Kikosi cha Simba msimu huu |
USIKU huu, klabu Simba imeshindwa kutimiza
ndoto za kusonga mbele kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, baada ya
kutolewa kwa penalti 9-8 na Al Ahly Shandy ya Sudan kufuatia sare ya jumla ya 3-3.
Simba ilihitaji kufungwa si zaidi ya mabao
2-0 ili isonge mbele, baada ya awali kushinda 3-0 nyumbani.
Kama ingepita hatua hii, Simba ingecheza na
moja ya timu zilizotolewa kwenye hatua kama hii, 16 bora Ligi ya Mabingwa
Afrika, kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Katika uhai wa soka ya Tanzania, haijawahi
kuingiza timu kwenye hatua hiyo ya Kombe la Shirikisho na kama SImba
ingefanikiwa ingekuwa ya kwanza.
KWA NINI IMETOLEWA?
Lazima swali hilo liwepo- kwa sababu Simba
ilikuwa imekwishapiga hatua kubwa baada ya kushinda 3-0 nyumbani, lakini
imetolewa- je kwa nini?
Zinaweza kuja sababu nyingi kutoka kwa wao
wenyewe Simba, kubwa hujuma za wenyeji wao, hila- marefa kuwapendelea Shandy-
lakini zote nasema hazina msingi.
Hazina msingi kwa sababu, Simba ilishiriki
kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika mwaka 1974 na leo hii ni miaka 38
baadaye.
Katika ushiriki wake wa kwanza michuano ya
CAF, SImba ilicheza Klabu Bingwa Afrika na ikafika hadi Nusu Fainali, ambako
ilitolewa na Mehallal El Kubra ya Misri.
Raundi ya kwanza, Simba iliitoa Linare ya Lesotho,
raundi ya pili ikaitoa Zambian Army ya Zambia na katika Robo Fainali ikaitoa Hearts
Of Oak ya Ghana
Hii ni timu yenye uzoefu mkubwa- haijalishi
viongozi wake wana uzoefu gani- kwa sababu wamerithi madaraka kwa lengo la kuendeleza
historia ya klabu, maana yake waliomba kufanya kazi ambayo wanaijua.
Kwa uzoefu wake, SImba si ya kulalamikia
hujuma kwenye mechi za ugenini, kwa sababu hata na wao wanapocheza nyumbani hufanya
mambo yao, ili kuwadhoofisha wapinzani wao- kadiri ya uwezo wao.
KUJIAMINI KUPITA KIASI:
Simba, baada ya kushinda 3-0 nyumbani, wakaamini
kazi imeisha na walijipa matumaini hata kama kufungwa haiwezi kuwa zaidi ya
2-0.
Waliona hazina ya mabao 3-0 ni kubwa- lakini
narejea pale pale kwenye uzoefu- kama wangezingatia wasingethubutu kubweteka na
ushindi wa 3-0 nyumbani.
Kwa nini? Mwaka 1979 Simba ilianza vibaya
Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa, enzi hizo ikiitwa bado Klabu Bingwa,
baada ya kufungwa mabao 4-0 nyumbani, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Mufulira
Wanderers ya Zambia, lakini katika mchezo wa marudiano, ikaenda kushinda 5-0
ugenini.
Hivyo kama wangerejea kwenye uzoefu-
wangekumbuka hili na wangejipanga sawa sawa kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Hujuma na hila za Wasudan; hili ni geni kwa
Simba? Mwaka 1994 Simba ilikwenda kucheza na El Merreikh nchini humo na ikafanyiwa
vurugu hadi wachezaji wake kupigwa.
Huu ulikuwa uzoefu tosha kwa Simba juu ya
Sudan. Wasudan wamechanganyikiwa na soka na hawana mzaha- unapokwenda kwao
kwenye mashindano jua kabisa unakwenda kwenye vita na hii ndiyo maana imekuwa nchi
yenye mafanikio zaidi kisoka katika nchi wanachama wa CECAFA.
Sasa leo Simba ni wa kulia na hila au
hujuma za Wasudan? Iko wapi maana au faida ya uzoefu wao kwenye mashindano ya
Afrika?
Narudi kule kule, kujiamini kupita kiasi
kulifanya wakapuuza umuhimu wa kutumia uzoefu wao katika kujipanga kwa mchezo
huo.
Zaidi walikumbuka waliitoa ES Setif kwa
faida ya bao la ugenini kupata ruhusu ya kucheza na Shandy- wakajua watawatoa
tu na Wasudan hao, bila hata ya kutengeneza mazingira ya kuwatoa.
Refa aliwauma kweli Simba, lakini
walichukua tahadhari gani kabla ya mchezo huo? Au tuseme ushindi wa 5-0 dhidi
ya Yanga uliwalevya?
WALIMUONEA AZIM DEWJI 1993
Mwaka 1993, SImba ilianza kwa sare ya bila
kufungana na Stella Abidjan ya Ivory Coast ugenini katika fainali ya Kombe la
CAF, lakini katika marudiano pamoja na wachezaji kuahidiwa na mfadhili wa klabu
hiyo, Azim Dewji zawadi ya gari aina ya KIA kila mmoja wakitwaa Kombe hilo,
wakafungwa 2-0 nyumbani kwenye mechi ya marudiano.
Baada ya matokeo, hayo uvumi ukaenea eti
Dewji aliihujumu timu kukwepa kutimiza ahadi yake ya kutoa KIA.
Pamoja na hayo Dewji aliwapa gari ndogo
aina ya Corolla wachezaji wa klabu hiyo pamoja na kufungwa kama kifuta jasho.
