Hussein Javu katikati kwenye mazoezi wa Stars, akiwatoka Ramadhan Chombo kushoto na Juma Nyosso kulia |
Mtibwa, mabingwa wa Tusker 2009 |
![]() |
Nizar Khalfan |
BARCELONA ya Hispania pamoja na kusifiwa kuwa klabu yenye
mafanikio makubwa na kutandaza soka safi kwa sasa- lakini pia ina sifa moja ya
ziada ambayo ni kuwa klabu inayozalisha wachezaji wengi bora.
Hata katika wakati ambao Barcelona ilikuwa haiwiki kwenye
soka duniani, bado iliendelea kuzalisha wachezaji bora waliochukuliwa na klabu
kubwa Ulaya wakiwa makinda- mfano Fabregas aliyekwenda Arsenal.
Hata Tanzania kuna klabu ambayo unaweza ukaibebesha sifa za
Barcelona, nayo ni Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Wachezaji wengi walio kwenye klabu kubwa Tanzania ama
waliibuliwa Mtibwa au walipitia chuo cha mafunzo, Manungu mfano kwenye kikosi
cha mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC utakutana na Juma Kaseja, Amir Maftah, Uhuru
Suleiman, Salum Machaku na Obadia Mungusa.
Yanga pale utakutana na Kiggi Makasy, Pius Kisambale, Kiggi Makassy, Shaaban Kado na Julius Mrope, wakati Azam, FC wanaye Deo Munishi ‘Dida’.
Bado hujamtaja kiungo Nizar Khalfan, aliyechezea klabu za Vancouver
Whitecaps na Philadelphia Union za Marekani, au Idrisa Rajab anayekipiga
Sofapaka ya Kenya.
Unaizungumzia klabu yenye maskani yake kjijiji cha Madizini,
tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero, kiasi cha kilomita 100 kutoka Morogoro
mjini, ambayo ilianzishwa mwaka 1988 na kikundi cha wafanyakazi wa kiwanda cha
sukari cha Mtibwa, Mtibwa Sugar Estates Ltd.
Timu hiyo ilianza kushiriki Ligi ya Wilaya Daraja la Nne
mwaka 1989 na iliendelea vizuri hadi kupanda Daraja la Kwanza 1996, ambayo
mwaka 1998 ilibadilishwa na kuwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Mwaka 1998, kiwanda hicho kilinunuliwa na kampuni ya
Tanzania Sugar Industry, ambao waliifanya klabu hiyo kuwa tishio, wakianza kwa
kufanya usajili wa kishindo, wakichukua nyota wa klabu za Simba na Yanga.
![]() |
Kado |
Monja Liseki, Yussuf Macho, Mwanamtwa Kihwelo, Ally Yussuf
‘Tigana’, waliokuwa Yanga mwaka huo, Geofrey Kikumbizi aliyekuwa Majimaji
walishuhudiwa msimu wa 1999 wakivaa jezi za Mtibwa. Mwishoni mwa msimu, Mtibwa
iliwaongeza Duwa Said, Abdulmalik Nemes kutoka Simba, Kassim Issa aliyekuwa
Zanzibar na Zuberi Katwila aliyerejea kutoka Ubelgiji kucheza soka ya kulipwa.
Wakali hao waliungana na nyota walioipandisha Mtibwa kama
Mecky Mexime, Hassan Mbarouk, Odo Nombo, Reuben Mgaza, Kassim Mwabuda, Mao
Mkami ‘Ball Dancer’, Vincent Peter, Rajabu Msoma chini ya kocha John
Simkoko.
Mtibwa Sugar ambayo kwa sasa inafundishwa na Mkenya, Thom
Olaba, imekuwa na sera ya kuinua vipaji, ambavyo baadaye vinapapatikiwa na
klabu kongwe za Simba na Yanga.
Lakini zaidi, Mtibwa ina mchango mkubwa katika timu ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars, kwani imekuwa ikitoa wachezaji wengi kwa ajili ya
timu hiyo.
Mtibwa Sugar, inayojulikana kwa jina la utani kama Wakata
Miwa wa Manungu, ni miongoni mwa klabu chache nchini zinazojivunia mafanikio
ambayo siri yake ni uongozi bora na mfumo bora wa utawala.
