SIMBA, SHANDY WAINGIZA MIL.216
WAKATI mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) baina ya Simba na Al Ahli Shendi ya Sudan ukiingiza shilingi milioni 216,kikosi cha Simba kinaendelea na maandalizi yake ya mchezo wake wa mwisho wa ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Yanga utakaopigwa jumamosi hii kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mamapipiro blog kwa simu kutoka Visiwani Zanzibar ambapo timu imepiga kambi, msemaji wa Simba Ezeckiel Kamwaga alisema kwamba kikosi chao ambacho kimepiga kambi eneo la Mbweni kipo katika hali nzuri na kinafanya mazoezi katika uwanja wa Fuoni.
Aliongeza kuwa wamepania kushinda mchezo huo ili kulipiza kisasi cha kufungwa bao 1-0 na mahasimu hao katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ambayo Simba inaongoza kwa pouinti 59 ikifuatiwa na Azam Fc yenye pointi 56 na Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46.
NCHUNGA APEWA LAANA
BARAZA la wazee la klabu ya Yanga limesikitishwa na kauli za kejeli na zenye kuwadhalilisha alizozitoa mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga juzi, hivyo kuanzia sasa wamemwachia aendelee na timu hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Nchunga kudai kuwa wazee hao walikurupuka na hawezi kukabidhi kwa wahuni, pia sehemu ambapo hana uhakika na usalama, huku akihofu timu hiyo kuhudumiwa na wauza dawa za kulevya.
Wakizungumza na mamapipiro blog leo asubuhi wazee hao wakiongozwa na katibu wao Ibrahim Akilimali walisema kwamba hawakukupupuka kutangaza kuichukua timu bali walikubaliana na Nchunga, lakini wanashangaa baadaye kuwageuka.
“Hatukukurupuka kuongea vile, ilikuwa ni ridhaa ya Nchunga, tulikuwa sahihi kutokana na mapenzi yetu na timu, pamoja na kuwa uongozi ndio una haki tuliikubaliana kuichukua timu kwa lengo la kuhakikisha inaifunga Simba, tunafanya usajili wa uhakika na kurejesha nidhamu,”alisema.
“Ni ajabu kwa Nchunga kututamkia sisi wauza unga, inamaana mama Fatma Karume, Francis Kifukwe, Seif Ahmed, Abdallah Binkleb na Yusuf Manji ni wauza unga?
...hivi Nchunga anajua umuhimu wa hawa watu ndani ya Yanga,tena kwa mshangao mkubwa amediriki hata kutuma watu wamzuie kuingia klabuni mzee Kitundu (Jabir)ambaye alishiriki kuijenga klabu,”alisema Mzee Akilimali.
Naye mjumbe wa baraza hilo, Yussuf Mzimba pamoja kusikitishwa na kauli za Nchunga, alisema Yanga ina wenyewe na kwamba ukifuga kuku wengi lazima utapata aliye kisirani ambao wanajifanya wanajua kumbe si lolote.
“Tunataka serikali iangali watu kama hawa, Nchunga hawezi kutukana watu kama kina mama Karume, inaonekana klabu imemshinda kwani aliingia madarakani kwa bahati tu na matokeo yake kaleta mgawanyiko badala ya umoja”,alisema mzee Bilal Chakupewa.
Aidha Mzee Chakupewa aliongeza kwamba hata kama wakiifunga Simba jumamosi Nchunga ni lazima aondolewe madarakani kutokana na udhaifu aliouonyesha kwenye uongozi wake na kuifikisha Yanga mahala pabaya.
MABONDIA WAWILI WATANZANIA WATINGA HATUA YA ROBO KATIKA MASHINDANO YA KUFUZU KUELEKEA OLIMPIKI YANAYOENDELEA CASSABLANCA, MOROCCO.
Mobondia wa timu ya taifa waTanzania Selemani Kidunda 69 kgs welter weight na Emillian Patrick 56 kgs bantam weight wamesonga mbele katika mashindano ya kufuzu kuelekea katika kushiriki mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika London Uingereza,katika mashindano yaliyoanza tarehe 28/4-5/5/2012 Casablanca Morocco.
Mabondia hao wamefika hatua hiyo baada ya kushinda mapambano yao ya awali kwa seleman Kidunda kumshinda Kab Thiam wa Senegal kwa RSC na Emillian Patrick kumshinda Tewodros Tilahun wa Ethiopia.
Mabondia hao sasa wamefika katika hatua ya robo fainali ambapo ni jumla wa mabondia nane waliofikia hatua hiyo na idadi inayotakiwa kufuzu ni mabondia sita kwa kila uzito.
Mabondia hao kesho tarehe 2/5/2012 watapanda ulingoni kwa Emillian Patrick kucheza na Isaac Dogboe wa Ghana na Seleman Kidunda atacheza na Mehdi Khalsi wa Morocco .
Endapo watashinda watakuwa wameingia hatua ya nusu fainali na tayari watakuwa wamefikia hatua ya kupata medali ya shaba .
Tanzania ilipeleka jumla ya wachezaji wanne na viongozi wawili wachezaji wawili Victor Njaiti na Abdalah Kassim walitolewa katika hatua za awali. viongozi walioambatana na timu ni Michael Changarawe na Remmy Ngabo.
Aidha kesho kutafanyika mkutano mkuu wa Shirikisho la ngumi la Afrika (AFBC) Tanzania katika mkutano huo itawakilishwa na makamo wa Rais wa BFT Michael Changarawe
Kwa niaba ya BFT tunawaomba watanzania wote kila mmoja kwa imani yake kuwaombea ili washinde na wafuzu kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa kuzingatia kuwa kwa upande wa ngumi tulishiriki olimpiki kwa mara ya mwisho mwaka 1996 Atlanta.
Makore Mashaga
Katibu Mkuu (BFT)
0 comments:
Post a Comment