Tunasemaje leo, nani kahujumu SImba Sudan wakati
hakukuwa na ahadi yoyote iliyotolewa hadi timu inaingia uwanjani?
Mwaka 2007, Simba ilianza kwa sare ya 1-1
ugenini katika Kombe la Shirikisho na dhidi ya Textil de Pungue ya Msumbiji- na
wakihitaji sare ya 0-0 ili wasonge mbele, wakatolewa kwa penalti 3-1 nyumbani,
baada ya sare nyingine ya 1-1.
Naikumbuka sana mechi hii iliyochezwa Januari
28 na marudiano yalikuwa Februari 11, kwani ndiyo siku ambayo aliaga dunia
mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Said Nassor Mwamba 'Kizota'.
Kizota aliyechezea pia Yanga kwa kipindi
kirefu zaidi, aligongwa na gari kwenye kituo cha mafuta, eneo la Veterinary, Temeke
mjini Dar es Salaam akitoka kuangalia mechi hiyo na kufariki dunia baada ya
kufikishwa hospitali ya Temeke.
KAUGONJWA SUGU KANAKOHITAJI TIBA:
Kuna kaugonjwa sugu ndani ya SImba, ambako
kanahitaji tiba ya haraka, tena haraka sana. Kubweteka baada ya matokeo mazuri
ya awali.
Inatosha sasa, SImba imekwishapata uzoefu
wa kutosha na kinachotakiwa kwa sasa ni kuzingatia- kuliko kujiandaa kurudia
hadithi zile zile za; ‘tulihujumiwa, tulionewa na marefa’.
Moja kati ya kauli nilizowahi kusikia
kutoka viongozi wa soka nchini na nadhani siwezi kuzisahau, ilitoka kwa
aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Tarimba Gulam Abbas mwaka 2001.
Tarimba alilalamikia timu yake kuonewa na
marefa hadi ikakosa ubingwa wa Bara mwaka huo na akasema, kuanzia wakati huo
angekuwa akisajili wachezaji wazuri mno na kuiandaa timu vizuri, ili hata kama
wakionewa wafanye vizuri tu kwa ubora wa timu yao.
Na hivi ndivyo wanavyofanya TP Mazembe ya
DRC hata sasa imekuwa tishio kwa timu za Kaskazini mwa Afrika.
Mapema asubuhi niliwasilisha makala, SImba
na Yanga tajiri kuliko Bakhresa, mmiliki wa Azam FC- kwa waliosoma watakumbuka
nilizungumzia usajili wa Simba wa kubahatishaa bahatisha, ambao faida yake imeishia
kuifunga Yanga 5-0 na kutwaa ubingwa wa Bara. Michuano ya Afrika hakuna lolote.
WAMEJIFUNZA NINI SASA?
Wametolewa- kwa vyovyote, iwe kuonewa au
kihalali- lakini huwezi kuona bao la kulalamikia kati ya mabao ya Shandy. Yote yalikuwa
halali. Lakini bado tu wameonewa na wamefanyiwa hila. Kama Simba hawajui home
advantage uko wapi uzoefu wao wa michuano ya Afrika?
Soka ni mchezo wa furaha na marefa mara
nyingi huwa hawapendi kuwaudhi mashabiki wa nyumbani kwa sababu wanajua hata
timu inapigana kwa ajili hiyo, hivyo ukiwa nyumbani kwako hata bila
kuwakaribisha chakula cha usiku wanaweza kukupa home advantage.
Hivyo Simba hawapaswi kulia na marefa ambao
hawakuruhusu bao hata moja la offside.
Kitu cha msingi kwa SImba hivi sasa, kwanza
ni kukubali matokeo na pili kufanyia tathmini ushiriki wao wa mwaka huu kuanzia
mwanzo hadi walipokomea.
Lakini warejee msimu mzima huu, kuanzia
kwenye kusajili timu, kuiandaa na hadi kuiingiza kwenye mashindano, walikosea
wapi?
Wanapaswa kufanya hivyo, kwa sababu kutolewa
na Shandy mwaka huu si mwisho wa maisha yao ya soka na mwakani wapo tena, tena
kwenye michuano mikubwa kuliko waliyoshiriki mwaka huu. Ligi ya Mabingwa.
Wamejifunza nini? Wanajipangaje? Au kinachofuata ni kufukuza wachezaji na kocha
kisha kuanza upya? Kuanza upya kila mwaka! Lini tutafikiria kuendeleza?
Nachopenda kuwaambia Simba, kutolewa na
Shandy siyo mwisho wa maisha yao ya soka- wachukulie hilo kama fundisho na
baada ya hapo wajipangaje kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa mwakani.
AZAM PIA WAJIFUNZE:
Wakati SImba ikicheza Ligi ya Mabingwa mwakani,
katika Kombe la Shirikisho Tanzania itawakilishwa na Azam FC.
Azam ni timu changa na mwakani ndio
watakuwa wakicheza kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika baada ya miaka minne
ya kucheza Ligi Kuu ya Bara.
Hawana uzoefu kama timu, lakini wakichukulia
uzoefu wa makosa ya kila mwaka ya SImba na Yanga, wakatumia kama changamoto
kwao, hawatakuwa na uchanga tena.
Mechi ya CAF inaisha baada ya filimbi ya
mwisho ya mchezo wa marudiano. Kuna hila na hujuma za ugenini na wakati
mwingine unaweza kukumbana nazo hadi uwanjani. Wasalam. BIN ZUBEIRY.
0 comments:
Post a Comment