Matajiri ndiyo maadui wa maendeleo ya soka Tanzania | Send to a friend |
Monday, 30 April 2012 14:29 |
MARA kwa mara tumekuwa tukiilaumu Serikali kwa kushindwa kuboresha sera yake ya michezo nchini ili kuweza kuwa na sera imara ya michezo ambayo itahakikisha tunakuwa na michezo ya kulipwa na ridhaa kwa ajili ya maendeleo ya michezo nchini. Kwa upande mmoja ni sawa, lakini kwa upande wa pili wapo wanaoitwa wadau wa michezo ambao wanalo jukumu la kupigania uboreshwaji wa michezo nchini kwa hali na mali kwa kushirikiana na vyama husika vya michezo. Nimeonyesha umuhimu wa Serikali na wadau, lakini leo nimeamua kuwachambua wadau matajiri waliopo kwenye mchezo wa soka na ambao hawajajitokeza katika mchezo huo. Mchezo wa soka ni burudani na kazi pia. Wachezaji wa soka wanajifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na mazoezi,mbinu,nidhamu,kuelewana katika kiwango cha juu na mambo mengi mengine. Kiujumla soka ni mchezo unaohitaji ujuzi na kipaji. Ili ujuzi na vipaji vya wachezaji wa soka viweze kushamiri wachezaji wanahitaji walipwe vizuri na mchezo wa soka wenyewe udhaminiwe na kusaidiwa kwa uhakika na ili hayo yaweze kufanikiwa ndipo linapokuja suala la wadau wa soka ambao ni matajiri. Upo wakati kundi maarufu katika klabu ya Simba linaloitwa Friends of Simba lilitaka kujitoa kusaidia klabu hiyo kwa sababu ya kushindwa kuelewana na viongozi watendaji wa klabu hiyo kwa sababu viongozi walikataa kuyumbishwa na kundi hilo ambalo huifadhili Simba. Leo hii Yanga kumezuka mgogoro,hii ni kwa sababu watu waliokuwa wanawafadhiri wamekaa mbali na timu hiyo na kuiacha yatima kwa sababu moja au ile. Wapo matajiri wengi wamejitokeza kuzifadhiri baadhi ya klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini kwa kiasi kikubwa ufadhiri wao haujaleta mabadiliko katika soka la Tanzania.Ni wazi kuwa ufadhiri unaofanywa na matajiri wa Tanzania unawasaidia matajiri kujenga majina yao na kuonekana watu maarufu sana kuliko hata wachezaji wenye kipaji na ujuzi wa kucheza soka. Pia ufadhiri unaofanywa na matajiri hao unalenga zaidi kujikuza wao kibiashara na biashara zao kuwa na majina makubwa kuliko klabu wanazofadhiri. Kinachoshangaza zaidi ni kuona matajiri wanavyokuwa na sauti kwenye timu wanazozifadhiri kuliko wanachama na viongozi wa timu waliochaguliwa na wanachama eti kwa sababu matajiri wametoa fedha za usajili au wamefadhiri masuala kadhaa kwenye timu. Jambo la msingi ni matajiri kuacha kutumia soka kukuza majina yao na biashara zao badala yake wale wote wanaojiona ni matajiri katika soka ya Tanzania waitishe mkutano na kuangalia mchezo huu unahitaji nini na kwa kutumia nguvu yao ya fedha waweze kutengeneza mkakati ambao utabadilisha na kuboresha soka ya nchi hii na kuwasaidia Watanzania wengi, badala ya kujinufaisha wenyewe ambao ni matajiri wachache. Hili litawezekana kwa tajiri mmoja kati ya wanaojiita matajiri katika soka kuitisha mkutano wa matajiri wanaofadhiri klabu za soka za Tanzania na matajiri wengine ambao hawajajitokeza kudhamini soka ili kuweza kutengeneza mkakati wa kulinusuru soka letu ambalo kila kukicha linazidi kudidimia kutokana na kukosa mipango endelevu. Matajiri wanatakiwa kuelewa wao ndiyo wamelishika soka pia wao ndiyo wanaoliua soka letu kwa kutoa fedha ambazo haziwezi kuwasaidia wachezaji na hazisaidii maendeleo ya mchezo bali linakuza umaarufu wao matajiri, kwa sababu wapo pia matajiri wa soka nchini ambao wanatumia fedha kuwarubuni wachezaji wacheze chini ya kiwango au wafungishe timu zao. Jambo la kushangaza matajiri hao wa soka la Tanzania wamekuwa wakifurahia wanavyoshangiliwa, kunyenyekewa na kuabudiwa na baadhi ya viongozi wa klabu, wanachama na mashabiki ili hali wakifahamu soka haliendelei nchini. Upo umuhimu wa matajiri kuelewa soka ni biashara kubwa duniani ambayo huingiza fedha nyingi kuliko makampuni mengi duniani, lakini soka huitaji uwekezaji mkubwa pia. Matajiri wakikutana na kutengeneza mkakati endelevu wa kubadilisha soka letu ni dhahiri watapata sapoti kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), serikalini na kwenye vyombo vya habari, ambapo makampuni mengi yatajitokeza kudhamini vilabu na soka kwa ujumla wake. Siku zote tumekuwa tukisema, klabu za soka hapa nchini zinahitaji viongozi makini wenye uwezo wa kutengeneza mikakati thabiti ya kuzifanya ziweze kujitegemea. Shida kubwa kwa viongozi wa klabu hizo wanakuwa wameingia madarakani bila ya malengo thabiti na matokeo yake klabu zimekuwa zikitegemea mifuko ya watu binafsi kujiendeleza. Soka ya sasa imebadilika na ipo kibiashara hivyo viongozi lazima wawe na mbinu za kisasa kufikia malengo yanayotakiwa na wanachama na mashabiki, pia wakijiepusha kutumiwa na matajiri wachache. GAZETI LA MWANANCHI: |
0 comments:
Post a Comment