehemu ya maisha ya klabu hiyo. Sitaki kuamini kama
wanavyoamini wengine, kwamba Yanga ina laana ya waasisi wake. Bali nachoamini,
ipo haja ya kuuangalia upya mustakabali wa klabu, ikiwa hata Katiba mpya
madhubuti, zilizotayarishwa kutokana na ushauri wa FIFA, haziwezi kuheshimiwa
Yanga na watu wapo tayari klabu ife.
Nilimsikia Mzee Akilimali anasema Yanga itahamia Zanzibar. Kama
hajui, hata Zanzibar ipo chini ya FIFA, haina uanachama kwa sababu ni sehemu ya
Tanzania- ila kwa kuwa wanachama wa CAF, lazima wafuate mwongozo wa wenye soka
yao, FIFA.
Kwa hiyo asikate kuwadanganya watu kwamba, atakaidi agizo la
FIFA kupitia TFF- halafu akawe mwanachama wa ZFA. Hakuna kitu kama hicho. Wadau, TFF na serikali- umefika wakati sasa
mustakabali wa klabu hii utazamwe upya.
Nasema hivyo kwa makusudi, kwa sababu kuna harakati
zinaendelea pale- iwapo watu watatulia na kuacha ziendelee, nahofia zinaweza kufuta
historia ya klabu na jengo la klabu pale Jangwani, likabaki kijiwe cha kuchezea
dhumna, drafti na kupiga majungu. Wasalaam.
0 comments:
Post a Comment