MWENYEKITI wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alex Mgongolwa (pichani kulia) amesema katika
kikao chao cha jioni ya leo, wameshindwa kuamini kwamba Mwenyekiti wa Yanga,
Wakili Llod Baharagu Nchunga amejiuzulu
na wameomba uthibitisho kutoka kwa sekretarieti ya klabu hiyo, ili wachukue hatua
zaidi katika kutatua mgogoro unaoendelea kwenye klabu hiyo.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY hivi punde, Mgongolwa
amesema kwamba bado wanaendelea kusistiza Yanga wafuate Katiba yao katika hilo.
“Tumeomba watuletee rekodi za Wajumbe waliojiuzulu, watatupatia
kesho, tukishapata tutawapa mwongozo kwa mujibu wa Katiba,” alisema Mgongolwa.
Akizungumzia kitendo cha Nchunga kusema anaikabidhi timu kwa
Baraza la Wadhamini wa klabu baada ya kujiuzulu, Mgongolwa alisema katika hilo
yuko yuko sahihi, ila akasema Wajumbe wote ambao bado hawajajiuzulu nyadhifa
zao bado wanatambuliwa kama Wajumbe halali na wanapaswa kutambuliwa.
Baraza la Wazee Yanga |
Mapema leo mchana, kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga
kujadili barua ya Nchunga kujiuzulu kilishindwa kufanyika, kutokana na safu
kutotimia.
Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa aliiambia BIN ZUBEIRY mchana kwamba, Mbaraka
Igangula yupo Afrika Kusini wakati Khalifa Mgonja yupo Arusha,
Mwesigwa alisema kwa sababu hiyo, wanasubiri Wajumbe wote wa
Kamati ya Utendaji wafike Dar es Salaam ndipo kikao kifanyike. Wakati huo huo,
Wazee wa klabu hiyo walikutana na waandishi wa Habari leo mchana makao makuu ya
klabu na kusema kwamba, hawamtambui Mjumbe yeyote wa Kamati ya Utendaji, kwani
Nchunga ameondoka na watu wake wote.
Aidha, baadhi ya Wajumbe waliotangaza kujiuzulu wameanza
kuzikana barua zao, wakidai walilazimika kuandika kutokana na vitisho
walivyokuwa wakipewa.
Jana, Nchunga (pichani kushoto) alitangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Yanga,
akisema timu anaikabidhi kwa Baraza la Wadhamini, ambalo kwa sasa linaundwa na
wajumbe watatu, Mama Fatuma Karume, Deo Filikunjombe na Francis Kifukwe.
0 comments:
Post a Comment