Lengo la Mtibwa ni kuwa timu imara na yenye mafanikio zaidi
kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Na kwa sababu hiyo, wakati wote Mtibwa imekuwa yenye
maandalizi mazuri chini ya makocha wa viwango vya juu. Mafanikio ya Mtibwa
Sugar hadi sasa ni kuwa timu ya tatu kutoka nje ya Dar es Salaam kuwahi kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa misimu miwili mfululizo, 1999 na 2000.
![]() |
Kaseja |
Hiyo ni timu pekee nje ya Simba na Yanga kuwahi kutetea
ubingwa wa Ligi Kuu, ingawa kwa sasa cheche zake zimefifia.
“Unajua wakati ule tulikuja kwa kishindo sana, hadi tukaitwa
Magalactico (Real Madrid) wa Manungu, lakini ule ulikuwa ni mwanzo tu ili kutafuta
namna ya kupata mashabiki. Ila baada ya hapo sera yetu imekuwa kuinua vipaji.
Na tunashukuru kwa asilimia 80 tumefanikiwa. Karibu kila
msimu tunauza wachezaji si chini ya wawili kwenda Simba na Yanga. Msimu huo
uliomalizika pia, SImba walichukua wachezaji wawili kwetu, Salum Machaku na
Obadia Mungusa, Yanga nao waliwachukua Mrope na Kado.
Bado kuna wachezaji wetu waliong’ara msimu huu ambao hizo
klabu zinawatolea macho mfano Juma Abdul na Hussein Javu. Wote hawa wanatoka
timu ya vijana ya Mtibwa katika mradi wetu wa soka ya vijana, ambao ni imara
sana. Tunasikitika vyombo vya habari haviuzungumzii, labda kwa sababu tupo
kijijini kule, lakini mbona matunda yake yanaonekana?”anasema Mratibu wa Mtibwa
Sugar, Jamal Bayser katika mahojioano na BIN ZUBEIRY leo mchana ofisini kwake,
Superdoll, barabara ya Nyerere, zamani Pugu, Dar es Salaam.
Tangu watwae ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo,
Mtibwa imekuwa timu tishio katika soka ya Tanzania na inavipasua kichwa haswa
vigogo, Simba na Yanga. Haijawahi kutetereka, licha ya kusajili wachezaji
mahiri, kuwa na mpango mzuri wa kuinua chipukizi, pia imekuwa ikiajiri makocha
wa kigeni.
Miongoni mwa makocha wa kigeni waliowahi kufanya kazi
Manungu ni Raoul Shungu, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Olaba,
Twahir Muhiddin na James Siang’a kutoka Kenya.
Mwaka 2009, Mtibwa Sugar ambayo ni timu nyingine yenye
Uwanja wake, Manungu baada ya Azam na Yanga inayomiliki ‘Uwanja mbovu’ wa Kaunda,
ilitwaa Kombe la Tusker, linaloshirikisha timu za Afrika Mashariki na mwaka juzi
ilitwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga 2-1.
Lakini cheche za Mtibwa zimefifia, Bayser anasemaje? “Fitina
zimezidi katika soka hii, rushwa imetawala mno, sisi hatuwezi kuhonga, tunataka
kushinda kwa uwezo. Kwa mfano msimu huu ulioisha dhamira yetu ilikuwa ubingwa,
ila soka ya nchi hii imeharibika mno hivi sasa,”anasema.
Hata hivyo, Bayser aliyewahi kuwa Makamu wa pili wa rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika awamu ya kwanza ya Utawala wa Leodegar
Chilla Tenga, anasema wanajipanga na wanaachana na sera za Arsene Wenger za
kuuza wachezaji bora wa timu. “Hatuuzi mchezaji tena, tunataka ubingwa msimu
ujao, tutahakikisha kila mchezaji tunayemuhitaji haondoki ili aisaidie timu.
Tayari Javu ambaye alikuwa amemaliza Mkataba, tumemuongezea
ili kuhakikisha haondoki,”anasema Bayser. Hao ndio Mtibwa ambao wana sifa za
Barcelona, mabingwa wa soka wa dunia.
Jamal Bayser kulia, akiwa na Ofisa mwenzake wa kampuni ya Superdoll na sanamu ya Michellin, moja ya bidhaa za kampuni yao, kampuni tanzu ya Mtibwa Sugar. |
0 comments:
Post a Comment